• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Mkalatusi una manufaa mengi ila pia adui wa vyanzo vya maji

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mkalatusi una manufaa mengi ila pia adui wa vyanzo vya maji

Na LEONARD ONYANGO

KERICHO ndiyo kaunti ya hivi karibuni kupiga marufuku upanzi wa miti aina ya mikalatusi (Blue Gum Eucalyptus) karibu na vyanzo vya maji.

Bunge la Kaunti ya Kericho lilipitisha hoja ya kupiga marufuku upanzi wa miti hiyo Jumanne iliyopita.

Mnamo Mei 2019 Gavana Paul Chepkwony aliwapa makataa wakulima kung’oa miti hiyo katika vyanzo vyote vya maji.

Gavana Chepkwony alichukua hatua hiyo kufuatia uwepo wa uhaba wa maji katika kaunti hiyo.

Makataa ya wakazi wa Kaunti ya Kisii kukata na kuondoa miti hiyo karibu na vyanzo ya maji yalikamilika Septemba 31, mwaka huu.

Makataa hayo yalitolewa na Gavana James Ongwae mnamo Julai 1, mwaka huu, ambapo aliwapa wakazi wa kaunti hiyo muda wa siku 90 kukata miti yao kwa hiari.

Sheria kuhusu Usimamizi wa Mazingira ya 1999 inampa gavana mamlaka kuongoza juhudi za uhifadhi wa mazingira katika kaunti yake.

Kwa nini mikalatusi inaondolewa karibu na vyanzo vya maji?

Mikalatusi hutumia kiasi kikubwa cha maji hivyo husababisha kukauka kwa mito na vyanzo vinginevyo vya maji.

Kwa zaidi ya miongo miwili kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ikiwa mikalatusi inachangia katika uhaba wa maji nchini.

Mnamo 2009, aliyekuwa waziri wa Mazingira John Michuki aliagiza kung’olewa kwa miti hiyo karibu na vyanzo vyote vya maji.

Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (Nema) iliwashauri wakazi wa Murang’a kung’oa miti hiyo na kuipanda umbali wa mita 100 kutoka katika vyanzo vya maji.

Rais Mwai Kibaki aliwashauri wakulima kupanda miti inayotumia maji kidogo kama njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira.

Lakini, Shirika la Huduma ya Misitu (KFS) lilijitokeza na kupinga kwamba hakukuwa na ushahidi wa kuonyesha kuwa miti hiyo inakausha vyanzo vya maji.

“Mengi yamesemwa kuhusu miti ya mikalatusi kwamba inasababisha uhaba wa maji lakini hakuna mtu ambaye amewasilisha ushahidi. Mjadala mkali uliopo kuhusiana na mti huo ni ithibati kwamba hakuna utafiti uliofanywa kubaini madhara yake,” shirika hilo lilinukuliwa na gazeti la Daily Nation mnamo 2009.

Kuna aina zaidi ya 700 ya mikalatusi na ililetwa katika mataifa ya Afrika Mashariki katika karne ya 19 kutoka nchini Ethiopia.

Aliyekuwa mwanaharakati wa mazingira na mshindi wa Tuzo ya Nobel Wangari Maathai, pia aliwahi kuhimiza kuondolewa kwa miti hiyo kutoka karibu na vyanzo vya maji akisema kuwa inachochea kuwepo kwa makali ya njaa.

“Mikalatusi imeua mimea mingine kwani inatumia maji yote. Kuna haja ya kupanda miti ya kiasili ilinayotumia kiasi kidogo cha maji,” akasema Prof Maathai.

Tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa mti mmoja wa mkalatusi unahitaji lita 785 za maji ili kutoa mti wa uzani wa kilo moja. Inakadiriwa kuwa hutumia lita 90 za maji kwa siku.

Lita mbili za maji kila siku

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), binadamu anahitaji angalau lita mbili za maji kwa siku.

Hiyo inamaanisha kuwa mti mmoja unatumia maji ambayo yangetumiwa na watu zaidi ya 40.

Upanzi wa miti hiyo pia umepigwa marufuku katika baadhi ya majimbo nchini India.

Mwongozo wa shirika la KFS unaonyesha kuwa miti ya mikalatusi inafaa kupandwa katika maeneo yaliyopoteza rotuba au kukumbwa na mmomonyoko wa ardhi.

“Mikalatusi pia inaweza kutumiwa kuondoa maji katika eneo fulani au katika ardhi iliyo na chumvi,” unasema mwongozo wa KFS.

Miti hiyo pia haifai kupandwa karibu na nyumba au barabara kwani matawi yake huvunjika kwa urahisi hivyo kusababisha uharibifu.

“Miti hiyo haifai kupandwa katika maeneo ambayo hukumbwa na uhaba wa mvua mara kwa mara kwani inatumia maji yote na kuacha mazao yakinyauka,” unasema mwongozo wa KFS.

Kulingana na mhadhiri wa Kitivo cha Mazao na Kilimo katika Chuo Kikuu cha Egerton, Carol Mutua, mikalatusi pia hutoa chembechembe za sumu ambazo huzuia mimea iliyo karibu kukua.

Mbali na kuwa na madhara kwa vyanzo vya maji, mikalatusi ina manufaa tele.

• Mikalatusi hutoa mbao na pia majani yake ni dawa.

• Majani ya mti huo hutumiwa nchini China, India, Ugiriki na hata mataifa ya Ulaya kutengeneza dawa ya mafua na kikohozi.

• Majani yake pia hutumika katika kutengeneza dawa ya kusafisha meno kwani hayapatani na bakteria.

• Kadhalika, mikalatusi huchangia kwa kiasi kikubwa katika kufyonza gesi chafu ya kaboni ambayo husababisha joto duniani.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: UTI husambazwa kupitia ngono?

AFYA JAMII: Kidume cha mbegu au goigoi chumbani?

adminleo