Akili MaliMakala

Mbinu za kisasa kuzalisha uyoga

Na SAMMY WAWERU May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKULIMA wa uyoga wangali wanatumia mbinu asilia kukuza zao hilo, ambalo ni chanzo mbadala cha virutubisho vya protini.

Uyoga ni jamii ya kuvu (fungi) inayokua ardhini, kwenye miti, au sehemu zenye unyevunyevu, na inajulikana kwa muundo wa kipekee ulio kama kofia juu ya kikonyo.

Kuboresha ukuzaji, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kimezindua mfumo mpya kusaidia kuongeza mazao na kutunza mazingira.

Chini ya teknolojia, Smart Mushroom Farming, wakulima sasa wanaweza kuzalisha kuvu kwa njia ya kiotomatiki – mtambo unaotumika kunyunyizia uyoga maji, kupulizia dawa na hata kudhibiti kiwango cha joto, unyevuunyevu na vigezo vingine muhimu.

Dkt Lawrence Nderu mwasisi wa JHUB Africa, JKUAT akionyesha jinsi mtambo mpya wa kukuza uyoga hufanya kazi. Picha|Sammy Waweru

Chini ya mradi – Smart Mushroom Farming Initiative, mradi huo, kituo cha utafiti cha JKUAT, ndicho JHUB Africa, mwasisi wake Dkt Lawrence Nderu anasema mfumo huo utasaidia kuboresha ukuzaji.

“Ni ukuzaji kwa njia ya kiotomatiki kuboresha kilimo cha uyoga,” akasema Dkt Nderu, wakati wa uzinduzi wa mradi huo JKUAT, Juja, Kaunti ya Kiambu majuzi.

Mpango huo, aidha, unalenga kufanikisha kilimo endelevu na kulinda misitu kwa sababu mfumo unaotumika unahitaji kiwango kidogo tu cha ardhi. Wakulima wengi wa uyoga wanalazimika kukata miti ili kuukuza.

Maafisa wa JKUAT na Mushroom & wakikagua uyoga unaoendelea kukua chini ya mfumo wa Smart Mushroom Farming. Picha|Sammy Waweru

Kwenye mahojiano ya kipekeee na Akilimali, Dkt Nderu ambaye pia ni mwenyekiti wa Kitengo cha Uchakataji wa Taarifa kwa Kutumia Kompyuta, JKUAT, alisema teknolojia hiyo inayotumika Korea Kusini inawezesha wakulima maeneo ya miji kukuza uyoga kwenye mabustani yao, hivyo basi kuzuia ukataji na uharibifu wa miti.

“Uzinduzi wa kilimo cha uyoga kwa njia ya kisasa ni mojawapo ya mbinu kuangazia ajenda ya usalama wa chakula, kuboresha mazingira na kulinda misitu Kenya,” Dkt Nderu akaelezea.

Uyoga, bidhaa mbadala ya nyama, huliwa kwenye hoteli na mikahawa mingi ya kifahari Nairobi, Nakuru, Mombasa, Kisumu, na Eldoret, na inaendelea kuwa maarufu kwenye menu.

Watu wanazidi kuwa makini na wanachokula, kwa sababu ya maradhi yanayohusishwa na afya. Kupitia mfumo wa Smart Mushroom Farming, wakulima hawahitaji kukata miti.

Dkt Lawrence Nderu mwasisi wa JHUB Africa na mfanyakazi JKUAT kwenye chumba cha kuzalisha uyoga JKUAT. Picha|Sammy Waweru

Shukran kwa JHUB Africa na ushirikiano wake na Mush &, kampuni kutoka Korea Kusini, na Korea International Cooperation Agency (KOICA), chini ya mpango wa teknolojia hiyo bunifu kukuza na kuboresha kilimo cha uyoga.

“Ni mfumo unaodhibiti kiwango cha joto, unyevuunyevu, hewa, Kaboni, na mwangaza hivyo kupunguza gharama ya uzalishaji,” akasema Jihyun Jung, Afisa Mkuu Mtendaji Mush &.

Mfumo huo, unashirikisha teknolojia ya kuunganisha mtambo kudhibiti huduma kwa simu ya mkono, ndiyo rununu, hivyo mkulima anaweza kujua jinsi ‘shamba’ lake la uyoga linavyoendelea hata akiwa mbali nalo.

Jihyun Jung, Afisa Mkuu Mtendaji Mush & akielezea kuhusu mfano wa kisasa kuzalisha uyoga. Picha|Sammy Waweru

“Huduma zote zinaendeshwa kutoka eneo moja,” Jihyun akaongeza, akisisitiza kwamba ni mfumo endelevu kuboresha kilimo cha uyoga na kulinda na kudumisha mazingira.

JHUB Africa, tayari imeanza kuhamasisha wakulima, Dkt Nderu akidokeza kuwa wakulima wapatao 400 kutoka Kiambu na Machakos wamepata mafunzo.

Mradi huo ni wa bajeti ya Sh29.82 milioni. Kaunti ya Kiambu pekee, alifichua kwamba wanalenga kufikia wakulima 60, 000.

Mradi huo wa miezi 15, unalenga kusambaza mbegu za uyoga (spawn) maeneo mbalimbali nchini, kutoa mafunzo kuhimiza ukumbatiaji wa zao hilo kwa njia ya kidijitali, ili kuongeza kiwango cha mazao na kulinda mazingira.

Mbegu za uyoga – maarufu kama spawns kwenye mifuko. Picha|Sammy Waweru