Akili MaliMakala

Mboga za kienyeji ng’ambo zampa hela

Na SAMMY WAWERU September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUKAA kwake nchini Ujerumani mwaka mmoja, kulimtosha Mkenya, James Shikwati, kugundua soko kubwa la mboga za kienyeji ambalo halikuwa limezamiwa.

Akiwa ughaibuni, Shikwati – mchanganuzi wa sera aliyegeuka kuwa mfanyabiashara, alishuhudia mahangaiko ya Waafrika kutafuta vyakula vya kiasili hasa mboga za kienyeji kama vile saga, murenda na terere.

Hata hivyo, upatikanaji wa mboga hizo haukuwa rahisi na zilizopatikana zikiwa ghali na zingine mlaji anakosa uhakika wake.

“Sawa na wengine, nilikosa sana ladha ya mboga za kienyeji kule ng’ambo,” anakumbuka.

Mboga za kienyeji zilizokaushwa na IREN Growthpad Ltd. Picha|Sammy Waweru

Ni kutokana na kuishi kwake Ujerumani, pamoja na uzoefu wa kumbukumbu za wakulima na kina mama alizokusanya jinsi ya kupika vitoweo vya mboga, alishawishika kuanzisha kampuni ya kuongeza thamani mboga asilia.

Shikwati, ambaye pia ni mwandishi, ndiye mwanzilishi na mkurugenzi wa IREN Growthpad Ltd, kampuni yenye kiwanda Kakamega inayosindika mboga za kienyeji kwa ajili ya soko la humu nchini na ng’ambo.

Kwa mwezi, anakadiria hukausha wastani wa kilo 300 za mboga na msimu ambao zinakuwa nyingi shambani anawahi kilo 750.

“Kiwanda kina uwezo wa kukausha kilo 500 za mboga kwa siku, lakini tunazalisha karibu kilo 300 kulingana na oda za soko na mifumo ya kuhifadhi tuliyonayo,” anaelezea Shikwati.

Mboga za kienyeji zilizokaushwa zikiwa kwenye shelfu ya afisi za IREN Growthpad Ltd, Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Lengo lake, anasisitiza ni kupanua uzalishaji hadi kufikia tani tatu kwa siku – sawa na kilo 3,000. Kukithi mahitaji ya soko, Shikwati anategemea kusambaziwa mboga na wakulima 1,300 aliotia saini kandarasi nao.

Aidha, wanazaraa hao hulima aina sita za mboga: murenda, managu, mito, kunde, terere na saga, ambazo huongeza thamani. Kwa mujibu wa takwimu zake, kila mkulima humsambazia kati ya kilo 40 na 60 na hulipwa wastani wa Sh50 kwa kilo.

IREN Growthpad hukausha mboga kwa kutumia nguvu za kawi yaani sola, zinapakiwa na kusafirishwa Jijini Nairobi kwa minajili ya usambazaji ambapo kampuni hiyo ina afisi na duka.

Masoko ya ughaibuni anayolenga ni pamoja na Amerika (US) na nchi za Mashariki ya Kati Uarabuni (Middle East).

James Shikwati akionyesha mboga za kienyeji anazouza ng’ambo. Picha|Sammy Waweru

Shikwati aliingilia rasmi biashara ya kusindika mboga mwaka 2021, na mwaka uliofuata mianya ikafunguka kusambaza bidhaa Amerika. Kuanzisha kiwanda cha kukausha mboga, anafichua kwamba ilimgharimu kima cha Sh3 milioni.

Mtaji huo, anadokeza ulitokana na fedha alizokuwa ameweka kama akiba na pia kuchukua mkopo. Kwenye mahojiano na Akilimali, mjasiriamali huyo alisema awali shabaha yake ilikuwa kuboresha ulaji wa ndani kwa ndani wa mboga za kienyeji.

“Licha ya kuwa soko la humu nchini mboga za kienyeji zina ushindani mkuu, wenzetu ughaibuni pia wanazithamini,” akasema.

Kulingana na ripoti ya Wizara ya Kilimo, ulaji wa ndani kwa ndani wa mboga asilia unasimamia asilimia 95 – hii ikiashiria kuwa ni asilimia 5 pekee inauzwa nje.

Mboga aina ya sucha, maarufu kama managu, iliyokaushwa na IREN Growthpad Ltd. Picha|Sammy Waweru

Ripoti ya Wizara, pia inaonyesha kwamba ukuzaji wa mboga nhcini uliongezeka kwa kasi kati ya 2011 na 2019, data zikionyesha Kenya kwa sasa inazalisha wastani wa tani 300,000 kwa mwaka.

Kuuza bidhaa za chakula nje ya nchi, mfanyabiashara sharti azingatie na kuafikia viwango vya ndani na vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na cheti cha FDA – Food and Drug Administration (FDA) cha sheria za Amerika na nchi muungano wa Bara Uropa (EU) kusafirisha mazao mabichi ya kilimo.

Hapa nchini, HCD na KEBS, ndizo taasisi zinazoshughulikia uthibitishaji.

Esperance Chesoli, msimamizi wa wafanyakazi IREN Growthpad Ltd akielezea jinsi mboga za kienyeji hukaushwa. Picha|Sammy Waweru

Hata ingawa anaridhia ufanisi kwenye mtandao wa biashara aliyozamia, Shikwati anakiri kuwepo kwa changamoto si haba — gharama za juu za usafirishaji mboga nje, sheria za ushuru zinazobadilika mara kwa mara na baadhi ya wakulima kumsambazia mboga ambazo hazijaafikia ubora.

Hata hivyo, anaamini sekta ya mboga ikiwa na mfumo rasmi sawa na wa kahawa na chai, inaweza kubadilisha maisha ya wakulima haswa wenye mashamba madogo.

Terere, mitoo na kunde zilizokaushwa na kampuni ya IREN GrowthPad. Picha|Sammy Waweru