• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Mboga za kienyeji ni riziki kwake

Mboga za kienyeji ni riziki kwake

NA PETER CHANGTOEK

MBOGA za kiasili hupendwa mno katika maeneo mbalimbali na wakuzaji wowote, hususan wale wanaozikuza mboga zizo hizo karibu na miji mikuu nchini, hawatakosa kukuambia kuwa mboga hizo zina tija tele.

Patrick Onzere ni mkuzaji wa mimea hiyo yenye tija, na aliling’amua jambo hilo na kukata kauli kujitosa katika ukuzaji wa mboga za kiasili, pamoja na nyinginezo ili kujipa riziki ya kila siku.

Mkulima yuyo huyo, ambaye alisomea uanahabari- unasaji wa video, anadokeza kuwa alijitosa kwa ukulima akiwa mdogo, japo alijitosa kikamilifu kwa shughuli iyo hiyo takribani miaka minne iliyopita.

“Nilijitosa kwa ukulima nikiwa mdogo, japo sikuwa nikifanya ukulima kama kazi hadi mwaka 2016, nilipoacha kushughulika kuzitafuta kazi za afisini, na kufanya ukulima kuwa kazi,’’ asema mkulima huyo.

Onzere huikuza mimea ainati za kiasili, mathalan; michicha (Amaranthus), minavu (black nightshades) , miboga (pumpkins), kunde, n.k., katika eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu

Aidha, mkulima huyo huikuza mimea mingineyo kama vile kabeji/kabichi nyekundu na kabichi nyeupe, pilipili hoho, brokoli, kaliflawa (cauliflower), sukumawiki, spinachi, vitunguu na dania.

Mbali na mimea hiyo, mkulima huyo huikuza mimea yenye harufu nzuri kama vile minanaa (mints), miongoni mwa mimea mingineyo mingi aikuzayo.

Anafichua kuwa hakuutumia mtaji mwingi kukianzisha kilimo hicho. “Sikuzitumia pesa nyingi kuanzisha. Nilizinunua mbegu za sukumawiki na spinachi na kuanzisha. Faida nilizopata ndizo nilizozitumia kuzinunua mbegu nyinginezo,’’ adokeza mkulima huyo.

Onzere anasema kuwa alilelewa katika familia iliyokuwa ikifanya shughuli za zaraa, na anamshukuru mamaye kwa kumpa uelekezi aula kuhusu masuala ya kilimo.

Mwanzoni, mkulima yuyo huyo alianza kwa kuyatumia magunia kuikuza mimea yake, lakini baadaye, mambo yakamwia vyema.

Anaongeza kuwa alisukumwa na moyo wa kutaka kuwaona watu wakila vyakula bora, hususan wakazi wa maeneo ya Nairobi.

Yeye hujitengenezea mbolea ambayo huitumia kuikuza mimea katika shamba lake. “Mimi huzitumia mbolea ya kiasili ninayojitengenezea kutoka kwa wanyama kama vile ng’ombe, kuku, sungura na mbuzi,’’ afichua Onzere.

Kwa mujibu wa mkulima huyo ni kuwa, wateja wake hupatikana katika mitaa ya Nairobi, japo anafichua kuwa milango imefunguka na kuanza kuwapata wateja wengine katika kaunti nyinginezo nchini.

Anadokeza kuwa, ni muhali mno kwa mimea yake kuathiriwa na magonjwa au kuvamiwa na wadudu waharibifu, kwa sababu yeye hudumisha usafi katika shamba lake.

Mkulima huyo anaongeza kwamba amekuwa akitegemea mvua kwa ajili ya kuikuza mimea yake. Hata hivyo, anadokeza kuwa wakati ambapo mvua haipo, yeye hushurutika kuyanunua maji ya kuyatumia katika shughuli hiyo.

Ni nadra sana kulipata jambo ambalo halina changamoto, na mkulima yuyo huyo anakiri kuwa amewahi kuzipitia changamoto za hapa na pale katika harakati zake za ukuzaji wa mimea.

Mojawapo ya ndaro ambazo amezipitia ni kulipata shamba lenye maji, la kulitumia kwa ukuzaji wa mimea karibu na jiji la Nairobi, ambapo wateja wake wengi huishi.

Pia, mbinu za kuyasafirisha mazao hadi kwenye masoko ni changamoto nyingine. Hata hivyo, anasema anatazamia kulisuluhisha tatizo hilo hivi karibuni, kupitia kwa njia ambayo hakuibainisha bayana.

Changamoto nyingine ambayo mkulima huyo huipitia ni ukosefu wa fedha za kumwezesha kuipanua biashara yake, ili kuyakimu matakwa ya wateja wake walioko jijini Nairobi pamoja na maeneo mengineyo nchini.

Mbali na kuikuza mimea yake kwa njia ya kiasili, amekuwa akiwafunza wakulima wengine wenye mashamba kuhusu zaraa hiyo, kusudi wao pia wajishughulishe nayo.

Anawashauri wale wanaotaka kujitosa katika ukulima kama huo kufanya utafiti, na wawe na uvumilivu.

Anafichua kuwa ana mipango ya kuikuza mimea hiyo kwa wingi katika siku za usoni. Isitoshe, anaazimia kulifungua duka la kuziuzia mboga pamoja na mazao mengine ya shambani, ili kumwezesha kuwa na uwezo wa kuyanunua na kuyauza mazao yaliyozalishwa kwa mbinu za kiasili.

You can share this post!

Corona yaongezea msumari moto kwa kidonda cha wakuzaji wa...

Ielewe teknolojia ya kisasa ya kuotesha mbegu