Makala

Mboga za tangu na tangu zina umuhimu mkubwa kiafya

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

CHAKULA asilia ni mazao yaliyokuzwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimohai.

Aidha, huu ni mfumo ambapo mazao yanazalishwa bila kutumia kemikali na kukumbatia mbolea itokanayo hasa na mifugo.

Pia, unajumuisha ulaji wa chakula cha kale kama vile viazivikuu na mboga za kienyeji.

Katika hilo, mboga asilia kama vile mnavu, kunde, mchicha, saget na kansella ni miongoni mwa ambazo watu wanashauriwa kula kwa wingi.

Mboga hizi zinakuzwa kwa wingi maeneo ya Bonde la Ufa, Kisii, Magharibi na Kati mwa Kenya.

Pia zinazalishwa kwa wingi nchini Nigeria, Uganda, Ghana, Afrika Kusini na Tanzania. Bara Uropa pia limekumbatia ukuzaji wa baadhi ya mboga hizi.

Hata hivyo, si wengi wanafahamu faida kiafya za mboga za kienyeji.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema kiwango cha mafuta, Cholesterol, kwenye mboga asilia ni cha chini mno.

“Cholesterol katika mboga za kienyeji ni kidogo sana. Mafuta mengi mwilini huziba mishipa ya damu na hatima ni kuugua ugonjwa wa shinikizo la damu na moyo. Wenye mazoea kula mboga hizi, matatizo ya aina hiyo kwao ni historia,” afafanua Juliet Mwanga, mtaalamu.

Anaendelea kueleza kwamba zimesheheni Vitamini A, C, madini ya Potassium na Fiber.

“Fiber ni madini muhimu katika usagaji wa chakula mwilini. Pia husaidia kudhibiti ugonjwa wa Kisukari na wa moyo,” aeleza mdau huyu.

Suala tata la Saratani pia litaweza kuangaziwa iwapo kila mwananchi atakubali kula mboga na chakula asilia.

Ingawa hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba kuna sababu mbalimbali za saratani.

Zinaliwa kwa kuandamanisha na ugali, matoke, nyama, wali au mlo wowote ule unaoandaliwa.

Kando na manufaa yake anuwai kisiha, wanaokuza mboga hizi wana kila sababu kutabasamu kutokana na mapato yake. Ni wachache mno wanaozizalisha.

Milcah Wahome ni mmoja wa wakulima hao nchini na hukuza mnavu maarufu kama managu au sucha, mchicha (terere) na kansella, katika kaunti ya Nairobi. Pia, hukuza spinachi na sukuma wiki.

“Mboga hizi ni mithili ya mahamri moto Nairobi. Hazikosi soko kwa sababu ya manufaa yake kiafya,” asema Bi Wahome.

Isitoshe, si lazima mkulima awe na kipande kikubwa cha shamba.

Kulingana naye, hata robo ekari ina uwezo wa kuzalisha mazao tele. Anaeleza kwamba taratibu zake za upanzi ni rahisi, ikiwa ni pamoja gharama nafuu.

“Mboga za kienyeji ni vigumu kuathiriwa na magonjwa,” asema mkulima huyu.

Wadudu wanaoshuhudiwa ni kama vile viwavi, vidukari na vithiripi.

Hata hivyo, mkulima akizingatia mbinu asilia na taratibu bora kitaalamu, changamoto hizo zitadhibitiwa.

Huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi. Aidha, kilo moja ya mboga hizi haipungui Sh30.