Mbotela aenziwa, wito wa ujenzi wa eneo la kuwazika mashujaa ukitanda
WITO wa kujengwa kwa eneo tengwa la kuwazika mashujaa jana ulitawala ziara ya wanasoka wa zamani na maafisa wa serikali katika makazi ya mtangazaji nguli marehemu Leonard Mambo Mbotela.
Mwanabari huyo wa miaka mingi alirejelewa na majagina hao kama mtu ambaye aliweka msingi wa ukuuaji wa soka wakati ambapo bado teknolojia ambayo ipo sasa, haikuwepo.
Kutakuwa na ibada ya wafu mnamo Ijumaa ya kumuenzi Mbotela katika Kanisa la All Saints Cathedral kabla ya mazishi yake Jumamosi katika makaburi ya Langáta.

Naibu Mkuu wa Wafanyakazi kwenye Afisi ya Rais Eliud Owalo na mbunge wa Muhoroni Onyango Koyoo waliwaongoza wanasoka hao kumwomboleza Mbotela wakisema jinsi alivyokuwa akiutangaza mpira iliwasisimua na kuwachangamsha wengi.
“Mbotela alikuwa shujaa katika fani ya soka na jinsi alivyokuwa akitangaza mpira miaka ya 80 kulifanya wengi wetu kupenda mpira na wakaishia kuwa mashabiki,” akasema Owalo katika boma la marehemu mtaa wa Nairobi Dam barabara ya Langáta.
Waziri huyo wa zamani wa ICT alizua kumbukumbu jinsi ambavyo Mbotela alitangaza mechi ya fainali ya Cecafa kati ya Kenya na Uganda uwanjani Nakivugo ambayo ilikuwa na ushindani mkali.

“Hapa tuna wachezaji ambao walishiriki mchuano huo ambao ugumu wake ulikuwa dhahiri kutokana na jinsi ambavyo Mbotela alivyoutangaza. Mambo alikuwa mtangazaji ambaye alichapa kazi na kuwasisimua wengi na alikuwa akithaminiwa sana na wachezaji,” akaongeza Owalo.
Waziri huyo alisema wachezaji wengi walikuja wakafahamika sana Afrika Mashariki na nje ya ukanda huu, kutokana na utangazaji wa mpira wa Mbotela.
Koyoo ambaye anahudumu muhula wake wa tatu, alisema kuwa atawasilisha mswada bungeni wa kuitaka serikali kujenga eneo la kuwazika mashujaa. Kuzikwa kwa Mbotela kwenye makaburi ya Langáta ni jambo ambalo halijapendeza baadhi ya Wakenya kutokana na mchango wake mkubwa kwenye tasnia ya uanahabari.
“Talanta na upekee wa utangazaji wake ulikuwa wa kiwango chake. Nitakuwa nawasilisha mswada wa kuhakikisha kuwa mashujaa na majagina wanazikwa eneo lao tengwa,” akasema Koyoo.
Jimmy, mwana mkubwa wa kiume wa Mbotela alisema babake aliupenda mpira na mara nyingi alikuwa akienda naye uwanjani kutangaza mchezo huo. Jimmy aliunga wazo la kuanzishwa kwa eneo la kuwazika Mashujaa akirai bunge kuweka sheria hiyo upesi.

“Sisi sote tunampenda Mbotela kutokana na jukumu alilotekeleza wakati ambapo alikuwa hai. Pia sote ikiwemo sisi wanafamilia tunaunga mkono kutengwa kwa eneo la kuwazika mashujaa, ni jambo ambalo hata sisi tumezungumzia na pia limesemwa bungeni,” akasema Jimmy.
Josephat Murilla ‘Controller’, John ‘Bobby’ Ogolla, Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee waliwaongoza majagina kutuma rambirambi zao na kuzua kumbukumbu jinsi walivyotangamana na Mbotela na pia wakamuenzi.
“Sote tuna kumbukumbu nzuri kutokana na jinsi ambavyo Mbotela alivyotutangaza. Alikuwa baba wetu, alitangamana nasi na juhudi zake zilifanya tukajulikana na hadhi yetu kupanda kwenye jamii,” akasema Ogolla.
Majagina wengine ambao walikwepo ni Mickey Weche “T9”, Sammy Owino “Kempes”, George Sunguti, Peter Otieno “Bassanga”, Micke Amwayi, David Ochieng “Kamoga”, Peter LichungU, Tobias Ocholla “Jua Kali”, Dennis Obua, Omar Shaban, Nick Okoth, John “Shotto” Lukoye na Micke Otieno.