MBURU: Kinoti ahakikishe kikosi kipya chatumikia wananchi
Na PETER MBURU
IDARA ya polisi ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikihusishwa na ufisadi kwa kiwango kikubwa zaidi nchini.
Polisi wamehusishwa na hata kushtakiwa kwa makosa ya ulaji hongo ili kufumbia macho uvunjaji sheria, kushiriki katika makosa ya jinai kama wizi na mauaji, kati ya maovu mengine ya kijamii.
Hii ni licha ya ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa kuwa, hali itaboreshwa, na hata wakuu wa idara hiyo kujaribu kufanya mageuzi aina aina, yamkini kuridhisha raia.
Kwa mfano, siku za hivi majuzi, visa vya maafisa wakuu wa polisi kuhamishwa kutoka vituo vyao vya kazi hadi vingine vimekuwa vikishuhudiwa, hasa kunapoibuka tetesi kuwa usalama unadorora maeneo walipo.
Wiki hii, Mkurugenzi wa Kitengo cha Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti alivunja kikosi Flying Squad ambacho kimekuwa kikikabiliana na wizi wa mabavu, ujambazi, na maovu mengine, badala yake akaunda kikosi cha Sting Squad Headquarters (SSH).
Aidha, alipunguza makali ya kitengo cha Uzuiaji wa Uhalifu (SPCU) akibakisha maafisa watakaohudumu katika Makao Makuu pekee, na kukipa jina la Kitengo cha Utumishi wa Kipekee (SSU).
Japo idara ya DCI inajaribu kuwahakikishia Wakenya kuwa kila kitu kitakuwa shwari kuhusu masuala ya usalama sasa, ni vyema Bw Kinoti kufahamu kuwa utendakazi wa polisi hautegemei majina wanayotumia, ila kibarua kikubwa kimo katika kuwafunza maafisa wake kuhusu umuhimu wa kutumikia taifa.
Kile maafisa wa polisi nchini, na wa umma kwa ujumla wamekosa, ni moyo wa kutumikia taifa, bila kujali rangi, kabila, ama hadhi ya mtu katika jamii.
Asilimia kubwa ya maafisa hawa wanashikilia dhana potovu kuwa endapo mtu fulani ni tajiri, mwanasiasa ama mtu wa eneo fulani, yeye ana haki kushinda wengine.
Ni vigumu kumpata afisa aliye tayari kufuata sheria hadi tamati, kuhakikisha kuwa haki inapatikana.
Wakati bado maelfu ya polisi wana imani za aina hii, itakuwa vigumu kufanya mageuzi ya kweli na ya kujivunia kama taifa. Kubadili majina ya vikosi, kuhamisha maafisa wanaokosea kazini ama hata kubadili sare si tiba.
Dawa ya kweli kwa ugonjwa huu unaoathiri idara ya polisi ni mageuzi ya nafsi na imani kwa kila mhusika na kuifanya idara ya kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa na bila kuazimia kujinufaisha.