Makala

MBURU: Naam, mavazi ya kitaifa yataboresha ubunifu, utaifa

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

AGIZO la serikali kwa watumishi wa umma kuwa wawe wakivalia mavazi yaliyoshonewa nchini kila Ijumaa na sikukuu za kitaifa ni lizuri, na ambalo linaweza kuzidisha utaifa, kuboresha ubunifu na kuinua uchumi wa nchi.

Kwa kuanza kukumbatia vitu vinavyotengenezewa Kenya, hii itakua mbinu mojawapo ya kuinua viwanda vyetu, na hivyo kuongeza nafasi za ajira kwa Wakenya.

Vilevile, itakuwa njia nzuri ya kupunguza pesa ambazo Wakenya hutumia kununua nguo kutoka mataifa ya nje, hali ambayo huhamishia utajiri wetu kwa mataifa hayo.

Washonaji wenye ubunifu, vilevile, watapata fursa ya kuuboresha, huku wakitengeneza bidhaa ambazo zinaisaidia nchi.

Ni vyema kuwa na viwanda vinavyofanya kazi saa 24, na ambavyo tunaweza kujivunia kuwa vitatutengenezea bidhaa, kama mataifa mengine yaliyojikuza kiuchumi.

Faida nyingine ya hatua hiyo itakuwa ni kuwainua wakulima ambao ndio wanakuza pamba na mimea mingine ya kutengeneza mavazi, ili wapate mapato zaidi.

Manufaa haya ni licha ya utaifa ambao tutakuwa tunazidi kuukuza, kwa kufahamu kuwa tuna uwezo wa kutengeneza bidhaa sisi wenyewe badala ya kutegemea mataifa mengine, jambo litakalotufanya kupeperusha bendera yetu juu zaidi.

Hata hivyo, jambo moja ambalo serikali inafaa kuzingatia wakati ikihimiza utekelezaji wa agizo hilo ni kuwa, sharti wakulima na watengenezaji wa bidhaa hizi watiwe motisha na wafanywe pia kula matunda ya jasho lao.

Kwanza, wakulima wanafaa kurahisishiwa utaratibu wa kilimo, kwa serikali kuondoa vikwazo vya kununua bidhaa zinazohitajika ili kukifanikisha, kama mbolea ili pia gharama ya uzalishaji wa hiyo mimea iwe ya chini.

Itakuwa vigumu sana kwa hatua hii kufanikiwa, endapo watu wenye umuhimu sana – ambao ni vijana wenye mapenzi ya ushonaji wa kiubunifu, wakulima na wafanyakazi katika viwanda husika – wataachwa nyuma.

Umuhimu wa kuhusisha kila mtu katika safari hii – badala ya maafisa wakuu serikalini pekee jinsi imekuwa kihisoria – ni kuwa Wakenya kwa jumla watajitolea pia kununua mavazi hayo, ili kwa pamoja tukuze nchi yetu.

Mtihani mkubwa kwa serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa katika safari hii inatembea na kila Mkenya, awe mkulima, mfanyakazi kiwandani, vijana wabunifu katika sekta ya ushonaji na hata watumishi wa umma.