Makala

MBURU: Ni wazi sasa, ajira kwa vijana ni ndoto ya mchana

October 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MASHIRIKA mbalimbali ya kiserikali yanaonekana kuwa na ari spesheli ya kuwaajiri wazee wakongwe wakati taifa linazongwa na utovu mkubwa wa ajira, haswa kwa vijana.

Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuendelea kujisifu jinsi wanavyowainua vijana, na kuendelea kuhubiri jinsi wanafaa kujiajiri, badala ya kusubiri kuajiriwa.

Katika matukio fulani, serikali imekuwa ikiwarejesha kazini maafisa ambao wamekamilisha muda wa kuhudumu kisheria, baada ya kustaafu. Tulipofika, imekuwa ni mtindo kwa watu waliostaafu kuteuliwa kwa awamu ya pili, licha ya uzee mkubwa.

Hata baada ya mipango ya jinsi ya kuongeza nafasi za ajira kwa vijana kujadiliwa mara nyingi, bado wengi wao wanazidi kuteseka mitaani kwa kukosa la kufanya. Wamesubiri kwa hamu na ghamu angalau kupata vibarua vya kujikimu ila wameambulia patupu.

Uteuzi wa aliyekuwa mbunge wa Othaya Mary Wambui kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ajira (NEA) ndio wa majuzi zaidi, na ambao umevutia hisia kali tena miongoni mwa Wakenya, ambao wanaikashifu serikali kwa tabia hii ambayo imeifanya kuwa mtindo.

Wengi, nikiwa mmoja wao, wanashangaa ni kipi Bi Wambui amelifanyia taifa letu hadi kupewa kazi hiyo.

Licha ya kukataliwa na wananchi uchaguzini mnamo 2017, serikali katika mtindo wake mpya bado imefanya juhudi za kumpa kazi, wakati kwa kweli hakuna ujuzi spesheli anaokuja nao kuokoa hali ya Kenya.

Vijana wamejitokeza wazi, na katika mitandao ya kijamii na kukashifu uteuzi wa Bi Wambui, na hata mbunge wa Starehe Charles Njagua ametangaza mpango wa kuwasilisha mswada wa kisheria utakaopunguza umri wa kustaafu.

Miaka mitatu zaidi

Kuteuliwa kwa Bi Wambui kumekuja siku chache baada ya muda wa mwenyekiti wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) Francis Muthaura, 72, kuendelea kuongoza Bodi ya mamlaka hiyo kuongezwa kwa miaka mitatu zaidi.

Miezi kadhaa iliyopita, aliyekuwa makamu wa Rais Moody Awori (aliye na zaidi ya miaka 90) aliteuliwa na Rais kuwa mwanachama katika Hazina ya Michezo na Sanaa. Rais Kenyatta alitetea uteuzi wake, akisema kuwa vijana wamekuwa na hulka ya kuibia serikali.

Wakenya bado hawajasahau teuzi za Esther Murugi, 69, kuwa mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Ardhi (NLC) Beth Mugo, 80, kama seneta maalum wa Jubilee, miongoni mwa wazee wengine ambao wanazidi kuteuliwa.

Japo serikali imekuwa ikiimba kuhusu mipango ya kuongeza ajira kwa vijana, lakini inaonekana kama itasalia tu kuwa ndoto kwa vijana.