• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
MC: Mfahamu chifu ‘simpo’ anayezipa sherehe ‘tempo’ ya nguvu kwa madoido

MC: Mfahamu chifu ‘simpo’ anayezipa sherehe ‘tempo’ ya nguvu kwa madoido

NA KALUME KAZUNGU

NI mtindo wa machifu na maafisa wengine wengi wa utawala nchini kuonekana wakiwa wamevalia sare, kikiwemo kirauni kichwani huku wakikamata bakora au ‘kifimbo’ mkononi.

Utawapata maafisa hao wakitoa amri hapa na pale ama kwa upande mwingine wakihimiza raia kutii sheria za nchi, iwe kwa kurai raia wapenda amani au kwa kulazimisha watundu.

Yaani kwa kawaida, maafisa hawa mwonekano wao huwa ni ule wa urasmi katika kazi na mtagusano na watu.

Lakini kwa chifu Khalifa Shariff Alwy, mambo kwake ni tofauti kabisa.

Bw Alwy,53, ambaye ni Chifu Mkuu wa lokesheni ya Mokowe iliyoko Lamu Magharibi, anatambuliwa na wananchi kama ‘Chifu Simpo’.

Jina hilo la mbandiko linatokana na hulka yake ya kupenda sana kutangamana na raia wa tabaka zote.

Kinyume na kawaida ya machifu wengine, Bw Alwy yeye mara nyingi hutamuona akiwa ameshikilia kifimbo mkononi wala kuvalia sare.

Mara nyingi utapishana au kutagusana na Chifu Alwy akiwa kavalia vivi hivi tu kama raia.

Kwa wageni wasiomfahamu Bw Alwy, huenda wakamfikiria tu kuwa mwananchi wa kawaida asiye haiba yoyote katika jamii yake.

Aidha wengine wasiomfahamu huishia kugutushwa wanaposikia wenyeji wa eneo lake wakisema “Hello Bwana Chifu…Hujambo?”

Isitoshe, ‘Chifu Simpo’ pia anafahamika ndani na nje ya kaunti ya Lamu kwa jinsi alivyo mweledi katika masuala ya ufawidhi-yaani MC.

Utampata Bw Alwy akizipamba vilivyo na kuzipa sherehe za kiserikali na zile za kijamii ‘tempo’ ya aina yake.

Umahiri wake katika kuipamba lugha, hasa ile ya Kiswahili na sauti yake nyororo umechangia pakubwa kwa chifu huyu kila mara kuteuliwa kuongoza sherehe, hasa zile za kiserikali kama vile Jamhuri Dei, Mashujaa Dei, Leba Dei, Madaraka Dei, na Siku ya Utamaduni–inayoadhimishwa kila Oktoba 10–ambayo kwa sasa itafahamika kama Mazingira Dei.

Lakini je, kwa nini chifu huyu, licha ya kuwa na hadhi hiyo serikalini, kaamua kuishi maisha ya kujishusha namna hiyo?

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne, Bw Alwy alisema hatua yake ya kujiweka katika hali ya kawaida kama raia imemsaidia pakubwa kutagusana vyema na wanajamii au wananchi wake anaowatawala kwa kuwa kazi yake imeainishwa chini ya ofisi ya Rais wa nchi.

Bw Alwy anasema ni kupitia hulka yake hiyo ya ‘u-simple’ ambayo imemwezesha kuwa mtu wa watu, hivyo kurahisisha vilivyo kazi yake ya kila siku ya utawala.

“Tangu udogoni mwangu mimi sijakuwa mtu wa majigambo. Huingiliana au kutangamana na kila mtu, iwe ni wa tabaka la juu au chini. Ninaamini sana kwamba ili kazi yangu itekelezeke ipasavyo, basi cha msingi ni kumpenda na kumheshimu kila mmoja, kuanzia mkubwa hadi yule mdogo kabisa,” akasema Bw Alwy.

Anasema ni kupitia kujishusha kwake ambapo kumemwezesha kupata taarifa hata zile nyeti kabisa za kusaidia kudhibiti usalama wa Lamu.

“Kukiwa na ngoma, utanpata pale nikidensi. Ikiwa ni masuala ya kutangaza, hapa ndo kwao. Kazi ya uchifu imenisukuma kufanya hivyo ili iwe rahisi pia kwangu binafsi kupitisha zile jumbe za serikali kwa umma na kwa njia rahisi,” akasema Bw Alwy.

Aidha anataja kuwa sababu kuu inayomfanya kuzidi kupasha makali kipawa chake cha ufawidhi ni kutokana na kwamba sherehe nyingi, hasa zile za kiserikali huandaliwa eneo lake la Mokowe.

Ikumbukwe kuwa miaka ya hivi karibuni mji wa Mokowe umepandishwa hadhi kuwa makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu.

Isitoshe, Mokowe ndipo kwenye ofisi za uwakilishi wa serikali ya kitaifa, ikiwemo ile ya Kamishna wa Kaunti hiyo.

“Lokesheni yangu ya Mokowe imebeba hadhi kubwa.  Ndiyo makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu. Ofisi zote kubwakubwa za serikali ya kitaifa pia ziko kwenye lokesheni yangu. Mokowe pia ndio mji mwenyeji wa Bandari ya Lamu. Hii inamaanisha sherehe au hafla nyingi hufanyika hapa. Na ndio sababu ukwasi wa ufahamu nilionao kuihusu Mokowe ukanifanya kila mara kupewa nafasi ya ufawidhi au kuziongoza sherehe hapa,” akasema Bw Alwy.

Ni chifu ambaye pia hupenda kupiga picha na wananchi wa tabaka mbalimbali kila kunapokuwa na mikutano au makongamano Lamu.

Aidha anawasifu wananchi wake wa Mokowe kwa kuwa watiifu wa sheria za nchi, hali anayoitaja kurahisisha kazi yake hata zaidi.

“Sioni haja ya kuvalia kirauni au kushika kifimbo ndipo wananchi wafuate sheria. Watu wangu ni raia wema na watiifu wa sheria za nchi bila kusukumwa. Nafurahia kwamba mimi ni mtu wa watu,” akasema Bw Alwy.

Himizo lake kwa wananchi ni kwamba wote wadumishe utangamano, waishi kwa kuvumiliana, wapendane, wadumishe umoja ili kuboresha usalama Lamu, hivyo kulijenga taifa la Kenya kwa pamoja.

Bw Alwy amezaliwa eneo la Mokowe, Lamu Magharibi mwaka 1971.

Alisomea Shule ya Msingi ya Mokowe na kuhitimu mwaka 1988.

Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Lamu Bujra na kisha kuhamia mjini Mombasa alikojiunga na Shule ya Upili ya Tudor Day.

Alikamilisha masomo yake ya sekondari (KCSE) shuleni humo mnamo 1992.

Hakusonga mbele kimasomo kwani baadaye aliajiriwa kama mlinzi wa ndege za kampuni ya African Airline katika uwanja wa ndege wa Moi jijini Mombasa kati ya mwaka 1993 hadi 2006, ambapo kisha alirudi kwao Lamu.

Mwishoni mwa mwaka 2006, Bw Alwy aliajiriwa kuwa Naibu Chifu wa Mokowe hadi 2015 alipopandishwa cheo kuwa chifu.

Kwa sasa ndiye chifu mkuu wa lokesheni ya Mokowe.

Ameoa na ni baba wa watoto saba.

  • Tags

You can share this post!

Sarah afichua sababu ya kukatalia mbali penzi la Diamond...

Askari jela aliyemwaga unga akitibiwa aomba arudishwe kazini

T L