Mchakato wa kutambua, kusimamia na kugawa mali ya marehemu
SHERIA ya urithi hudhibiti jinsi mali na madeni ya mtu aliyefariki yanavyopitishwa kwa warithi au walengwa.
Sheria kuu inayosimamia mchakato huu inaeleza jinsi urithi unavyosimamiwa, kugawanywa na kuendeshwa.
Mali ya marehemu ni jumla ya mali yote, madeni, haki, na wajibu wa mtu wakati wa kifo chake.
Hii inaweza kujumuisha: Ardhi na majengo, akaunti za benki, hisa na dhamana, magari, mali ya kibinafsi kama vile vito na samani au mali nyingine yoyote aliyomiliki
Kama nilivyowahi kueleza katika makala haya, mali ya marehemu inaweza kugawanywa kupitia wosia halaliau kwa kuzingatia sheria ya urithi bila wosiaiwapo hakuna wosia alioacha.
Iwapo marehemu alitoa zawadi kubwa kwa walengwa fulani kabla ya kufariki (kama vile kuhamisha ardhi au msaada wa kifedha), zawadi hizi – zinazoitwa manufaa maalum – zinaweza kuzingatiwa na mahakama wakati wa kugawa urithi ili kuhakikisha usawa kwa warithi wote.
Watu wana uhuru wa kuuza, kutoa zawadi au kuhamisha mali yao wakiwa hai. Hata hivyo, uhamisho wowote unaokiuka maadili ya umma – kama vile njama za kudhulumu warithi halali – unaweza kupingwa mahakamani.
Mtu anaweza kugawa mali yake kupitia wosia, ilmradi wosia huo uzingatie masharti ya Sheria ya Urithi.
Hata hivyo, sheria ya Kenya inalinda baadhi ya warithi kama vile mke au mume, watoto na jamaa wa karibu dhidi ya kudhulumiwa au kuachwa nje ya wosia.
Mahakama zinaweza kuingilia kati kupitia Kifungu cha 26 cha sheria hii kutoa msaada kwa waliopuuzwa.
Kenya pia inakubali wosia wa mdomokwa mali ya thamani isiyozidi Sh30,000, ilmradi utolewe mbele ya mashahidi wawili, na anayeutoa afe ndani ya miezi mitatu tangu kutoa wosia huo.
Iwapo kuna wosia, mtekelezaji anayejulikana kwenye wosia atatekeleza ugavi wa mali lakini pale hakuna wosia mahakama humteua msimamizi.
Msimamizi au mtekelezaji huombahati ya usimamizi au hati ya utekelezaji wa wosia ili aweze kusimamia na kugawa mali.
Mali hugawanywa kulingana na wosia au sheria ya ugavi bila wosia, baada ya mpango wa ugavi kuidhinishwa na mahakama.
Migogoro ya urithi ni jambo la kawaida nchini Kenya, hasa pale ambapo hakuna wosia au warithi fulani wanahisi kutotendewa haki.
Mahakama zina mamlaka ya kutatua migogoro hiyo kwa kuzingatia mchango maalum wa mrithi, haki za waliotegemea marehemu na usawa na haki kwa wote.
Sheria ya urithi nchini Kenya inalenga kuhakikisha kuwa mali ya marehemu inagawanywa kwa haki miongoni mwa warithi, iwe kwa wosia au bila.
Ni muhimu kwa kila mtu kuelewa haki na wajibu wao ili kuepuka migogoro ya baadaye.