Mchanganyiko wa hoho, brokoli na saladi humpa kibunda cha kudondosha ute
Na CHRIS ADUNGO
AYUB Otieno, 20, hujishughulisha na kilimo cha nyanya, broccoli, mboga za saladi (lettuce) na pilipili-mboga ndani ya vivungulio (greenhouses) katika eneo la Kiondoo, Nakuru.
Mwanafunzi huyu wa masuala ya uhandisi katika Chuo Kikuu cha KCA ni miongoni mwa watu wachache wanaozidi kufurahia mafao ya kilimo wakati huu ambapo janga la corona limevuruga mipango ya watu wengi kiuchumi.?
“Niliteua kuiandama ndoto yangu ya ukulima pindi nilipokamilisha masomo ya shule ya upili. Kilimo ni jambo nililoanza kulichangmkia tangu utotoni. Tatizo kubwa wakati huo ilikuwa jinsi ya kupata mtaji,” anatanguliza Otieno ambaye pia amesomea sayansi ya data katika Chuo Kikuu cha Strathmore.
Kilimo ambacho Otieno kwa sasa anakiendesha katika shamba lake la ekari mbili kinamvunia kitita cha kudondosha mate. Anamiliki vivungulio viwili vyenye urefu wa mita 30 na upana wa mita nane.
Anatumia kimojawapo kukuzia nyanya na kingine kustawishia broccoli, lettuce na pilipili-mboga. Katika kivungulio hiki cha pili, Otieno amepanda ‘lettuce’ kwenye mistari miwili na mstari mwingine mmoja wa broccoli kwa minajili ya majaribio.
“Lettuce na broccoli hutumiwa kutengenezea saladi ambayo kwa kawaida, huliwa kwa mseto wa vitunguu na nyanya,” anaeleza.?Otieno alianza kujishughulisha na mradi huu mnamo 2018 baada ya kuhitimisha safari ya masomo ya sekondari.?“Wazazi wangu walinisaidia kupata mkopo wa benki wa Sh200,000. Nilitumia fedha hizi kuunda kivungulio cha kwanza kwa minajili ya nyanya,” anasema kwa kukiri kwamba kuwepo kwa kisima cha maji nyumbani kwao kulimfaa sana.
Katika msimu wa kwanza wa upanzi, nyanya zilimpa faida kubwa aliyoiwekeza tena kwenye kilimo hivi kwamba kufikia mwanzo wa mwaka huu, alikuwa tena ameunda kivungulio cha pili kwa gharama ya Sh300,000.
Hiki ndicho kivungulio anachokitumia kukuzia aina tatu za pilipili-mboga ambazo hutofautishwa kwa rangi; manjano (Golden Sun F1), kijani-kibichi (Grandisimo F1) na rangi ya chungwa (Orange Pepper Glow F1).?Alisimika fito zinazounda herufi ya ‘T’ ndani ya kivungulio hiki kwa minajili ya pilipili kutambalia baada ya kipindi cha miezi miwili ya kumea au pindi zinapoanza kutoa maua na kuzaa maboga au matunda.
Otieno anasema alijifunza kuhusu ukuzaji wa pilipili-mboga aliposhiriki Maonyesho ya Kilimo katika uwanja wa Nakuru mwanzoni mwa 2019. Alijisajilisha kwa programu ya mtandaoni ambayo ilimsaidia sana kufahamu mengi kuhusiana na mahitaji ya soko la mazao haya na jinsi ya kuimarisha kilimo chenyewe.
Kupitia mradi huo, alishauriwa na wataalamu kuhusu aina ya pilipili-mboga ambayo ingenawiri katika kivungulio chake baada ya udongo kufanyiwa vipimo vya kitaalamu na kiwango cha pH kubainika.
Alinunua mbegu zilizoidhinishwa kutoka kampuni ya Amiran na akazitia kwenye kitalu kisha kuhamishia miche shambani, ndani ya kivungulio, baada ya kipindi cha wiki nne ikiwa na urefu wa takriban sentimita 12.
“Miche huachwa wazi kitaluni na kiwango cha unyunyiziaji wa maji kupunguzwa siku moja kabla ya kuhamishiwa kivungulioni au shambani. Miche hupandwa ikifuata paipu za maji na nafasi ya hadi sentimita 60 baina ya mistari na sentimita 30 kati ya mche na mwingine huachwa.”
“Pilipili-mboga hupogolewa kila baada ya wiki moja ili kuhakikisha kwamba kila mmea unatumia kiasi kidogo zaidi cha maji,” anaeleza Otieno.
Mbolea ya dukani huwekwa mwezi mmoja baada ya miche kuhamishiwa kivungulioni na dawa aina ya Extrim na Vidalia kupulizwa mara moja kwa wiki ili kuzuia magonjwa mbalimbali na uvamizi wa wadudu kama vile tokonyasi, viwavi na vidukari.
Kwa mujibu wa Otieno, upogoaji wa mara kwa mara pia husaidia mimea kuzalisha matunda ya kiwango sawa huku maboga au matunda madogo au yaliyo na maumbo mabovu yakiondolewa kabisa.?Ili kuhahakisha kuwa pilipili-mboga zinastawi vyema na kusalia na maumbo yatakayovutia wateja sokoni, Otieno hunyunyizia mimea yake maji angalau mara mbili au tatu kwa wiki.
“Zikitunzwa vyema na masuala yote mengine kuzingatiwa ipasavyo, pilipili-mboga huvunwa kuanzia siku 70 baada ya upanzi na msimu wa uvunaji hudumu kwa takriban miezi miwili,” anasema.
Hata hivyo, anaonya kuwa pilipili-mboga aina ya Grandisimo F1 huanza kubadilisha rangi na kuwa ya chungwa iwapo itaachwa shambani kwa muda mrefu baada ya kukomaa.
Otieno anakiri kwamba pilipili-mboga za rangi ya kijani huwaniwa sana sokoni na ni maarufu mno miongoni mwa wakazi wa Lanet ambao huja kujinunulia mazao hayo shambani.
Kwa sababu ya kutoharibika upesi, pilipili-mboga za rangi ya manjano hupendwa sana na wateja wanaouza katika maduka ya jumla ya Woolmatt na Gilanis mjini Nakuru.
Japo kwa sasa asilimia kubwa ya mazao yake huuzwa katika masoko ya humu nchini, Otieno anapania kujitosa katika masoko ya kimataifa na kusambaza sehemu nyingine ya pilipili-mboga zake mjini Nairobi na Eldoret.
“Kilimo hiki ni nafuu zaidi ikilinganishwa na ukuzaji wa mimea mingine kama vile mahindi au nyanya. Kati ya manufaa yake ni kwamba mkulima ana uhakika wa kuwa na fedha kila wiki badala ya kusubiri pesa kwa mwaka mmoja kutokana na kilimo cha mahindi au Sh60 kwa kilo moja ya nyanya.”
Kwa wiki moja pekee, Otieno huvuna hadi kilogramu 300 za pilipili-mboga na huuza kila kilo kwa Sh200. Ina maana kwamba yeye hutia mfukoni hadi Sh60,000 kwa juma.
“Wakati huu wa janga la corona, bei ya pilipili-mboga imeshuka sana sokoni hadi kufikia Sh300 kwa kilo. Kwa kawaida, huu ni msimu ambapo bei ya mazao haya hutarajiwa kupanda na hata kufikia Sh400 kwa kilo katika masoko mbalimbali ya humu nchini.”
Otieno ambaye kwa sasa anapania kujitosa kwenye kilimo kisichohitaji udongo (hydroponics), anashauri vijana wenzake kujishughulisha na ukulima ili kubuni nafasi nyingi za ajira.
“Ninawahimiza vijana kuanza kilimo hiki kwa sababu pilipili-mboga zina soko kubwa lililo tayari siku zote na mapato yake ni ya kujivuniwa.”