Mchuuzi asukumiwa kifungo jela kwa kukiri kudanganya polisi
MCHUUZI mwenye umri wa miaka 58 aliyejiokoa kwa kudai analala kwenye jaa la takataka katika hoteli moja ya kifahari atatumikia kifungo cha mwaka mmoja kwa kutoa habari za uwongo kwa polisi.
Kishan Sachania alisukumiwa kifungo hicho na mahakama ya Milimani Nairobi baada ya kukiri aliwadanganya polisi kwamba amenyang’anywa gari na wezi waliokuwa wamejihami kwa bastola.
Hakimu alipomwuliza mshtakiwa sababu ya kudanganya, Sachania aliungama, “nimekua nikilala katika shimo la kutupa takataka katika hoteli ya kifahari hapa jijini Nairobi.”
Akaendelea, “Nilitimuliwa na walinzi katika hoteli hiyo ambapo pia nilikuwa naokota chakula. Ili nijifunike aibu niliamua kutoa habari za uwongo kwa polisi kwamba nimenyang’anywa gari langu.”
Akijibu maswali la hakimu mkuu Dolphina Alego kile anachofanya kujikimu kimaisha, ikiwa yuko na wazazi na familia, Sachania alisema “Wazazi wangu walikufa zamani. Niko na binti anayeishi nchini Uingereza pamoja na dada zangu wawili. Nauza vifaa vya elektroniki mitaani Parklands na Westlands.”
Akaendelea kufungua moyo, “Naomba hii mahakama isimpigie binti yangu na dada zangu simu. Kitendo changu ni cha aibu na sitaki wafedheheke wakiwa ughaibuni. Naomba hii mahakama iwache niubebe msalaba na mzigo wangu.”
Mshtakiwa huyo alichagua kujukumikia matendo yake baada ya kuulizwa na hakimu endapo “angelitaka msaada wa mahakama na serikali.”
Baada ya kukataa akisaidiwa Desemba 10, 2025 na korti hakimu aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa.
Ripoti ilipowasilishwa kortini Desemba 30, 2025 hakimu aliombwa na wakili Oliver Tangara asimsukumie kifungo cha jela Sachania akifichua “hoteli alipokua akilala kwenye jaa la takataka imeamua kumpa kazi, makao na chakula.”
Hata hivyo, hakimu alimsukumia kifungo cha mwaka mmoja lakini hataenda jela.
“Hii mahakama imekuhukumu kifungo cha mwaka mmoja. Wakati wa kipindi hiki hautafanya makosa. Endapo utashiriki uhalifu ukamatwe na kufikishwa kortini hii mahakama itakufunga jela makosa haya ya sasa ya kudanganya polisi kisha usukumwe jela kwa hatia hiyo mpya. Chagua ni lako kukwepa uhalifu upone,” hakimu alisema.
Mshtakiwa aliahidi kutii sheria.
Pia aliishukuru mahakama na hoteli hiyo kwa kumwonea huruma.
Sachania alikuwa amekiri kutoa habari za uwongo kwa afisa wa polisi (PCW) Elizabeth Wambui mnamo Desemba 10, 2025 katika kituo cha polisi cha Parklands Nairobi kwamba ameibiwa gari lake.
Wambui alisambaza habari za wizi huo kwa vituo vyote vya polisi gari hilo lisakwe.
Hakimu alimpa mshtakiwa siku 14 kukata rufaa endapo hakuridhika na uamuzi wake.
Wakili Tangara aliondoka na Sachania kortini kumpeleka kwenye hoteli hiyo iliyompa mshtakiwa makao na kazi.