Makala

Mfahamu Benny Hinn, mwinjilisti anayeongoza maombi nchini Jumamosi na Jumapili

February 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

LICHA ya umaarufu wake mkubwa kote duniani, mwinjilisti Benny Hinn kutoka Amerika ana baadhi ya sifa ambazo zimezua utata kumhusu.

Mwinjilisti huyo anaongoza mkutano mkubwa wa maombi katika Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi, kati ya Jumamosi na Jumapili.

Yuko nchini chini ya mwaliko wa mkewe Rais, Bi Rachel Ruto.

Maombi hayo yamefadhiliwa na serikali, na wale wanaopanga kuhudhuria wanatakikana kujisajilisha kwenye tovuti maalum ambayo imebuniwa kwa hafla hiyo.

Mwinjilisti huyo alizaliwa mnamo Desemba 3, 1952 katika mji wa Jaffa, nchini Israeli.

Alielekea nchini Amerika mnamo 1968. Baadaye, alianza safari yake katika uhubiri, hali ambayo ilimzolea umaarufu mkubwa kote duniani. mahubiri yake yakipata umaarufu wa kipekee.

Huwa anafanya mahubiri yake kupitia njia ya televisheni na mitandao.

Mahubiri yake huwafanya watu kuzungumza kwa ndimi. Mfumo wake wa kipekee wa uhuburi huwa unamzolea ufuasi mkubwa kwenye mikutano ambayo amekuwa akiongoza katika sehemu tofauti duniani. Wafuasi wake wengi wamekiri “kumwona Mungu” baada ya kuombewa.

Uwezo wa kuponya

Baadhi ya watayarishi wa mikutano yake miwili ya maombi nchini wamesema kuwa “upekee wa mahubiri na maombi yake ndizo sababu zilizowafanya kumwalika”.

Wengine huwa wanamsifia uwezo wake katika kuponya magonjwa sugu kwa watu anaowaombea.

“Niliponywa kabisa ugonjwa niliokuwa nao nilipoombewa na mhubiri [Benny Hinn],” alikiri mfuasi mmoja.

Hata hivyo, kama wahubiri wale wengine maarufu duniani, Mhubiri Benny Hinn hajakosa utata anaokumbwa nao.

Kwa mfano, baadhi ya watu huwa wanamkosoa kwa kueneza injili ya kujitajirisha.

Mhubiri huyo amekuwa akikosolewa kwa kutilia mkazo sana kiwango cha pesa ambazo watu huwa wanatoa katika mahubiri yake au makanisa yake.

Utata mwingine ambao huwa unamwandama ni madai ya kuwaponya baadhi ya watu “baada ya kuamini”.

Wakosoaji wake wanasema kuwa baadhi ya mafundisho ya miujiza ya uponyaji anayodai kuanya “haina msingi wa Kibiblia”.

Hata hivyo, baada ya shinikizo dhidi yake kuongezeka, Hinn alitangaza “kuacha mahubiri ya utajiri na kuangazia masuala ya kiroho”.

“Nimebadilisha mkondo wa imani yangu. Kuanzia sasa, nitazingatia sana masuala ya undani wa imani ya kiroho. Nitaangazia kuhusu vile Wakristo wanaweza kumkaribia Mungu kutokana na imani yao,” akasema kwenye mkutano mmoja nchini Amerika Agosti mwaka uliopita.

Licha ya kudai huwa anaishi maisha ya kikawaida, alikosolewa mnamo 1993 kwa kuishi kwenye makazi yenye thamani ya Sh100 milioni na kuendesha magari ya kifahari kama Mercedes Benz.

Ripoti ya upekuzi

Kulingana na baadhi ya ripoti za kipekuzi, imedaiwa kwamba baadhi ya maponyaji yake huwa si ya kweli.

Mnamo 2015, mfanyakazi wa gazeti la kipekuzi la ‘Inside Edition’ nchini Amerika, alijifanya ameugua ugonjwa wa kifafa. Aliombewa na mhubiri huyo na kukiri kwamba amepona. Hata hivyo, alikiri baadaye kwamba alijifanya alikuwa akiugua.

Mnamo 2007, alijipata matatani pale Seneta Chuck Grassley alipoanzisha uchunguzi kwenye kanisa lake kupitia Kamati Maalum ya Seneti ya Amerika kuhusu Fedha kufuatia ukosaji kwamba alikuwa anatumia ndege bei ghai aina ya Gulfstream G4SP kwa likizo za kibinafsi kupitia sadaka isiyotozwa ushuru.

Mhubiri huyo pia alizua utata mnamo 1999, alipodai kuonyeshwa na Mungu kwenye ndoto maelfu ya wafu wakifufuka kutoka makaburini mwao.

Kwenye mahubiri yake, aliwaambia watu waliowapoteza watu wao kugusa televisheni zao ili kuombewa wafufuke.

Jambo jingine ambao watu hawajui kumhusu Benny Hinn ni kwamba hakumaliza masomo yake ya sekondari. Alisomea katika Shule ya Upili ya Georges Vernier katika jimbo la Ontario, nchini Canada, japo hakumaliza masomo yake.

Licha ya kuzaliwa nchini Israeli, ana uraia wa Amerika na Canada.