Makala

Mganga aliyetaka kuokoa Sh18.5 milioni ‘alizolipwa na mteja’ alemewa kortini

Na SAM KIPLAGAT May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MGANGA ambaye pia anatoa tiba kwa kutumia dawa za kienyeji Jumatatu alipata pigo katika juhudi za kuokoa mali yake na kuzuia pesa zake zisitwaliwe na serikali.

Stephen Vicker Mangira ambaye anakabiliwa na ulanguzi wa fedha alikuwa anataka kupambana hadi Mahakama ya Juu kwenye kesi ambapo Sh18.5 milioni pesa taslimu zilitwaliwa kutoka kwake mnamo 2017.

Bw Mangira ambaye anadai yeye ni mganga alisema pesa hizo zilikuwa sehemu ya Sh50 milioni ambazo alilipwa na mteja wake.

Alipata pigo baada ya Mahakama Rufaa kutupilia mbali utetezi wake ambao alikuwa anataka ufike hadi Mahakama ya Juu kuhakikisha mali yake haipotei.

Kando na Sh18.5 milioni ambazo zilidaiwa kutokana na vitendo haramu, mahakama pia ilitoa amri magari yake manane ya kifahari na Sh2.6 milioni kwenye akaunti yake ya benki zichukuliwe na Mamlaka ya Kutwaa Mali Nchini (ARA).

Rufaa yake dhidi ya Uamuzi wa Mahakama Kuu ulipuuzwa na majaji watatu mnamo Oktoba mwaka jana.

Jumatatu Majaji Agnes Murgor, Dkt Imaana Laibuta na Grace Ngenye-Macharia walisema Bw Mangira pamoja na Nabil Loo Mohamed na Ali Cars walikosa kueleza kuwa rufaa yao inaibua masuala yanayozingatia maslahi ya umma na lazima yashughulikiwe na Mahakama ya Juu.

“Rufaa yao inalenga tu kutetea mali yao na pesa ambazo serikali inalenga kutwaa. Tayari kuna sheria inayozungumza kuhusu kutwaliwa kwa mali iliyopatikana kwa njia ya haramu,” ikasema uamuzi wa majaji hao.

Mganga huyo wakati wa kesi alikuwa ametishia kuroga upande wa mashtaka iwapo angelemewa kwenye kesi hiyo.

ARA ilikuwa imepinga kesi hiyo ikisema hakuna chochote kipya ambacho kiliibuliwa na Bw Mangira ambacho kinahitaji Mahakama ya Juu kuingilia kati.

Pesa na magari yake yalitwaliwa na ARA na polisi mnamo 2017 baada ya kunyakwa kwenye hoteli moja Mombasa kwa kuchapisha pesa bandia na kushiriki biashara ya mihadarati.

Wawili hao walishtakiwa na raia wa Tanzania kwa ulanguzi wa mihadarati lakini wakaondolewa kesi miaka minne baadaye wakati ambapo upande wa mashtaka ulilemewa kutoa ushahidi wa kutosha.

Kwenye utetezi wake, Bw Mangara alisema aliuza kipande cha ardhi Kericho, akaweka pesa nyingine kwenye akaunti yake kisha kubeba Sh18.5 milioni kwenye mkoba.

Alidai pia alikuwa amelipwa Sh50 milioni na mgonjwa ambaye alikuwa amemtibu kwa kutumia mbinu zake za ushirikina. Alidai alikuwa analenga kununua nyumba na pia magari mawili ya kubeba maiti kwa pesa hizo ila hakuweza kuthibitisha hilo.