• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mhubiri afunguka kuhusu fidia ya ng’ombe 25 kuepushia nduguye jela

Mhubiri afunguka kuhusu fidia ya ng’ombe 25 kuepushia nduguye jela

NA MWANGI MUIRURI

MWANZILISHI wa Palace of Integrity Ministries, Mhubiri Peter Ngumbi Mutinda, sasa amekubali alilipa zaidi ya Sh600,000 kulipa fidia katika makubaliano tata ya kumkinga nduguye mdogo asikamatwe kwa madai ya mauaji.

Pesa hizo zilitumika kumfidia Bi Teresia Wanjiku ambaye mumewe, Francis Waweru alikuwa amedaiwa kushambuliwa na genge la vijana watatu nje ya Shule ya Msingi ya Muti iliyoko katika eneobunge la Gatanga usiku wa kuamkia Mei 15, 2017, na akaaga dunia baadaye.

Mjane huyo kupitia kwa wazee waliotumwa na chifu wa kijiji chake cha Ngelelya waliafikiana kumtoza mhubiri Mutinda fidia ya ng’ombe 25 na ambao baada ya kukadiriwa bei bili ya Sh300,000 iliandaliwa.

Aidha, wazee hao, kwa mujibu wa Bi Wanjiku, walipewa Sh15,000 kama marupurupu ya kikao na pia wakaahidiwa kuchinjiwa mbuzi, ahadi ambayo hadi leo hii haijafanikishwa.

Sasa, mhubiri Mutinda katika mahojiano na Taifa Leo amekiri kwamba mmoja wa washukiwa hao wa mauaji aliishia kuwa nduguye “na mimi kama msaidizi wa kifamilia nikaona tu nitafute maridhiano na familia ya mjane ndipo niwapanguse machozi”.

Mtumishi huyo wa Mungu, alisema alifanya hivyo kwa msingi wa roho ya utu na kwa kusaidia ndugu yake asitupwe jela na “wala sio kwa makusudi ya kusaidia kutapeli mkondo wa sheria na haki”.

Akasema: “Nilitumia kitita hicho kuwapa wanafamilia hiyo fidia na pia kiasi kingine nikatumia katika safari za hapa na pale kwa sababu maafisa mjini Murang’a walitaka kujua namna mambo yanavyoendelea.”

Akisimulia jinsi mambo yalivyochacha hadi akaamua kulipa hela hizo, mtumsihi huyo amesema kwamba alipokea simu kutoka kwa babake mzazi mwendo wa saa saba usiku akilia kwamba “ndugu yangu alikuwa ameingia katika mtego wa mauaji”.

“Babangu aliniambia ndugu yangu ambaye alikuwa mhudumu wa bodaboda, alikuwa amedanganywa baada ya kununuliwa pombe na vijana wawili wamvamie Bw Waweru ambaye alikuwa mlinzi katika shule hiyo ya Muti,” akaeleza.

Mtumishi Mutinda alisema kwamba mmoja wa vijana hao wawili alikuwa akimsingizia Bw Waweru kwamba alikuwa kwa uhusiano wa kimapenzi na mama yake, na ndipo akatafuta vijana wawili mmoja akiwa ni ndugu yake, kumuadhibu.

Anasema kwamba ndugu yake alimuarifu kwamba hakuwa akijua alikuwa akipelekwa kutekeleza mauaju na alihepa eneo la uvamizi akiacha pikipiki yake nyuma.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi iliyoandaliwa katika kituo cha Ngelelya, Bw Waweru alikuwa amekatwakatwa, kupigwa, kulawitiwa na hatimaye kukanyagwa mara kadha kwa kutumia pikipiki hiyo ya vijana hao.

Aliaga dunia siku nne baadaye katika hospitali ya Thika Level Five na ndipo uvamizi huo ukageuka kuwa kesi ya mauaji.

Bw Mutinda anasema kwamba alimwelekeza baba yake awajibikie mazungumzo ya maridhiano kati ya familia yao na ile ya mwaathiriwa “na nilipopewa matokeo kwamba tungelipa fidia, nikakubaliana nao na nikatafuta pesa peke yangu hata bila ya kuhusisha familia za washukiwa wale wengine wawili na nikalipa”.

Vikao vya kukadiria gharama ya fidia viliandaliwa mnamo Mei 27, 2017, siku moja baada ya kuzikwa kwa Bw Waweru ambaye aliuawa akiwa na umri wa miaka 71, Bi Wanjiku akaelezea.

Hata hivyo, kesi hiyo imerejea kumsumbua Bw Mutinda kwa kuwa baada ya mtandao wa nation.africa  kuiangazia  mnamo Oktoba 12, 2023, wakuu wa kiusalama Murang’a waliteta.

Kamanda wa polisi wa Murang’a Bw Mathiu Kainga amesema kwamba “huo ulikuwa ukora dhidi ya haki kwa kuwa kesi zote za mauaji ni lazima ziwasilishwe mahakamani”.

Alisema kwamba yalikuwa makosa makuu kwa baadhi ya maafisa wa usalama akiwemo chifu wa eneo hilo kusuluhisha kesi ya mauaji nje ya mahakama.

Bw Kainga alisema kwamba hata ikiwa ni kuafikiana kuhusu suluhu ya fidia, mahakama ndiyo inayofaa kushirikisha wala sio vikao vya wazee au vya maafisa wa usalama wakishirikiana na wahudumu katika mfumo wa kidini.

Katika hali hiyo, Bw Kainga ameamrisha kwamba kesi hiyo ichunguzwe upya na wote waliohusika warekodi taarifa na watakaopatikana kwa lawama wafunguliwe mashtaka.

Tayari, kitengo cha uchunguzi wa makosa ya jinai cha kaunti ndogo ya Gatanga kimezindua uchunguzi na ambapo kimerekodi taarifa kutoka kwa baadhi ya familia ya marehemu na pia kwa mshirikishi wa haki za kibinadamu eneo hilo la Ithanga Bw Romano Kan’gethe.

Wengine ambao wanalengwa ni maafisa waliofika katika eneo la umavizi, waliorekodi taarifa ya tukio na pia waliopokezwa hongo katika afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ili kupisha ulipaji wa fidia.

Sasa, Bw Mutinda anasema kwamba “ningejua nilikuwa najiingiza katika janga hili la kisheria singehusika…lakini nikiitwa kurekodi taarifa nitafika na nitoe ukweli wangu kwa kuwa sikuhusika kamwe na kosa la kuvamia na kuua”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Njia ‘mboga’ ya mama mboga kumiliki nyumba za bei nafuu

Miguna Miguna amrudisha Larry Madowo darasani

T L