Makala

‘Mhubiri’ Sharlyne Anindo Temba: Malkia wa vifo kichakani kwa Bi Nzaro afichuliwa

Na MAUREEN ONGALA September 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UFICHUZI wa kushtua umejitokeza kuhusu dhehebu kali la Kwa Bi Nzaro, Kaunti ya Kilifi ambako waumini wamekuwa wakifunga hadi kufa wakiahidiwa kuwa hiyo ndiyo njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu.

Kwa mara ya kwanza maelezo ya kina kuhusu mshukiwa mkuu, ‘mhubiri’ Sharlyne Anindo Temba yameanikwa wazi na wapelelezi wa serikali.

Anindo Temba, anayetoka eneo la Emuhaya, Kaunti ya Vihiga, ndiye anayeshukiwa kuwa kiongozi wa dhehebu hilo hatari ambalo limehusishwa na mauti ya makumi ya watu kufikia sasa.

Hadi sasa, miili ya watu 34 imepatikana katika kijiji cha Kwa Bi Nzaro, msituni Chakama, Kilifi. Pia zaidi ya vipande 100 vya miili ya watu vimepatikana.

Nyumbani kwa Anindo, 30, eneo la Kaoeni kuna nyumba mbili. Waumini kutoka sehemu mbalimbali za Kenya walikuwa wakipokelewa katika nyumba hizo kabla ya kufunzwa kunga za dhehebu hilo tata.

Kaoeni si mbali na Furunzi, Malindi ambako ni nyumbani kwa mhubiri anayekabiliwa na kesi ngumu ya mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie.

Dhehebu hilo, uchunguzi umebaini huenda lina uhusiano na lile la Shakahola ambalo zaidi ya waumini 400 waliangamia kutokana na mafunzo ya itikadi kali yaliyoenezwa na Mackenzie mnamo 2023.

Wapelelezi wameeleza namna shughuli za dhehebu la Kwa Bi Nzaro zilivyoendeshwa kichinichini katika kijiji hicho, viungani mwa mji wa Malindi bila yeyote kushuku au kutambua chochote.

Walishawishiwa kwa msingi wa dini kukaa njaa, wakala kiapo cha siri na mwishowe kuelekezwa kwenye njia ya mauti.

Uchunguzi, kadhalika, umebaini baada ya Bi Temba, ambaye anaishi Furunzi, kuwapokea waumini na kuwaandaa, alikuwa akiwasafirisha hadi Kwa Bi Nzaro.

Mwanzoni alikuwa amekodisha nyumba moja lakini akaongeza nyingine kutokana na kuongezeka kwa idadi ya waumini waliotaka kuelekezwa hadi aliko Mungu.

Nyumbani kwake Kwa Bi Nzaro ambako maovu haya yalifanyika, kuna nyumba ya madongoporomoka, na nyingine ya mabati ambayo ina vyumba vitatu.

Hii inajumuisha chumba cha maandalizi na vyumba viwili vya maombi.

Chumba cha mwisho ndicho kina siri zaidi kwa sababu waumini walifunga hadi wakafa wakiwa wamelala humo sakafuni.

Baada ya kufa walikuwa wakifungwa kwa shuka na miili yao kutupwa.

Maandalizi ya mauti yalianza kwa kupewa chakula kidogo, kupunguziwa kiwango cha mlo, kupewa maji na hatua ya mwisho kuachwa ili malaika waje wazichukue roho zao baada ya kulemewa na njaa.

Mmoja wa makachero anayechunguza shughuli ya dhehebu hilo alifichua kuwa Bi Temba alikuwa akitembelea Furunzi kuwapokea waumini wapya kisha kuwaelekeza Kwa Bi Nzaro ambako walitakiwa kuanza kufunga.

Mhudumu wa bodaboda pia alikuwepo kuwasafirisha waumini wapya -shughuli iliyoendeshwa kwa siri.

Katika nyumba hizo, makachero walipata stakabadhi kadhaa ikiwemo risiti ya kununua pikipiki, makubaliano ya kununua ekari tano za ardhi kwa Sh20,000 ambapo Sh10,000 zilikuwa zimelipwa tayari.

Ununuzi huu unamhusisha Bi Temba na ardhi ambako nyumba zilizoko Kwa Bi Nzaro zipo.

Pia kitambulisho cha Lilian Akinyi, mkewe Jarius Otieno, ambao ni wanandoa kutoka Siaya, kilipatikana.

Watoto sita wa wanandoa hao hawajulikani waliko na wawili hao ni kati ya washukiwa wanaoendelea kuzuiliwa na polisi.

Bw Jairus ambaye alikosana na uongozi wa dhehebu hilo alitengwa baada ya kukataa kuzika miili ya waliofunga hadi kufa na hata mkewe kuzua maswali kuhusu imani ya dhehebu hilo akidai mtoto wake wa mwisho alifia hapo.

Baada ya kutengwa, Jarius alibahatika kuomba simu ya mmoja wa wanakijiji na kupasua mbarika kuhusu kilichokuwa kikiendelea ndani ya dhehebu hilo kwa maafisa wa usalama ndipo uchunguzi ukaanza.

“Majirani hawangeweza kugundua chochote kwa sababu shughuli za Bi Temba zilikuwa za siri na wageni walionekana tu kama watu wa kawaida.

“Mara moja moja alikuwa akiwapokea wanafamilia na walionekana tu kama rafiki zake waliokuja kumtembelea,” akasema kachero mwingine.

Kwa sasa vitengo mbalimbali vya usalama vinaendelea na uchunguzi kufahamu mengi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya dhehebu hilo.

Makachero hao wamebaini kuna mwanaume mmoja ambaye alikuwa akitembelea sana Bi Temba anayeshukiwa kuwa na ushirikiano na Mackenzie.

Wiki jana Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliamrisha kuwa uchunguzi uendelee katika ranchi yote ya Chakama ambako inakisiwa dhehebu hilo limekuwa likiendeleza mauti ya waumini wengi.