• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mhudumu bodaboda anayeendesha pikipiki kwa madoido kuvutia wateja 

Mhudumu bodaboda anayeendesha pikipiki kwa madoido kuvutia wateja 

NA KALUME KAZUNGU

AMANI Jeremiah Yaa ni mhudumu wa boda boda ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka saba sasa.

Yaa,29, ambaye ni baba wa watoto wawili, aliingilia huduma za bodaboda 2017, na wakati wote huo hadi sasa amekuwa akihudumia wakazi wa mji wa Witu na viunga vyake.

Witu ni eneo linalopatikana eneobunge la Lamu Magharibi.

Yaa anatambulika kwa wateja wake na hata wahudumu wenzake wa ndani na nje ya Witu kama ‘bodaboda wa makeke.’

Alibandikwa jina hilo kutokana na umachachari wake na vishindo katika kuifanya kazi yake ya kuendesha pikipiki.

Aidha, anatambulika mitaani na kwenye stendi yao ambapo mara nyingi utampata akizungusha pikipiki yake miguu ikiwa juu, au kichwa kikiwa kwenye kochi la pikipiki yake.

Vimbwanga hivyo vyote huvifanya muradi aonekane na wateja kwa haraka, hivyo kujipatia kazi ya kuwasafirisha watakako.

Licha ya hulka ya abiria wengi wa pikipiki nchini kuogopa boda boda wanaoonekana kuwa na vishindo au umachachari mwingi wakati wakiendesha pikipiki zao, kwa Yaa, hali ni tofauti.

Wateja wamekuwa wakimfurahia na kukimbilia huduma za jamaa huyo kwani machachari au makeke yote anayoonyesha huyafanya wakati akitafuta wateja.

Rama Kahindi, mmoja wa wateja kindakindaki wa Yaa, anamtaja mhudumu huyo wa boda boda kuwa mwendeshaji shupavu na mwangalifu barabarani.

“Bw Yaa ndiye bodaboda ninayependa kubebwa naye kila mara ninaposafiri nikiwa na mizigo. Watu wafahamu kuwa Yaa huonyesha tu umachachari au makeke yake akiwa steji lakini punde anapopata abiria kama sisi, yeye huendesha pikipiki yake kwa uangalifu mkuu, akizingatia sheria zote zinazofungamana na usalama wa barabarani asisababishe ajali, majeraha wala maafa. Ni kipenzi cha wengi hapa Witu na viunga vyake,” akasema Kahindi.

Maryam Abdi, mkazi wa kijiji cha Pandanguo kilichoko karibu kilomita 21 kutoka mjini Witu, anasema yeye pia amekuwa akitafuta huduma za Yaa kila mara anapozuru Witu Mjini kujinunulia bidhaa za nyumbani.

Abdi anasema tangu alipoanza kubebwa na Yaa hajawahi kuangushwa na mhudumu huyo hata siku moja.

“Ni kijana mngwana na mpole. Nilimjua tu kupitia makeke yake akiwa juu ya boda boda steji. Niliposikia sifa zake za uangalifu akiwa barabarani, nikajaribu kusaka huduma zake na nimezipenda. Mara nyingine huja Pandanguo kunichukua kununua bidhaa madukani Witu na kisha kunirudisha,” akasema Bi Abdi.

Amani Jeremiah Yaa, 29, akiwa ameandamana na wabodaboda wenzake kwenye kampeni ya kuhubiri amani mjini Witu, Lamu. PICHA|KALUME KAZUNGU

Mbali na kujipatia riziki kupitia kubeba abiria kwa pikipiki yake, Bw Yaa pia amekuwa akikodishwa na mashirika mbalimbali au wakati wa kampeni za kisiasa, ambapo amekuwa akionyesha madoido mbele ya hadhira, hivyo hujipatia mtaji.

“Wanasiasa, mashirika ya mazingira kwenye kampeni zao wamekuwa wakinikodisha, ambapo huonyesha weledi wangu wa kuendesha pikipiki, hivyo kunilipa kitu kidogo. Isitoshe, watu wanaohudhuria hafla hizo kujionea na kuvutiwa na maarifa yangu ya kuendesha pikipiki huishia kunitunuku hela,” akasema Yaa.

Anataja kazi ya boda boda kuwa ya tija, hasa kwa wenye nidhamu kazini.

Anasema ni kupitia kazi hiyo ambapo amefaulu kukimu familia yake, ikiwemo mkewe na wanawe wawili.

Yaa anafichua kuwa siku nzuri yeye hujizolea kati ya Sh2,000 na Sh2,500 kwa kubeba abiria na mizigo sehemu tofautitofauti za Witu, ikiwemo Pandanguo, Taa, Maisha Masha, Kipini, Moa, Katsaka Kairu, Jipendeni, Pangani, Mpeketoni, Majembeni, Kibaoni, Hongwe na kwingineko.

“Siku ikiwa mbaya hupata kati ya Sh800 na Sh1,000,” Yaa akaambia Taifa Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Licha ya umakeke wake, anasema ni kisa kimoja tu cha kuanguka amewahi kushuhudia.

Aliuguza maejeraha ya mkono.

Yaa ni mzawa wa tano katika familia ya watoto 11. Alizaliwa eneo la Kanagoni, Kaunti ya Kilifi.

Kwa sababu ya umaskini katika familia yake, aliacha masomo akiwa darasa la sita 2016 akaenda Witu, Lamu ambapo aliingilia biashara ya huduma za bodaboda.

  • Tags

You can share this post!

Maombi ya saa moja yaliyomfanya Omosh akaacha pombe na...

Maafa ya mwanamke ndani ya shamba la Kakuzi    

T L