Michango ya mitandaoni yageuka karaha kwa Wakenya wakarimu
NA WANDERI KAMAU
TANGU ujio wa mtandao wa intaneti, dunia iligeuka na kuwa kama kijiji kidogo ambapo watu wanaweza kuwasiliana kwa urahisi.
Kama mataifa na jamii tofauti katika sehemu mbalimbali duniani, Wakenya walianza kuonyesha umoja wao na hali ya kujaliana kupitia mitandao ya kijamii.
Kujaliana huko ni kuungana na kusaidia watu wanaokumbwa na changamoto tofauti za kimaisha, kupitia michango ya fedha.
Maelfu ya Wakenya wamesaidika kupitia michango hiyo; baada ya kupata usaidizi kutatua changamoto za kielimu, kiafya, ujenzi wa makanisa kati ya nyingine.
Baadhi ya watu ambao wamejijengea majina kupitia michango hiyo ya mitandaoni ni mwanamuziki Karangu Muraya, Bw Ndung’u Nyoro, Mcheshi Muthee Kiengei, Mcheshi Eric Omondi kati ya wengine wengi.
Kupitia uchangishaji pesa mitandaoni, Bw Muraya amesaidia makumi ya watu kupata matibabu bora katika mataifa ya nje kama India, huku Bw Nyoro akifanikiwa kusaidia mamia ya wanafunzi kupata ufadhili wa kimasomo kupitia Wakfu wa Affecto.
Bw Nyoro huwa anatumia kauli ‘Watoto Wasome’.
Naye Mcheshi Kiengei amefanikiwa kujengea watu wengi makazi, huku Bw Omondi akifanikiwa kuendesha masuala na miradi tofauti ya kuisaidia jamii kupitia mpango wa ‘Sisi kwa Sisi.’
Licha ya mafanikio makubwa ambayo yamekuwa yakipatikana kupitia michango hiyo, inaonekana kuanza kupata doa.
Hili linafuatia visa kadhaa ambavyo vimeibuka, ambapo watu waliochangishiwa wamedai kutopata pesa zao au wengine kudai walilaghaiwa.
Moja ya kisa hicho kinamhusu mwanamuziki Peter Mwangi, maarufu kama ‘Miracle Baby’, ambaye huimba nyimbo za mtindo wa Mugithi na Gengetone.
Kwa muda sasa, mwanamuziki huyo amekuwa akiugua na amelazwa katika hospitali kadhaa.
Zaidi ya hayo, amefanyiwa michango kadhaa na Wakenya.
Mnamo Januari 26, 2024, mwanamuziki Karangu Muraya alimchangishia Miracle Baby zaidi ya Sh1 milioni kulipia deni la hospitali alilokuwa akidaiwa.
Mkewe mwanamuziki huyo, Carol Katrue, alijitokeza na kushukuru Wakenya kwa usaidizi waliompa mumewe, ijapokuwa hakuwa amekamilisha matibabu yake.
Mchango wa pili uliongozwa na Eric Omondi, ijapokuwa pesa zilizopatikana hazikutosha kulipa deni lililobaki.
Mcheshi huyo alimrai Rais Ruto na viongozi wengine kumsaidia mwanamuziki huyo kupata matibabu bora.
Kutokana na kilio cha Bw Omondi, watu kadhaa maarufu—waliojumuisha mwanamuziki na mwanasiasa Chares Kanyi ‘Jaguar’, wanamuziki KRG the Don, Weezdom kati ya wengine wengi — ‘waliitika’ kilio cha mwanamuziki huyo kwa kumpelekea Sh300, 000 walizodai zilitolewa na Rais Wiliam Ruto.
Baadaye, Bi Katrue alijitokeza na kudai kwamba ‘macelebs’ hao hawakuwa wametumwa na Rais, bali walikuwa wakitumia masaibu ya mumewe kujijengea majina yao.
“Walikuwa wakitumia jina la Rais kujijenga!” Akafoka Bi Katrue, madai ambayo yamepingwa vikali na mwanamuziki KRG.
Bw Omondi naye anadaiwa kutomaliza kulipa deni la hospitali la mwanamuziki huyo, licha ya kupokea pesa nyingi kutoka kwa Wakenya.
Wakenya pia wamekuwa wakilalamika kwamba walipumbazwa kumchangia pesa mwanamuziki Alpha Mwanamtule, baadhi wakidai hakuwa mgonjwa.
Kutokana na hali hiyo, serikali inasema ingawa Wakenya wamekuwa wakitumia mitandao hiyo kusaidia watu wenye matatizo, ni vizuri wawe na kibali kutoka kwa maafisa wa utawala anakotoka au anakokaa mwathiriwa.
“Kama waziri anayesimamia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT)—inayosimamia matumizi ya mitandao ya kijamii—namshauri Mkenya yeyote anayelenga kuendesha michango kama hiyo kutafuta kibali kutoka kwa wizara yangu na maafisa wa utawala wa kitaifa, ili kuhakikisha watu wanaochangishiwa pesa wana matatizo ya kweli ili isiwe njia ya kupunja Wakenya,” akasema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Bw Eliud Owallo.