Mihadarati yafungia vijana wengi Kaunti ya Lamu kujiunga na jeshi
IDADI kubwa ya vijana wa Lamu walikosa nafasi ya kujiunga na jeshi (KDF) mwaka huu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, hasa bangi.
Ripoti kutoka kwa idara ya jeshi zinaashiria kuwa licha ya makurutu waliojitokeza kupita katika kila hatua muhimu iliyotakikana, walifeli pale walipofanyiwa ukaguzi wa kimatibabu, ikiwemo kupimwa mkojo na kisha kupatikana na chembechembe za mihadarati katika sampuli zao.
Zaidi ya vijana 500 walikuwa wamejitokeza kutafuta nafasi za kuingia jeshini kwenye vituo vitatu vya usajili wa makurutu vilivyoandaliwa Lamu kati ya Oktoba 13 na 15.
Vituo hivyo ni Lamu ya Kati (Uga wa Kibaki), Lamu Magharibi (Uga wa Tiger Mpeketoni) na Lamu Mashariki (Uga wa Faza).
Jumla ya vijana 19 pekee ndio waliofaulu kusajiliwa kuingia jeshini ambapo tisa (9) ni kutoka Lamu Mashariki, sita (6) kutoka Lamu Magharibi na wanne (4) wakiwa ni kutoka Lamu ya Kati.
Aidha, mwaka huu ulishuhudia vituko miongoni mwa makurutu waliojitokeza kutafuta nafasi ya kujiunga na KDF kwani kuna walioonyesha ukakamavu usio wa kawaida wakati walipoagizwa kutimka mbio kwenye awamu za kwanza kwanza.
“Mtu anaambiwa akimbie tu mbio kidogo kupasha misuli moto ila yeye anatimka kasi ya ajabu. Muda mfupi baadaye unampata amezimia huku akitokwa na jasho lisilo la kawaida. Hapo ndipo tulianza kushuku baadhi ya waliojitokeza hawakuwa sawa kabisa walipotimka mbio bali walikuwa wamevuta bangi,” akasema mmoja wa maafisa wa KDF aliyedinda kutaja jina.

Aliongeza, “Baadaye ilidhihirika wazi kwani tulipowapima wengi wao walionyesha wametumia dawa za kulevya, hasa hiyo bangi, hivyo tukawachuja.”
Katika ujumbe wake baada ya shughuli ya siku tatu ya kusajili makurutu kuingia jeshini kukamilika Lamu, Afisa Mkuu wa Masuala ya Ukaguzi wa Kimatibabu jeshini aliyesimamia Lamu, Luteni Kanali Edward Wasike, alikiri kuwa idadi kubwa ya vijana waliojitokeza walitolewa kutokana na changamoto mbalimbali miongoni mwao ikiwa ni matumizi ya mihadarati.
Licha ya kuwa na alama nzuri na pia afya njema inayohitajika kutumikia KDF, Bw Wasike aliweka wazi kuwa wengi hawangeweza kuteuliwa kwani ukaguzi wa kimatibabu ulidhihirisha walitumia dawa za kulevya.
“Unapata mtu ana alama nzuri katika KCSE, urefu nao ni ule utakikanao, mwili mzuri na nguvu zifaazo ila kitengo cha matibabu kinawafeli kwani wanapatikana wametumia dawa za kulevya,” akasema Bw Wasike.
Aliisisitizia jamii na wadau kuungana na kuendeleza hamasa kwa jamii katika kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya zinazoharibu vijana ambao ni tegemeo la sasa na katika siku za usoni.
Naye Afisa Mkuu Msimamizi wa Usajili wa KDF Lamu, Luteni Kanali Eliud Nangole, aliwasifu vijana kwa kujitokeza kwenye vituo vya usajili mapema na kwa kuzingatia nidhamu.
“Kama idara ya jeshi, tunazingatia masuala yafaayo kuteua makurutu. Ikiwa hukufanikiwa mwaka huu bado kuna nafasi zitakuja. Usichoke kujaribu. Nashukuru kwamba wengi wamejitokeza mapema vituoni. Hilo linadhihirisha wazi ari waliyo nayo katika kutaka kulitumikia taifa,” akasema Bw Nangole.
Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wanawake wa Lamu (LAWA) Raya Famau hata hivyo aliwasihi vijana kuacha dawa za kulevya kuepuka kujinyima nafasi muhimu za ajira maishani.
Bi Famau hata hivyo aliomba nafasi zaidi za kujiunga na jeshi ziongezwe Lamu miaka ijayo ili wengi zaidi wanufaike.
Chifu Mstaafu wa Lokesheni ya Kiunga, Bw Mohamed Atik hata hivyo alipinga hatua ya KDF kuwatema vijana kwenye usajili kwa sababu ya matumizi ya bangi.
Badala yake, Bw Atik aliomba kuwepo na programu maalum ya kuwasajili vijana hao na kisha kuwapitisha katika ushauri utakaowawezesha kusitisha kabisa uraibu wakati wakihudumia taifa lao jeshini.
“Si suluhu kuwanyima vijana nafasi jeshini eti kwa kuvuta bangi. Dawa za kulevya ni tatizo la nchi nzima na wala si Lamu pekee. Kuwanyima vijana ajira unawafanya iwe rahisi kwao kuraiwa kujiunga na makundi ya uhalifu,” akasema Bw Atik.