• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Miji inavyoweza kugeuzwa kuwa kitovu cha kilimo

Miji inavyoweza kugeuzwa kuwa kitovu cha kilimo

NA SAMMY WAWERU

HUKU serikali ya Rais William Ruto ikijikakamua kuangazia uhaba na usalama wa chakula nchini, maeneo ya miji pia yanapaswa kulengwa katika mjadala huo.

Mpango wa kufanikisha uzalishaji wa chakula unaegemea maeneo ya mashambani pekee, miji mikuu ikionekana kusahaulika.

Chini ya Mifumo na Teknolojia za Kisasa, ndiyo Smart Agriculture Solutions, miji inaweza kugeuzwa kuwa ngome ya ukuzaji mazao.

Kwenye maegesho ya magari, mabustani na kutani, Wilson Ndung’u, ambaye ni mwasisi wa Lavington Herbs, kampuni inayounda ‘mashamba ya kisasa’ kuendeleza kilimo mijini, anasema si ajabu miji ikizalisha chakula chungu nzima.

Wakulima wakihamasishwa kuhusu mifumo ya kisasa kuendeleza kilimo mijini. PICHA|SAMMY WAWERU

Anataja matumizi ya vertical gardens (mashamba ya ghorofa yaliyoundwa kwa kutumia paipu – PVC), storey gardens (karatasi ngumu za nailoni zilizoundwa kuwa mashamba ya ghorofa ya mduara) na pia mitungi ya maji iliyogawanywa, kama bunifu ambazo zinaweza kutumika kukuza mboga, matunda na mseto wa viungo vya mapishi.

“Ni teknolojia na bunifu ambazo zinadhibiti na kupunguza matumizi ya maji kwa kiwango kikubwa, hasa msimu wa kiangazi na ukame,” Wilson anasema.

Mashamba ya ghorofa (vertical gardens) yanayoweza kutumika kukuza mboga, matunda na viungo vya mapishi mijini. PICHA|SAMMY WAWERU

Isitoshe, mifumo hiyo ya kisasa inafanikisha oparesheni dhidi ya wadudu na magonjwa.

Dkt James Koske, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) anapigia upatu teknolojia za mabustani, akisema ni njia mojawapo kugeuza miji kuwa kijani.

“Tunapozungumza kuhusu ‘Greening Cities’, bunifu hizo zinachangia pakubwa hususan katika kuangazia uhaba na usalama wa chakula,” Dkt Koske anasema.

Ni mifumo ambayo ikikumbatiwa itasaidia kuangazia athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

  • Tags

You can share this post!

Utakachokatwa kwenye mshahara kwa ajili ya bima mpya ya...

Picha za CCTV zaonyesha dakika za mwisho za Dkt Kiptoo...

T L