Makala

Mikataba ya dijitali kati ya wazazi na matineja na athari zake

Na  BENSON MATHEKA November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Uhusiano kati ya mzazi na mtoto sasa umejengwa juu ya mawasiliano ya kudumu – saa 24 kwa siku kupitia simu za mkono.

Wazazi wengi husema wanawapa watoto wao simu za mkono wakilenga kuwa na “amani ya moyo,” kwa kuwa wanaweza kuwasiliana nao kila wakati kujua iwapo wako salama.

Lakini vijana wanachukuliaje hali hii mpya inayofahamika na wataalamu wa malezi kama mkataba wa kidijitali kati ya wazazi na watoto wao matineja? Mkataba huu unawaruhusu kutoka nyumbani peke yao tu iwapo wataahidi kubeba simu kila wakati na kujibu mara moja kila ujumbe au simu kutoka kwa wazazi wao.

Wale wanaofanya kazi na watoto lazima waelewe shinikizo wanazokabiliana nazo chini ya mfumo huu wa uangalizi wa kila wakati, hasa wanapofikia utineja – kipindi ambacho uhuru na kujitegemea ni hatua muhimu ya kimaendeleo.

Wataalamu wa malezi dijitali, walimu, na wale wanaofanya kazi na matineja wanapaswa kuelewa jinsi  kutegemea simu kupita kiasi kunavyoweza kupunguza mawasiliano ya kweli kati ya wazazi na watoto na hata kudhoofisha uaminifu wao.

“Simu za kisasa zimeunda hali mpya ya kijamii ambapo mtu anaweza kufikiwa popote alipo, bila kujali anafanya nini. Wazazi wengi hulalamikia watoto wao kupokea ujumbe wakati wa muda wa familia, lakini kwa uhalisia, sasa ni wazazi wanaoendeleza tabia hii kwa kuwataka wajibu majibu simu mara moja wanapowapigia,”asema mtaalamu wa malezi dijitali, Tracy Makiel.

Mtaalamu huyu anasema katika utafiti wake kuwa kwa vijana wengi, kuongea na wazazi wao ni sehemu ya kujifunza jinsi ya kujijali katika maeneo ya umma huku wakijenga mahusiano yao binafsi. Hata hivyo, njia hizi za kidijitali za kuwasiliana pia hutoa nafasi kwa  mitandao ya wahalifu kufikia taarifa binafsi za familia wakati ambao wazazi wanahofia usalama wa watoto wao mtandaoni.

Kwa njia hii, watoto wanatambulishwa kwa utamaduni mwingine wa kidijitali  bila kufahamu- ule wa kutoa taarifa zinazoweza kufanya wahalifu kuwafuatilia.

Makiel anabainisha kwamba ingawa wazazi husema wanawasiliana kwa sababu ya usalama wa watoto, mara nyingi hufanya hivyo ili kuhakikishia kuwa watoto wao bado wako mtandaoni na wanajibu.

Wengi wa vijana waliohojiwa katika utafiti uliochapishwa katika jarida la Psychology Today walisema wazazi wao huwapigia au kutuma ujumbe hata wakiwa darasani – si kwa dharura, bali ili kuhakikisha tu kuwa wako “hewani.”

Ripoti yake inasema, “uhusiano wa kidijitali unaotarajiwa kutoa hisia ya usalama, mara nyingi huleta hisia tofauti kabisa na ile iliyokusudiwa.”