Mila zinavyoongeza mzigo wa gharama ya mazishi
NA BENSON MATHEKA
MILA za jadi zinazokumbatiwa na baadhi ya jamii za humu nchini zimefanya shughuli za mazishi kuwa ghali mno.
Kulingana na desturi za jamii nyingi nchini, shughuli za mazishi huambatana na sherehe chungu nzima, huku waliofiwa wakifanya juu chini kumzika marehemu kwa njia ya kipekee.
Familia nyingi huchukua fursa hii kuandaa sherehe ya kupendeza, ili kuonyesha umoja na uwezo wao wa kifedha.
Pengine hakuna jamii zinazotambuliwa nchini kwa mazoea haya, kama zile za kutoka Nyanza na Magharibi. Mbali na gharama kubwa ya usafiri hadi maeneo ya mashambani, kiasi kikubwa cha pesa hutumika kufanikisha shughuli zingine za kimila zinazotekelezwa mtu akifa.
Sherehe hizi hufanya waliofiwa kubaki na madeni chungu nzima baada ya shughuli za mazishi kukamilika.
Mojawapo ya sababu inayochangia gharama ya mazishi kuongezeka ni desturi ya kale inayoilazimu familia ya marehemu kuusafirisha mwili wake hadi alikozaliwa.
“Hii ni mila ambayo imefanya gharama ya mazishi kuwalemea watu wengi. Inafaa kuangaliwa upya,” asema kasisi Jonah Obonyo wa kanisa la Cathedral of Praise jijini Nairobi.
Inaaminika kuwa, uamuzi wa familia ya mhusika kwenda kinyume na itikadi za mila huwaletea laana watoto na jamaa za marehemu.
Kwa familia zisizo na uwezo wa kifedha gharama za kufanikisha shughuli hii huwa ghali mno, na hivyo kusababisha miili ya jamaa zao kukaa katika vyumba vya kuhifadhi maiti kwa muda mrefu.
Ili kuepuka fedheha hii, jamii nyingi huishia kuomba usaidizi kutoka kwa wahisani, kupitia michango ya harambee.
Ingawa hapo awali michango hii ililenga kusaidia familia ya marehemu kuandaa mazishi , kumekuwepo na tashwishi kuhusu shughuli hizi, huku manung’uniko yakichipuka kuwa, kunao jamaa wanaochukulia fursa hii kujifaidisha.
Migogoro ya kifamilia kuhusu atakapozikwa marehemu pia huongeza gharama ya mazishi. Obonyo asema ipo haja ya jamii za humu nchini kukumbatia mabadiliko ya wakati ikiwa gharama ya kuandaa mazishi itapungua.
“Itakuwa vigumu kwa masikini kumudu gharama ya mazishi ikiwa mila hizi zitaendelea kutawala wengi,” asema.
Kampuni za humu nchini zimejitahidi kuwapunguzia Wakenya gharama ya kuandaa mazishi. Kupitia mpango wa bima familia zilizofiwa sasa zinaweza kuwazika wapendwa wao bila kulemewa na gharama ya mazishi.
Wanaonunua bima husafirishiwa mwili kutoka sehemu ulipo hadi kunakofanyika mazishi.
“Hii inaamanisha kuwa, sasa kila mtu ana uwezo wa kufanyiwa mazishi ya heshima, bila kujali hadhi yake katika jamii,” asema Violet Omondi, mama wa watoto watatu kutoka Siranga, Ugenya mkoani Nyanza.
Mamake alipofariki tayari alikuwa amenunua bima ya mazishi siku 22 kabla ya kifo chake.
“Familia yetu ilikuwa ya kwanza kufaidika na huduma hii ilipoanzishwa Kenya,” aeleza Bi Omondi
Bi Omondi asema bima hiyo ilishughulikia gharama zote za mazishi, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza, maua, kulipa bili ya kuhifadhi maiti mochari na gharama ya usafiri.
“Mazishi ya mamangu yaliandaliwa kana kwamba alikuwa afisa mkuu serikalini, licha ya kuwa mwanakijiji wa kawaida,” asema Bi Omondi ambaye wakati huo hakuwa na ajira.