Makala

Milima ya mchanga mweupe Shella Beach yageuzwa uwanja wa malavidavi

April 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

MIINUKO ya mchanga mweupe eneo la Shella kisiwani Lamu miaka ya hivi karibuni imegeuzwa kuwa chemichemi ya malavidavi kwa wanaopendana au kuchumbiana.

Mandhari ya milima ya mchanga mweupe ni ya kipekee kwani ni yenye kuvutia kwa macho, kufariji au hata kuburudisha nafsi, hasa kwa wale wanaofika sehemu hiyo.

Ikumbukwe kuwa milima au miinuko hiyo ya mchanga mweupe ni muhimu kwa wanakisiwa cha Lamu kwani ndiyo chemchemi ya pekee ya maji safi ya kunywa yategemewayo na wakazi zaidi ya 30,000 wa miji ya Lamu, Shella, Matondoni, Ras Kitau na viunga vyake.

Vyanzo hivyo vya maji eneo la Shella viko kwenye ardhi ya muinuko iliyopanuka kwa zaidi ya kilomita 12 na ukubwa wake mraba ukiwa karibu ekari 2,300 na urefu wa juu wa zaidi ya mita 60.

Kwa kawaida, hasa nyakati za asubuhi au magharibi inapowadia, milima hiyo ya mchanga mweupe ya Shella huwa na mandhari ya kuvutia ambayo hukolezwa zaidi, hasa wakati jua la macheo au lile la machweo linapochomoza au kutua.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa ni kutokana na mandhari hayo sufufu ambapo wengi wanaopendana wamekuwa wakivutiwa kuja kukutanika milimani kunogesha mahaba yao.

 

Milima au miinuko ya mchanga mweupe ipatikanayo eneo la Shella Kisiwani Lamu. Miaka ya hivi punde milima hiyo imegeuzwa kuwa chemichemi ya malavidavi kwa wapendanao. Picha|Kalume Kazungu

Aidha kuna wale ambao wameshuhudiwa wakivalishana pete za kuchumbiana kwenye sehemu mojawapo ya milima hiyo.

Kuna walioshuhudiwa wakipokezana ahadi za kugandana kama kigaga kwenye huba, daima dawamu wakati wakiwa wamepiga magoti au kushikana kwa upendo miinukoni hapo.

Isitoshe, kuna kundi lingine la wapenzi ambao wanaposhuhudia purukushani kwenye mahusiano yao huishia kufanya matembezi maalumu milimani kutazama mazingira hayo ya asili, hivyo kuwawezesha kuondoa msongo wa mawazo na presha za ulimwengu na hatimaye kutatua tofauti zao kiurahisi na hata kuzizika kwenye kaburi la sahau.

Bw Ali Abdalla, mkazi wa Shella, alikiri kuwa miaka ya hivi punde imedhihirisha bayana jinsi milima ya mchanga mweupe ipatikanayo eneo hilo imekuwa kiungo muhimu, si kwa kutoa maji yatumiwayo kuendeleza uhai tu kisiwani bali pia ni chemichemi ya mahaba kwa waja, iwe ni wenyeji wa Lamu, wageni, watalii wa ndani kwa ndani na hata wa kimataifa.

“Twafuraha jinsi mazingira tamu ya milima yetu ya mchanga mweupe hapa Shella yanavyozidi kutumiwa na waja kutekeleza majukumu muhimu ya kimaisha. Utapata wapenzi wakiitumia milima yetu kama sehemu ya makutano, kuchumbiana, kuvalishana pete au kufika tu kwa lengo la kuongeza nakshi au kunogesha mahaba yao huku wakitazama mandhari haya sufufu,” akasema Bw Abdalla.

Wanandoa watalii wa kimataifa, Bw Benjamin Liam,35, ambaye ni raia wa taifa la Canada, na mkewe, Bi Emilia Ahti, 30, ambaye ni kutoka nchini Finland, walikiri kuwa na kumbukumbu njema kuhusu miinuko hiyo ya mchanga mweupe ya Shella.

Bw Liam alifichua kuwa miaka mitano iliyopita alisafiri yeye na mchumba wake Bi Emilia kutoka mataifa yao hadi Lamu.

Anasema siku moja akaamua kumtembeza mchumba wake, Bi Emilia kwenye miinuko hiyo ya mchanga mweupe kipenda roho huyo asijue fika kuwa kipenzi chake, Bw Liam alitaka kumshtua kwa kumvisha pete ya kutaka waoane.

Mmojawapo wa miinuko ya mchanga mweupe Shella, Lamu. Picha|Kalume Kazungu

“Tulitembea kwa miguu kutoka hoteli moja ya Shella ambayo ilikuwa makazi yetu. Tukafika milimani majira ya saa kumi na moja unusu hivi jioni. Miale ya jua lililokuwa likitua na kuitandika milima ilileta mandhari ya kuridhisha si haba. Na hapo ndipo nikapiga magoti mbele ya kipenzi changu Emilia nikiwa nimeshikilia pete. Mengine ni historia tu,” akasema mzungu huyo huku akicheka na mkewe kuashiria mengi mema yaliyotendeka kwa wakati huo.

Bi Hawa Athman alisema limekuwa jambo la kawaida kila unapozuru miinuko hiyo ya Shella kuwapata wapenzi wawili wawili wakiwa wamejibanza pembezoni wakijadiliana na kutafakari ya mbeleni kuhusu uhusiano wao.

Familia, ikiwemo bibi na bwana na watoto, pia mara nyingi utazipata zikifanya ziara zao, ikiwemo kutembea au hata kujiburudisha kwa vyakula juu ya miinuko hiyo ya mchanga mweupe.

“Sisi tumeifanya kuwa desturi yetu kama familia kufika maeneo haya ya milima kujivinjari. Tunatembea miinukoni na kuchoka kabisa. Baadaye tunajibanza pahali na kula pamoja. Ni jambo jema kwetu, hasa nyakati za wikendi baada ya juma zima la pandashuka za kikazi kama wazazi na masomoni shuleni kwa watoto wetu wanafunzi,” akasema Bi Athman.

Wapenzi pia wamekuwa wakionekana wakifanya mazoezi ya mwili wakiwa wawili wawili, iwe ni kuipanda milima hiyo ya mchanga mweupe aste aste au kushuka mbio, ilmradi viungo vya mwili vipashike makali na jasho kuwatiririka wakizichoma kalori.