Makala

Mipango maalum kukabiliana na dhuluma na ukatili dhidi ya watoto

Na NYABOGA KIAGE July 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU katika Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii, Bw Joseph Motari amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha mikakati kukomesha ukatili dhidi ya watoto.
Bw Motari alisema kuwa wizara hiyo itazidi kutetea watoto na kuomba rasilimali zaidi kutoka kwa serikali kuu ili kuhakikisha mikakati yote inawekwa ili kuzuia ukatili dhidi ya watoto nchini.
“Tumepiga hatua kubwa katika harakati za kukabiliana na visa vya ukatili dhidi ya watoto nchini,” alisema.
Kulingana na Bw Motari, kuna haja ya kuingilia kati mikakati na juhudi za ushirikiano katika sekta mbalimbali zinazoshughulikia masuala yanayoathiri watoto.
Alisema kwa sasa kuna mpango unaoendelea kuboresha mikakati hiyo.
Ni Mpango wa Inua Jamii ambao umekuwa ukisaidia karibu watoto 1.6 milioni hasa mayatima, wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapa mahitaji muhimu ya kimsingi kila mwezi.
“Mpango huu unalenga kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Mpango wa Kuboresha Lishe kupitia Fedha na Afya katika Elimu (NICHE) unasaidia zaidi kaya zenye mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitatu, na kunufaisha zaidi ya kaya 33,000 tangu 2020,” alisema Bw Motari.
Katibu Motari pia alisema kuwa eneo jingine muhimu ambalo wanaangazia ni kupambana na unyanyasaji kingono kwa watoto mitandaoni.
Alisema kuwa serikali imeandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Kazi wa Taifa kuhusu suala hilo.
“Maafisa wamefunzwa kuzuia na kukabiliana na itikadi kali za kikatili, na kuongeza juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya itikadi hizo,” alisema.
Ukatili dhidi ya watoto unajumuisha aina mbalimbali za unyanyasaji wa watoto, ikiwa ni pamoja na kutelekezwa, unajisi, unyanyasaji wa kimwili na kihisia, na mila mbaya za kitamaduni.
Athari zake ni kubwa na husababisha majeraha ya kimwili, kiwewe cha kisaikolojia na matokeo mabaya ya afya kwa watoto.
Kwa miaka mingi, Kenya imejikita zaidi katika kubainisha mikakati madhubuti kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto.
Mwaka 2010, Kenya ilishiriki katika Utafiti wa kwanza wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana (VACS), ambao ulifichua viwango vya kutisha vya ukatili dhidi ya watoto.
Baadaye, Kenya ilitengeneza Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Unyanyasaji dhidi ya Watoto 2013-2018, ukitoa mfumo wa kina wa kuzuia na kukabiliana na hali hiyo.
Mwongo mmoja baadaye, uchunguzi wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto nchini Kenya uliofanyika 2019 ulionyesha kupungua kwa kiwango kikubwa cha unyanyasaji dhidi ya watoto, hasa katika unyanyasaji wa kingono na kimwili.