Makala

Miradi hewa ilivyoacha watoto wakisomea katika mazingira duni Kilifi

Na MAUREEN ONGALA February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAMIA ya wanafunzi wa chekechea katika Kaunti ya Kilifi wanasomea katika mazingira duni kwa sababu ya ukosefu wa madarasa.

Imebainika kuwa, shule nyingi za chekechea zilizounganishwa na shule za msingi huwa zimetelekezwa huku viongozi wa kisiasa hasa madiwani wakipendelea zaidi ujenzi wa shule mpya ambazo huishia kutotumiwa ipasavyo kwa kukosa rasilimali za kutosha.

Wazazi walio na watoto katika shule ya chekechea ya Muryachakwe iliyo Wadi ya Sokoke, eneobunge la Ganze, walilalamikia ahadi nyingi kutoka kwa serikali ya kaunti ambazo hukosa kutimizwa.

Darasa la Forodhoyo ECD ambapo wanafunzi 52 wa PP1 na PP2 wamelazimika kusoma pamoja kwa sababu ya ukosefu wa madarasa. Picha|Maureen Ongala

Watoto hapo walihamishwa kutoka kwa jengo lililokuwa hatari kwa maisha yao na sasa hawana darasa. Katika Shule ya Forodhoyo, ujenzi wa darasa la chekechea ulikwama miaka mitatu iliyopita.

Watoto hutegemea darasa lililojengwa kwa udongo bila madawati wala walimu wa kutosha.

“Inasikitisha kuwa watoto wa PP1 na PP2 ambao umri wao ni tofauti, wanajazwa pamoja ndani ya darasa moja kwa vile ujenzi ulikwama,” akasema Bi Rachael Kahaso, mwanachama wa kamati ya chekechea katika shule hiyo.

Kabla wapelekwe katika darasa la sasa ambalo kuta zake za udongo zina mashimo, watoto walikuwa wakifunzwa katika darasa jingine ambalo liliporomoka.

“Wakati mwingi watoto wetu huugua mafua kwa sababu ya vumbi,” akasema Bi Christine Sidi, mzazi. Hali sawa na hii hushuhudiwa katika shule ya Bogamachuko.

Kulingana na wazazi, uzinduzi wa kujenga madarasa mawili ya chekechea ulifanywa mwaka uliopita ila hakuna ujenzi wowote uliofanywa hadi sasa.

“Diwani na mkandarasi hawajawahi kurudi na hakuna kazi yoyote imefanyika kufikia sasa,” akasema.

Wanafunzi wa chekechea hutumia madarasa ya zamani ambayo yaliachwa na wanafunzi wa shule ya msingi, baadhi yakiwa bila paa. Wengine wao hufunzwa chini ya miti.

Diwani wa Sokoke Thaura Mweni, alikiri kwamba kuna shule nyingi ambapo madarasa yalifaa kujengwa lakini miradi hiyo ikakwama.

“Tulianza kujenga madarasa mawili Migumoni lakini mkandarasi hajaanza, madarasa mawili Kahingoni ambapo mkandarasi aliondoka na kuna mradi uliokwama Forodhoyo ambapo hatuna mkandarasi hadi sasa,” akaeleza.

Jengo lililo katika hali mbaya katika Shule ya Msingi ya Muryachakwe eneo la Sokoke ambalo lina afisi ya mwalimu mkuu na madarsa. Picha|Maureen Ongala

Alisema miradi hiyo mingi iliachwa nje katika bajeti ya ziada.

Kulingana na Waziri wa Elimu katika Kaunti Felkin Kaingu, kumekuwa na changamoto katika idara ya ununuzi wa mali za umma.

Bw Kaingu alisema karibu asilimia 75 ya shule za chekechea zilizounganishwa na shule za msingi ziko katika hali duni inayohatarisha maisha ya watoto.

Bw Kaingu alisema madiwani walianzisha shule nyingi za chekechea bila kuzingatia kuwa, kulikuwa tayari kuna madarasa ya chekechea ndani ya shule za msingi.

Alieleza kuwa, idara ya elimu ilitenga Sh156 milioni kukamilisha ujenzi wa madarasa uliokwama.

Baadhi ya miradi ilikwama kwa sababu ya mizozo ya ardhi au kwa vile wanakandarasi walikuwa hawajalipwa na kaunti.

“Kuna miradi zaidi ya 150 iliyokwama ya shule za chekechea. Tumeweka uzito kwa suala la kukarabati shule hizo zilizo ndani ya shule za msingi ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira mazuri,” akasema.