Miradi inayoshushia Rais hadhi pindi anapoteketeza mamilioni kwenda kuizindua
RAIS William Ruto amekosolewa kwa mazoea ya kufanya ziara zinazogharimu pesa nyingi kukagua, kuanzisha au kuzindua miradi midogo yenye thamani ndogo.
Kuanzia usafiri, gharama ya mahema, hadi matumizi ya mafuta na safari za helikopta, ziara hizi zimeibua maswali kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha za umma wakati taifa linakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, anatetea ziara hizo akisema ni muhimu kwa kufuatilia maendeleo.
“Kiongozi lazima awe karibu na wananchi ili asikie kilio chao na mawazo yao, ili afanye maamuzi yanayowanufaisha kwa maana ni wao waliompa mamlaka,” alisema.
Katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilionyesha kuwa, serikali ya kitaifa ilitumia Sh27.2 bilioni kwa usafiri.
Kuna haja gani kwa Rais kutoka Nairobi, akiandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa serikali, kukagua mradi mdogo kama ujenzi wa madarasa? – Mtaalamu wa masuala ya Uongozi Barasa Nyukuri
Viongozi wa vyeo vya juu walitumia Sh8.1 bilioni kwa safari za ndani na Sh9.2 bilioni kwa safari za kimataifa yakiwa matumizi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini.
Ofisi ya Rais iliongoza kwa matumizi ya Sh1.7 bilioni, ongezeko la asilimia 28 kutoka mwaka uliotangulia.
Katika ziara za hivi karibuni za Rais maeneo ya Nyeri, Murang’a na Laikipia, waendesha pikipiki (boda boda) walilipwa Sh1,000 kwa siku, huku raia wa kawaida wakipewa Sh500 kila mmoja.
Siku ya kwanza ya ziara yake Mlima Kenya, Aprili 1, 2025, Rais aliweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa madarasa 10 katika Shule ya Msingi ya Nanyuki DEB, eneo bunge la Laikipia Mashariki, kaunti ya Laikipia.
Baadaye siku hiyo, alikagua ujenzi wa Soko la Kisasa mjini humo litakalogharimu Sh350 milioni kabla ya kukagua ua wa kudhibiti wanyama pori katika hifadhi iliyoko Rumuruti eneo bunge la Laikipia Magharibi.
Katika eneo la Naromoru, kaunti ya Nyeri, Rais Ruto aliongoza shughuli ya kupeana hatimiliki za mashamba, akazindua miradi ya uwekaji umeme maeneo ya mashambani na kukagua ujenzi wa soko jipya la Naromoru.
Mnamo Aprili 4, 2025 kiongozi wa taifa, aliyeandamana na maafisa wakuu serikali na wanasiasa, alikagua ujenzi wa miradi ya unyunyiziaji ya Kaihi na Maragua Ridge katika kaunti ya Murang’a.
Katika eneo la Mt Kenya Mashariki, Rais Ruto alizindua mradi wa kutakasa maji katika eneo bunge la Mbeere Kusini, kaunti ya Embu, kabla ya kuweka mifereji ya maji ya urefu wa kilomita 26 katika mradi wa maji wa Bwawa la Kamburu.
Mjini Embu, Rais Ruto alikagua mradi wa ujenzi wa soko la kisasa utakaogharimu Sh300 milioni.
Alielekea katika kaunti jirani ya Tharaka Nithi ambapo alifungua rasmi jengo la kuendeshea shughuli za masomo katika Chuo Kikuu cha Tharaka kabla ya kukagua mradi wa ujenzi wa Soko la Gatunga, utakaogharimu Sh60 milioni na kufaidi zaidi ya wafanyabiashara 200.
Dkt Ruto na ujumbe wake, walisafiri kwa helikopta, magari ya kifahari, yote ambayo yalikadiriwa kugharimu mamilioni ya fedha.
Aidha, kila alikoenda, Rais Ruto na ujumbe wake walisindikizwa na wanabodaboda na umati wa watu, wengi wao, waliosemekana kulipwa pesa nyingi.
Kabla ya ziara yake ya Mlima Kenya, kiongozi wa taifa alifanya ziara ya siku tano katika kaunti ya Nairobi, mnamo Machi, ambapo alikagua na kuzindua miradi mbali, miongoni mwao iliyotekelezwa na serikali ya kaunti na Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF).
Kwa mfano, katika eneo bunge la Dagoreti Kusini, Rais Ruto alitangaza kuwa serikali kuu itatwaa mradi wa upanuzi wa Hospitali ya Mutuini hadi kiwango cha Level 5.
Lakini kabla ya ziara yake, Serikali ya kaunti ya Nairobi ilikuwa imetenga Sh238 milioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025 kwa mradi huo huo wa upanuzi wa hospitali hiyo.
“Nimemwambia Gavana Johnson Sakaja aniachie hii hospitali. Aliniambia kuwa inahitaji Sh230 milioni na baada ya wiki mbili kuanzia sasa nitatuma mwanakandarasi akamilishe kazi hiyo. Nitakuja hapo kuizindua rasmi,” Rais Ruto akaeleza.
Mradi huo ulikuwa umekwama kwa miaka kadhaa baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS).
Miongoni mwa miradi ambayo Rais Ruto alizindua na kukagua wakati wa ziara hiyo ni ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mabatini, katika eneo bunge la Mathare.
Aidha, aliahidi kujenga madarasa matano zaidi katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Teresa.
Rais Ruto pia alikagua mpango wa lishe shuleni katika shule mbalimbali jijini akimuahidi Gavana Sakaja kwamba, atanunua mtambo wa kutengeneza chapati milioni moja kwa siku, kupiga jeki mpango huo.
Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uongozi Barasa Nyukuri, ni ubadhirifu wa rasilimali za umma kwa kiongozi wa taifa kuzuru maeneo mbalimbali kukagua miradi ya maeneo kwani kazi hiyo inaweza kutekelezwa na maafisa wa serikali katika maeneo husika.
“Kuna haja gani kwa Rais kutoka Nairobi, akiandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa serikali, kukagua mradi mdogo kama ujenzi wa madarasa?” anahoji.
“Kimsingi, Rais huwateua mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wengine wakuu kumsaidia katika kazi ya kufanikisha utekelekezaji wa sera zake. Kwa hivyo, sio lazima kwake kufanya kila kitu,” Bw Nyukuri anaeleza.
Lakini Mwakilishi wa Kike wa Laikipia Jane Kagiri, anapinga kauli hii akisema kama kiongozi wa nchi, ni wajibu wa Rais kuzuru kote kukagua miradi ambayo yeye mwenyewe aliwaahidi raia wakati wa kampeni.
“Rais Ruto atakapokuwa akifanya kampeni tena kuomba nafasi ya kuhudumu muhula wa pili, ni yeye ataulizwa maswali na wapiga kura ikiwa ametekeleza miradi ambayo aliahidi.
Hao maafisa wengine hawataulizwa, kwa hivyo ni sharti Dkt Ruto afike katika kila pembe ya taifa hili kujionea jinsi ajenda inavyotelezwa,” anaeleza Bi Kagiri ambaye ni mmoja wa wandani wa Rais Ruto kutoka Mlima Kenya.