MIRADI MASHINANI: Mradi wa kaunti kuvipa vikundi ng'ombe waanza kuleta ufanisi
Na SAMUEL BAYA
UFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa ni mojawapo ya ukulima ulio na faida nyingi.
Na kwa sababu hiyo, makundi na hata watu binafsi wameendelea kushabikia ufugaji huu na kujipatia chumo zuri la kusukuma maisha yao.
Hali hii imejidhihirisha wazi katika maeneo mbali mbali ya Pwani kama vile katika kaunti ya Kilifi ambapo makundi yameibuka vijijini yakiuendeleza kwa bidii.
Tulipozuru baadhi ya vijiji hivyo hivi majuzi, tulikumbana na wakulima wakiendelea na shughuli za kufuga ng’ombe ambao wamepatiwa na idara ya mifugo ya kaunti kujiendeleza.
Katika kijiji cha Kibokoni karibu na mji wa Malindi, tulimpata Dama Gabriel akimshughulikia ndama, bomani mwake.
Ndama huyo ni mmoja wa wale kikundi chao kilipokea Machi 2019.
Yeye ni mwanachama wa kikundi cha Nyota Women Group ambacho kilianzishwa mapema mwaka 2019 kwa lengo la kuwainua akina mama kimaisha.
“Tulianzisha kikundi hiki mwanzoni mwa mwaka huu na mwezi wa Machi, tukapatiwa ndama mmoja na idara ya mifugo ya kaunti ili tuweze kujiinua kimaisha. Tuko wanachama kumi na tuna matumaini kwamba ndama huyu akianza kuzaa tutafaulu na kubadilisha maisha yetu,” akasema Dama.
Katika kijiji jirani cha Mtangani tulikutana na Zaituni Isa, mwenyewkiti wa kikundi cha akina mama kinachojulikana kama Amkeni Mtangani Women Group.
Hiki ni kikundi ambacho kinahusisha wakulima wadogo wadogo kujiendeleza kimaisha.
“Mwezi wa Machi tulipata ndama wawili kupitia kwa kitengo cha mifugo cha kaunti. Matumaini yetu ni kuwa ndama hao wakikomaa na kuzaa tutaweza kuuza maziwa kwa wingi na kujiendeleza kimaisha,” akasema Bi Isa.
Mwekahazina wa kikundi hicho Bi Asha Kitsao alisema kuwa mradi huo utawasaidia pakubwa kujikimu kimaisha.
“Tulipoulizwa na idara ya kilimo na mifugo kama ni mradi gani ambao tungetaka, tuliomba tuletewe ng’ombe wa maziwa. Tunajua kwamba huu ni aina ya ufugaji ambao kamwe hauwezi kutuangusha,” akasema Bi Kitsao.
Bi Rebbeca Wanyama ambaye pia ni mmoja wa wanachama wa kikundi hicho alisema kuwa mradi huo wa ufugaji uliwafikia kwa wakati wake na utamsaidia sana yeye pamoja na kizazi kitakachokuja.
“Tangu tupate mradi huu matumaini yamekuwa mengi na tunafanya bidii kuwalisha na kuwafuga ndama hawa. Wakianza kutoa maziwa, basi tunaamini kwamba maisha yetu yataimarika zaidi,” akasema.
Mzee wa kijiji cha Mitangani Bw Stephen Ponda alisema kuwa mradi huo wa ng’ombe wa maziwa utaboresha maisha ya wakazi katika eneo hilo.
“Tangu ndama hawa waletwe hapa, akina mama hawa wamekuwa wakifanya bidii kuwalisha na kijiji chote kinatarajia mengi wakianza kutoa maziwa,” akasema Bw Ponda.
Mwenyekiti wa kikundi cha Sabaki Community Development Project (SCDP) Mzee Charo Kahindi alisema mradi huo wa ufugaji umeleta matumaini mengi kwa wakulima katika eneo hilo.
“Mwezi wa Machi, kitengo cha ukulima na mifugo katika serikali ya kaunti kilituletea ng’ombe 50 ambao tuligawia vikundi mbalimbali.Alisema nia na madhumuni ya mradi huo ni kumaliza umaskini ambao umekuwa ukiwakumba wakazi wa Sabaki na Kilifi kwa jumla.
“Umaskini umekuwa tatizo kubwa katika eneo hili ila tunaamini kwamba mradi huu utakuwa mojawapo ya suluhu. Ikiwa tunaweza kupata ng’ombe 200 zaidi, basi ninaamini kwamba tutaweza kuendelea mbele na kuimarisha maisha yetu,” akasema Mzee Kahindi.
Katibu wa SCDP Bw Stembo Kaviha alisema kuwa tayari baadhi ya ng’ombe ambao walipatiwa wameanza kuzaa na kutoa maziwa.
“Ng’ombe mmoja ana uwezo wa kutoa lita 15 kwa siku na kwa vile lita moja huuzwa kwa Sh80 mkulima hupata Sh1, 200 kwa siku. Tunatarajia kwamba kadri ambavyo wanaendelea kuzaa, kiwango cha maziwa tunachopata pia kitaongezeka,” akasema.
Aidha alisema kuwa wanatarajia kupata tena ng’ombe wengine 80 hivi karibuni ili kutimiza ndoto na lengo lao kufanikiwa kupitia kwa ufugaji.
Mwakilishi wa wadi ya Sabaki Bw Edward Dele alisema kuwa mradi huo ni wa gharama ya Sh10 milioni ambazo zinatolewa kwa awamu ikiwa lengo kamili hasa ni kumaliza umaskini katika eneo hilo.
“Kilichonisukuma kupendekeza mradi huu wa ufugaji ni faida zake ambazo nilijua zitakuwa za msaada mkubwa sana kwa wakazi. Endapo tutafaulu kuhakikisha kwamba kila boma liko na ngombe wa maziwa, basi tutakuwa katika nafasi nzuri ya kumaliza kero la umaskini,” akasema Bw Dele.