• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
MIRADI PWANI: Minazi mipya inayokomaa baada ya miaka mitatu pekee

MIRADI PWANI: Minazi mipya inayokomaa baada ya miaka mitatu pekee

Na LUDOVICK MBOGHOLI

MAAFISA wa kilimo katika kaunti ndogo ya Taveta wamezindua ugavi wa miche 10,000 ya minazi kwa wakulima wa kata ndogo, wadi ya Mboghoni.

Kwenye uzinduzi huo, mamia ya wakulima walifurahia hatua hiyo huku wakishikilia kuwa serikali inafaa kugawa miche hiyo kwa usawa.

Akizindua mpango huo, afisa mkuu msimamizi wa kilimo katika Kaunti ya Taita Taveta Boniface Mwakio alikumbana na changamoto tele.

“Miche hii ni yenu, imeletwa kwa lengo la kuhakikisha wakulima hapa Mboghoni wananufaika na kuendeleza ukulima wa minazi,”alisema Bw Mwakio.

“Leo tumeleta miche 4,000 ya zao hili inayotosheleza ekari 180 pekee ya shamba, vumilieni maana miche mingine zaidi yaja karibuni,” Boniface Mwakio alidokezea wakulima hao.

Mbali na miche ya minazi, alisema serikali inapanga kuletea wakazi hao wa Mboghoni miche 20,000 ya korosho.

Afisa huyo wa kilimo alifichua kuwa ardhi kubwa ya Taveta ina rutuba ambayo inaweza kukuza na kustawisha vyema mazao ya korosho na minazi.

“Serikali inafahamu ardhi ya Taveta ni bora mno kwa ukulima wa minazi. Minazi mingi inayokuzwa hapa ina ubora wa thamani kuliko minazi inayokuzwa Mombasa na maeneo mengine ya mwambao wa pwani,” alisema msimamizi huyo wa kilimo wa Kaunti ya Taita Taveta.

Naye afisa wa nyanjani wa kilimo katika kaunti ndogo ya Taveta, Bw Ronald Masinde, aliwahimiza wakulima wawe wavumilivu kutokana na changamoto nyingi zinazoshuhudiwa wakati huu wa ugavi wa miche ya minazi.

“Ni lazima tuwe wavumilivu wakati huu wa ugavi wa miche hii inayodumu kwa miaka mitatu tu kabla ya mavuno,” alisema Masinde.

“Nimekuwa nikizuru kwenye mashamba mengi hapa Taveta nikagundua shida iliyopo, tunalopasa kufanya ni kushirikiana pamoja na kuondoa tofauti zetu za kimawazo, ukinzani miongoni mwetu hauwezi kutupa mwelekeo wowote wa ukulima bora,” alizidi kushauri.

Kwenye shughuli hiyo ya ugavi wa miche ya minazi, wakulima walionyesha masikitiko wakidai kuna ubaguzi kwenye shughuli nzima ya ugavi.

“Tunapewa miche kwa kupimiwa, wengine wanapewa idadi kubwa ya miche na wengine wananyimwa kabisa,” waliteta wakulima.

“Hata ugavi wa mbolea na pembejeo pia ni wa ubaguzi, hapa Taveta kuna wakulima wanaoonekana bora zaidi kuliko wengine,” walilalamika.

 

Maafisa wa kilimo nyanjani wapakua miche kutoka hifadhi ya mbegu kwenye afisi kuu ya Taveta, tayari kuwakabidhi wakulima wa Mboghoni. Picha/ Ludovick Mbogholi

Hata hivyo, ilibidi maafisa wa kilimo katika eneo hilo watulize ghadhabu za wakulima, ambao idadi kubwa iliyodai kunyanyasika inatoka katika kata ndogo ya wadi ya Mboghoni.

“Tumesikia yote mliyosema, tumeyanakili na tutayashughulikia, kama kuna afisa anayekiuka kanuni za sekta ya ukulima, atakabiliwa kisheria,” alisema afisa mmoja mkaguzi wa mbegu za mazao na matunda Kaunti ya Taita Taveta.

Baadhi walisikika wakilalamikia orodha ya majina ya wakulima wakidai haiambatani kabisa na mahitaji yao kwani kuna ubaguzi wa kisiri unaotekelezwa na maafisa wakuu wa kilimo.

Taasisi ya utafiti wa Ukulima la KARI katika kaunti ndogo ya Matuga liliagiza takriban miche 6,000 ya minazi kutoka India, inayokua na kuvunwa ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu pekee.

Lengo la shirika hilo lilikuwa kuwapa wakulima wanaokuza zao hilo miche hiyo kwa wingi.

“Miche hiyo ilinuiwa kuwafaidi wakulima 32 wa mwanzo kabla ya kusambazwa kwa wakulima wengine katika maeneo yote ya wakulima wa pwani,” walidokeza maafisa wa KARI, wakiongezea kuwa miche hiyo haikusambazwa kabla ya kufanyiwa utafiti.

Kwenye shughuli hiyo, walitafuta wakulima katika maeneo ya Kwale, Kilifi na Taita Taveta na kuwaorodhesha saba miongoni mwao kunufaika na mpango huo ambao ndio wa kwanza nchini Kenya.

Kabla ya kuzinduliwa harakati za upanzi wake mnamo Februari mwaka huu, wakulima walifunzwa kwanza jinsi ya kuikuza, na kila mmoja aliuziwa mche kwa Sh500 akitakiwa akuze miche 32 kwenye shamba la nusu ekari au ekari moja.

Maafisa wa KARI walibainisha kwamba ukuzaji wa miche hiyo unafanyiwa utafiti ili kubaini changamoto zinazoweza kutokea, na hakuna aliyepatiwa kama shamba lake halina maji ya kutosha.

You can share this post!

AKILIMALI: Kifaa kipya kinachotatua changamoto nyingi za...

BIASHARA MASHINANI: Malengo yake ni kugeuza kijiji kuwa...

adminleo