Mitandao ya kijamii na msongo wa mawazo
BAADA ya utafiti wa kitaifa uliofanywa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Amerika (CDC) kuonyesha ongezeko kubwa la mfadhaiko, kukata tamaa na mawazo ya kujiua miongoni mwa vijana, wasiwasi kuhusu athari za mitandao ya kijamii kwa afya ya akili umeongezeka sana.
Sheria zinazolenga kupunguza upatikanaji wa mitandao ya kijamii kwa vijana zimekuwa gumzo, sambamba na wito wa kupiga marufuku programu maarufu ya TikTok.
Wazazi na watafiti wana hofu kuhusu mchango wa mitandao hiyo kwa matatizo ya ulaji, hali inayochochewa na mfumo wa mitandao unaoeneza maudhui yanayosisitiza mwonekano wa mwili “kamili”, pamoja na athari kwa hali ya kujiamini.
Vilevile, ukatili wa mtandaoni umechangia kuongezeka kwa visa vya mfadhaiko, kwani aibu anayopata mtu anayedhalilishwa inafikia maelfu wa watumiaji wa mitandao.
Hata hivyo, je, ni kweli kwamba mitandao ya kijamii na jamii za mtandaoni ni chanzo cha madhara tu? Tafiti fulani zimeonyesha kuwa kunaweza pia kuwa na faida.
Imebainika kuwa msaada wa kijamii ni nguzo muhimu ya furaha na ustawi wa akili. Mahusiano ya kijamii ni silaha madhubuti dhidi ya msongo wa mawazo, upweke na mfadhaiko.
Kuwa na mtandao wa msaada kunahusishwa na uwezo mkubwa wa kustahimili matatizo na hupunguza uwezekano wa kupata dalili za msongo wa mawazo baada ya tukio la kuumiza. Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia hifadhidata yake, limetoa mapendekezo ya kuimarisha uhusiano wa kijamii kama njia mojawapo ya kupunguza viwango vya vifo vinavyotokana na kujiua.
Utafiti mwingine wa muda mrefu kutoka Chuo Kikuu cha Harvard umefuatilia maisha ya watu kwa zaidi ya miaka 80, ukichunguza vyanzo vya furaha na changamoto zake.
Moja ya matokeo yake makubwa ni kwamba watu wenye uhusiano wa kijamii wa karibu wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha marefu na yenye furaha zaidi.
Mahusiano yanasaidia kupunguza msongo, wakati ukosefu wa mahusiano huzidisha msongo, husababisha uzalishaji wa homoni za msongo kwa kiwango kikubwa na kuleta uvimbe wa kudumu mwilini.
Upweke umeelezewa kama janga la karne ya sasa, na suluhisho lake ni kuwa na watu wa karibu wanaokusaidia kubeba changamoto za kila siku.
Lakini si rahisi kuunda uhusiano huo katika jamii inayozidi kutengana. Wataalamu wa saikolojia huwasaidia wateja wao kuelewa umuhimu wa msaada wa kijamii, na kuwafundisha mbinu za mahusiano ili kuimarisha uhusiano wao na wengine. Ni muhimu kukumbuka kuwa msaada wa kijamii hauishii tu kwa mawasiliano ya ana kwa ana.
Utafiti uliofanywa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ulilenga kuchunguza kama mitandao ya kijamii inaweza kuwa chanzo cha msaada wa kijamii wakati wa msongo. Washiriki walionyesha kuwa walikuwa na uwezekano mkubwa wa kutafuta msaada kupitia mitandao ya kijamii kuliko kwa wazazi au wataalamu wa afya ya akili, wakivutiwa zaidi na jamii za watu wenye mapenzi au changamoto sawa. Hata hivyo, walikiri kuwa mitandao hiyo hiyo pia inaweza kuongeza msongo.
Utafiti wa CDC ulibaini kuwa ingawa mfadhaiko umeongezeka, vijana wengi wanachukulia matumizi ya mitandao kama chombo cha msaada wa kijamii na kinachowasaidia kujihisi karibu na marafiki wao.
Kwa nini watu – vijana na watu wazima – hujiunga na jamii za mtandaoni? Tafiti zinaonesha kuwa watu hujiunga kwa sababu mbalimbali, kuanzia burudani hadi kutafuta mahali pa kupokelewa.