Makala

Mji ambapo utahitaji Sh100 kusindikizwa kwenda nyumbani ukitoka kazini

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA STEPHEN ODUOR

MJI wa Madogo, ambao ni wa pekee katika Kaunti ya Tana River ambapo biashara zimekuwa zikiendelezwa kwa muda wa saa 24, sasa huzima pindi tu jua linapozama.

Saa kumi na mbili jioni, biashara huanza kufungwa na ifikapo saa moja na nusu usiku, mji huwa umeingia gizani, ukiachia nafasi magenge ya wahalifu yanayoendeshwa na vijana kutawala.

Siku 30 zilizopita zimekuwa jinamizi kwa wakazi ambao wanalazimika kuzoea masaibu yanayosababishwa na ukosefu wa umeme ambao haujashughulikiwa.

“Nimelazimika kuwafuta kazi wafanyakazi katika baa yangu kwa sababu hatuwezi kufanya kazi usiku. Kutumia jenereta ni ghali na kukaa peke yako katika biashara usiku pia ni hatari,” alisema Japheth Mutua, mmiliki wa baa.

Baa na hoteli zinazofanya biashara hadi alfajiri huwa zinalazimika kulipa magenge ya wahalifu fedha kwa ajili ya usalama ili wasije wakaibiwa.

Gharama hizo huwa ni hadi Sh1,000 kwa wamiliki wa baa na Sh500 kwa wamiliki wa maduka na hoteli. Hata hivyo, usalama wa mteja nje ya eneo la biashara si hakikisho.

Wakazi wanaotoka kazini usiku wamejizoesha ustadi wa kufahamiana na kujadiliana na wanachama wa magenge ya wahalifu kwa ajili ya usalama wao.

“Mimi huwa natumia Sh100 kila siku ili kusindikizwa nyumbani. Nikitoka kazini lazima niambatane na mmoja wao, bila hivyo mimi ni mlengwa,” alisema Anne Silwa, mfanyakazi wa dukani.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Tana River, Bw Ali Ndiema, alisema kuwa polisi wako macho kuhakikisha kuwa mji huo uko salama.

Anabainisha kuwa, ingawa genge la vijana linaloitwa Kayole Brothers ni tishio, maafisa wa usalama wameweza kupunguza shughuli zao mjini kwa kiwango kikubwa.

“Tunajitahidi kadri ya uwezo wetu na tunawaomba wakazi kutuunga mkono kwa kuripoti matukio ya aina hiyo pamoja na kutusaidia kuwakamata wahusika hawa badala ya kuwavumilia,” alisema.

Zaidi ya hayo, alionya kwamba wazazi wa washukiwa wa genge wataadhibiwa sawa kwa uhalifu uliofanywa na watoto wao ikiwa watakamatwa.

“Kila mzazi anapaswa kujua watoto wake walipo, tukipata taarifa au kumkamata mtoto yeyote anayejihusisha na uhalifu, mzazi naye atashtakiwa kwa kula njama,” alisema.

Tatizo la umeme huko Madogo lilisababishwa na mafuriko kwenye Barabara Kuu ya Madogo-Garissa ambayo yaliangusha nguzo za umeme.

Mbali na uhalifu, giza kutokana na kukatika kwa umeme limefanya maisha kuwa ghali sana, huku watu wachache sana wakiwa na bahati ya kuwa na kawi ya jua ambapo wanatoza huduma za kuchaji simu kwa Sh50.

Maji safi pia yamekuwa haba kwa vile usambazaji hauwezekani bila nguvu za umeme na kuwalazimu wakazi kununua maji kutoka kwa wachuuzi wanaochota kutoka kwa Mto Tana huku kukiwa na tishio la mlipuko wa maradhi ya kipindupindu katika kaunti hiyo.

Kulingana na Meneja wa Kampuni ya usambazaji umeme ya Kenya Power katika kaunti hiyo, Bw Silas Limo, maji kutoka kwa Mto Tana yaliangusha nguzo za umeme kando ya barabara hiyo na kusababisha usambazaji kukatika.

“Tumedhamiria kurejesha umeme katika eneo la Madogo, lakini eneo hilo bado limejaa maji na hivyo inaweza kuchukua muda kurekebisha nguzo zilizoko kwenye maji na kurejesha umeme,” alisema.

Huku hayo yakijiri, amewataka wakazi wa Madogo kuwa na subira huku kampuni hiyo ikipanga mikakati mbadala ya kukabiliana na kukatika kwa umeme.