• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mjue seneta Joe Nyutu anayemponda Gachagua Mlimani

Mjue seneta Joe Nyutu anayemponda Gachagua Mlimani

NA MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Joe Nyutu ambaye kwa sasa amegeuka kuwa jenerali wa kikosi cha kumponda Naibu Rais Rigathi Gachagua bila huruma katika eneo la Mlima Kenya akipendekeza Rais William Ruto amfute kazi kabla ya 2027, ana umri wa miaka 55.

Bw Gachagua naye ana umri wa miaka 59 kwa sasa.

Kwa sasa, seneta Nyutu anasisitiza kwamba Gachagua amegeuka kuwa tishio kwa viongozi wengi Mlima Kenya kupitia kuwadunisha, kuwakanyagia, kuwaaibisha mbele ya Rais na wafuasi wao na pia kuwasemasema vibaya katika mikutano yake ya siri.

Katika msingi huo, Bw Nyutu anasema kwamba ana ufuasi mkuu wa wapigakura nyuma yake na maafikiano kati ya wanasiasa wengi Mlima Kenya ni kumtaka Rais Ruto akiwania awamu ya pili mwaka 2027, amteme Bw Gachagua kama mgombea mwenza wake na badala yake amteue mwanasiasa mwingine, kwa sasa akimpendekeza mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwahutubia wananchi wakati wa uziduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu za serikali mnamo Januari 10, 2024. PICHA | JOSEPH KANYI

Msimamo huo na bidii anayotia katika kuusukuma umemweka Bw Nyutu katika darubini ya siasa kitaifa, watu wakitaka kujua yeye ni nani, ametoka wapi na msukumo wake ni gani na hata anayemfadhili ni nani.

Seneta Nyutu ni wa imani ya Kikatoliki na ambaye katika ndoa yake, ni baba kwa watoto watatu. Wa kwanza ni msichana wakili kitaaluma, mvulana ni mhandisi na kijana mwingine yuko katika shule ya upili.

Bw Nyutu alizaliwa katika eneobunge la Maragua na kwa sasa anahudumu mwaka wake wa pili katika siasa za kuchaguliwa, baada ya kuwania useneta na uspika wa bunge la Kaunti ya Murang’a mwaka wa 2017 lakini akaangukia pua.

Alirithi mikoba ya useneta Murang’a kutoka kwa Gavana Irungu Kang’ata na ametoa hakikisho kwamba “mwaka wa 2027 mimi sina tamaa ya kuwania ugavana”.

“Watu waache kuwa na wasiwasi na kunisemasema eti nazusha ndipo nijijengee umaarufu wa kuwania kiti cha Bw Kang’ata,” akasema Bw Nyutu.

Bw Nyutu anapendwa na wengi katika Kaunti ya Murang’a kwa kujiepusha na mtindo wa kufunika ukweli ulio moyoni mwake ili kufurahisha wengi na pengine waongo.

“Mimi sina jingine ila kunena ukweli tu… Unipende, unichukie au ufanye nini, ukweli utasimama tu na sitakuwa miongoni mwa watakaosulubiwa kwa kuwa walinena uongo kimakusudi,” asema.

Katika hali hiyo, Bw Nyutu amekuwa mwiba kwa utawala wa gavana Kang’ata akimtaka kuwajibikia huduma mbovu katika hospitali za umma zilizoko Kaunti ya Murang’a akidai kwamba “kunao wanaaga dunia katika hali ambazo zingezuiliwa ikiwa ubutu, utepetevu na uzembe kazini, vyote vingezimwa”.

Bw Nyutu pia amejitokeza kama mtetezi sugu wa kipekee wa kile anachodai ni udhalimu mkuu dhidi ya majirani wa Kampuni ya Kimarekani ya kukuza na kuchakata mananasi kutengeneza juisi, Del Monte.

“Hii kampuni ijue kwamba inatumia mashamba ambayo mababu zetu walipigania uhuru ili wayatwae kutoka kwa wabeberu. Walinzi wa kampuni hii wamegeuka kuwa wa kuua vijana wetu, kuendeleza unyanyasaji wa kingono dhidi ya kina mama na pia kutekeleza mashambulio yanayoacha wengi wakiwa vilema. Huo ni ukoloni na hatutaukubali kamwe, liwe liwalo,” akadai.

Aidha, Bw Nyutu anasema kwamba mahakama na pia kamati ya bunge kuhusu ardhi imeamua kuwa baadhi ya maskini wa Murang’a wapewe makao katika shamba hilo linalomilikiwa na Del Monte.

“Ni juu ya kampuni hiyo sasa ijue jinsi ya kutenga kipande cha ardhi na kutii amri hizo za mahakama na bunge. Kunao wanang’ang’ania hilo lisifanyike ndipo waibe vipande vya shamba hilo. Hapo tena tutakwaruzana kwa kuwa sitakubali nikiwa seneta,” akasema.

Akifahamika kwa ucheshi wake katika hotuba, Nyutu ni mwalimu kitaaluma na amewekeza katika sekta ya elimu ambapo ni mumiliki wa taasisi za kunoa bongo za wanafunzi.

Alisomea shule ya upili ya Kijabe kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi kusomea Shahada ya Elimu na akafuzu mwaka wa 1994.

Mwaka wa 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Strathmore kusomea uhasibu na pia akafululiza hadi Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea masuala ya usimamizi wa biashara.

Alisomesha somo la Dini ya Kikiristo na pia lile la Kiswahili katika shule ya upili ya Senior Chief Koinange iliyoko Kaunti ya Kiambu huku pia akihudumu kama dereva wa teksi ili kujipa mihela zaidi.

Kwa sasa, Nyutu ameapa kwamba ataongoza mdahalo katika Kaunti ya Murang’a wa kuvuta wapiga kura wa eneo hilo hadi kumpigia debe Nyoro ateuliwe kuwa Naibu wa Rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2027 na hatimaye awanie urais mwaka wa 2032.

“Nitapendwa na nitachukiwa kwa hali sambamba. Lakini cha maana ni kujua kwamba hili ni taifa la kidemokrasia na kila mtu ana uhuru wa kutumia ubongo wake kufanya maamuzi yake. Kwa sasa nashikilia kwamba Bw Gachagua hafai na Bw Nyoro ndiye kiboko chake cha kumuadhibu akome hizo tabia alizo nazo za kujiona tu ni yeye kwa kuwa yeye ni Naibu Rais,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Mshangao kubainika mshukiwa alijifungulia...

Kenya yapokea mkopo wa Sh150 bilioni kutoka IMF

T L