• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Mkapa anazikwa leo

Mkapa anazikwa leo

Na SAMMY WAWERU

RAIS wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa anazikwa leo Jumatano, Julai 29, 2020, nyumbani kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi eneo la Mtwara, katika hafla itakayoongozwa na Rais wa sasa wa nchi hiyo John Pombe Magufuli.

Jana, Jumanne, Dkt Magufuli aliongoza mamia na maelfu ya waombolezaji katika kumuaga Mzee Mkapa. Jana piailikuwa zamu ya viongozi wakuu Tanzania na Afrika Mashariki kuutazama mwili wa marehemu, ili kumpa heshima za mwisho.

Mzee Mkapa alifariki mwishoni mwa wiki iliyopita, usiku wa kuamkia Ijumaa, Julai 24, 2020, kwa mujibu wa taarifa ya Rais Magufuli.

Akitoa tangazo hilo la tanzia kupitia Shirika la Habari la Kitaifa Tanzania, TBC, Dkt Magufuli alisema Rais huyo mstaafu aliaga dunia katika Hospitali Dar es Salaam wakati akiendelea kupokea matibabu.

“Kwa masikitiko makubwa, tumepata msiba mkubwa. Mzee wetu, Mzee Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu amefariki. Naomba Watanzania walipokee hili, ni msiba mkubwa,” akatangaza Rais Magufuli.

“Tuendelee kuombea Mzee wetu Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki,” Dkt Magufuli alisema kupitia taarifa iliyopeperushwa kupitia runinga ya TBC.

Mnamo Jumapili, familia yake ilisema Rais huyo wa zamani alifariki kutokana na ugonjwa wa Malaria na Shinikizo la Moyo, kinyume na tetesi zilizohoji Mzee Mkapa alifariki kutokana na Covid-19.

Huku mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki yakiungana na Tanzania kumuaga mwendazake, Mzee Mkapa ametajwa kama kiongozi aliyejali maslahi ya Afrika Mashariki kwa jumla.

Marais na viongozi mbalimbali waliotuma salamu za pole kwa jamaa, marafiki na Watanzania, kilichojitokeza bayana ni ukwasi wa moyo wenye amani aliokuwa nao Rais Mkapa.

Akituma salamu za pole, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alimtaja marehemu kama kiongozi aliyejitolea mhanga kuhakikisha amani na utangamano unapatikana na kudumu Afrika Mashariki.

“Ni kiongozi aliyejali Afrika Mashariki na kuhakikisha utangamano, amani na maendeleo yamekuwepo,” taarifa ya Rais Kenyatta kutoka Ikulu ikaeleza.

Kenya inamkumbuka Rais Mkapa, kutokana na jitihada zake kuleta taifa hili pamoja kufuatia ghasia, fujo na machafuko yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007.

Mzee Mkapa alikuwa miongoni mwa baraza la viongozi wa Afrika, lililoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan (ambaye kwa sasa ni marehemu), lililosaidia kupatanisha Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM Raila Odinga, 2008, ambapo serikali ya mseto ilibuniwa, Bw Raila akawa Waziri Mkuu.

Machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya Wakenya 1,300 na maelfu kufurushwa kutoka makao. Uchaguzi huo ulishirikisha Rais Kibaki na Bw Raila, kama wagombeaji wakuu.

“Mzee Benjamin Mkapa hakufikiria maslahi ya Tanzania pekee, ila ya Afrika Mashariki kwa jumla. Wakati wa ghasia za uchaguzi 2007/2008 alizungumza na Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga, mazungumzo yaliyoongozwa na mpatanishi mkuu Kofi Annan. Alichangia pakubwa kuleta pamoja viongozi waliotofautiana. Wakenya tulipomhitaji, alituitika na kuja mara moja,” akasema kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, na ambaye alihudumu kama Makamu wa Rais chini ya serikali ya mseto.

“Alielewa Kenya. Tuna mengi ya kumshukuru. Kama Ukanda wa Afrika Mashariki, tunaomboleza kigogo aliyejitolea mhanga kutushughulikia,” Bw Kalonzo akasema, wakati akitoa rambirambi zake za pole.

Isitoshe, Rais Mkapa alikuwa mpatanishi mkuu wa Burundi 2016, ambapo alisaidia kuleta pamoja serikali ya nchi hiyo na mrengo wa upinzani, kufuatia tofauti za kisiasa zilizodumu kwa muda mrefu.

Miongoni mwa viongozi ambao pia walituma salamu zao za pole ni pamoja na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kati ya wengine.

Kwa heshima na tadhima ya Mzee Mkapa, Tanzania imepeperusha bendera zake nusu mlingoti tangia Ijumaa, alipotangazwa kuaga dunia.

Aidha, Kenya pia imemuomboleza marehemu kwa kupeperusha bendera yake pamoja na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nusu mlingoti kati ya Jumatatu na Jumatano.

Bw Mkapa na ambaye alikuwa amebobea na kuwa sanifu katika lugha ya Kiingereza na pia Kiswahili, alizaliwa mnamo Novemba 12, 1938. Alikuwa Rais wa Tanzania, kati ya 1995 – 2005 na pia mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Mzee Mkapa alirithi uongozi kutoka kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete naye akamrithi Mkapa, ambapo alihudumu kati ya 2005 hadi 2015 ambapo Dkt John Pombe Magufuli alichaguliwa.

Bw Mkapa, akiwa mwandishi wa habari na mwanadiplomasia, ambapo alihudumu katika mashirika kadhaa ya habari Tanzania, alisomea katika Chuo Kikuu cha Makerere na Chuo Kikuu cha Columbia.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 81, ambapo amemuacha mjane Anna Mkapa na wanawe watatu.

Buriani Mzee Benjamin William Mkapa.

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana wanacheza na maisha ya Wakenya

Kikao cha seneti chaahirishwa malumbano yakiwa yamechacha

adminleo