Makala

Mke na mwana wa rais wa zamani wa Gabon watupwa jela miaka 20

Na WINNIE ONYANDO Na MASHIRIKA November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA moja nchini Gabon imewahukumu kifungo cha miaka 20 mke na mwana wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo aliyepinduliwa mwaka wa 2023, Ali Bongo.

Uamuzi huo ulifanywa bila wawili hao Sylvia Bongo, na mtoto wake, Noureddin Bongo Valentin, kuwapo mahakamani mnamo Novemba 11, 2025.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 62 na mwanawe mwenye umri wa miaka 33 wanaishi uhamishoni nchini Uingereza.

Wawili hao wametiwa hatiani kwa kutumia nafasi zao kumpotosha Ali Bongo kufanya ubadhirifu wa fedha za walipa kodi wa taifa hilo.Bongo, mkewe Sylvia Bongo, na mwanawe Noureddin waliondolewa gerezani mnamo Mei mwaka huu na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

Wamekuwa wakizuiliwa tangu Agosti 2023 wakishutumiwa kwa kushiriki uhalifu ikiwemo ufujaji wa mali na ulanguzi wa fedha.

Ali Bongo mwenyewe awali aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani baada ya mapinduzi hayo. Baadaye aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

Sylvia na Noureddin Bongo walihamishwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mnamo Mei.Walikuwa wakizuiliwa kwenye seli za chini katika ikulu ya rais.

Mnamo Aprili 30, Baraza la Usalama na Amani katika Umoja wa Afrika (AU) lilirejesha Gabon kwenye umoja huo. Gabon iliondolewa kwenye AU kutokana na mapinduzi yaliyomwondoa Ali Bongo madarakani.

Kupitia taarifa wakati huo, AU ilitoa wito kuachiliwa kwa familia ya Ali Bongo na hakikisho kuwa haki zao pamoja na afya yao italindwa.

Kabla ya kuondolewa na rais wa sasa kupitia mapinduzi ya jeshi mnamo 2023, AIi Bongo alikuwa ameongoza Gabon tangu mwaka wa 2009.