Mkenya anayevumisha kilimo Amerika
AKIWA mzaliwa wa Kijiji cha Itivo, Kesabakwa, Kaunti ya Kisii, ndoto ya Kevin Ntabo akikua ilikuwa kusafiri Amerika na ikiwezekana awe mwenyeji.
Azma yake ilichochewa na msukumo wa kupata ajira yenye malipo ya kuridhisha.
Hali kadhalika, alitamani mazingira mapya kujiendeleza kimaisha.
Kati ya 2016 na 2017, Ntabo alisafiri Amerika na Uingereza kusaka kazi.
Hatimaye, 2021 aliangukia bahati akahamia Amerika akiwa amejihami na Digrii ya Masuala ya Uhasibu.
Ntabo, 35, anasimulia kwamba alijaribu kujiunga na kikosi cha jeshi cha nchi hiyo yenye ushawishi mkubwa duniani ila hakufaulu.
“Sikufanikiwa kwa sababu ya uzito wangu uliopita uzani unaohitajika,” anasema.
Anasema alikuwa na uzani wa zaidi ya kilo 100.
Babake ana zaidi ya mke mmoja, na anasema familia yake ina historia ya maradhi yanayohusishwa na afya.
Mamake alifariki majuzi, Agosti 204 kutokana na ugonjwa wa Kisukari.
Maradhi hayo yanahusishwa na uzani kupita kiasi.
“Kwa sababu ya changamoto hizo, nilifunguka mawazo,” asema.
Ntabo anaamini kukabiliana na maradhi ya afya na uzani kupita kiasi, suluhu ni anachokula binadamu.
Jawabu si kuwa mateka wa vituo vya kupunguza uzito au kuunga misuli maarufu kama jimu.
Kugonga ndipo, safari kupunguza uzito na kula chakula chenye virutubisho faafu ilianza 2022 alipoingilia shughuli za kilimo.
Akiwa mkazi wa King County, Washington, Ntabo ni mkulima hodari wa vyakula asilia.
Aidha, hukuza mboga za kienyeji zenye asili ya Kiafrika, zikiwemo mnavu, maarufu kama managu au sucha, mchicha (terere), kunde, mrenda na saga.
Isitoshe, pia hukuza sukuma wiki, spinachi, maboga (almaarufu malenge), maharagwe ya Kikenya, mseto wa viazi, minji, okra, karoti na mahindi.
Anafichua kwamba hulima kwenye ekari 100.
“Ni shamba asilia linalopewa makundi ya matabaka yasiyo na idadi kubwa ya watu, waendeleze kilimo bila kuliharibu,” akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano Jijini Nairobi.
Alipata ufadhili wa shamba hilo kupitia shirika la Living Well Can, lenye maono na malengo ya ulaji wa chakula chenye virutubisho bora na faafu.
Akiwa pamoja na wakulima wengine 50, Ntabo ni kati ya makundi yaliyopewa kima cha Dola 100,000 za Amerika (sawa na Sh12 milioni thamani ya Kenya), wagawane kuendeleza uzalishaji chakula.
Hali kadhalika, walipewa bima ya mimea.
Mavuno ya kwanza, hata hivyo, anasema hakupata wanunuzi vile kwa sababu alikuwa mgeni Amerika na aliishia kuyaweka kama akiba.
“Kwa muda wa mwaka mmoja, gharama ya chakula niliiweka pembeni,” anadokeza.
Anasema, ndio Amerika kuna hela ila gharama za bili ndizo kibao.
Alivyoendelea kunogesha kilimo ughaibuni, anasema alijuana na Wakenya wanaoishi Amerika ambao sasa ni miongoni mwa wateja wake wakuu.
Shirika la Living Well Can lina soko Washington, sawa na masoko ya Muthurwa na Gikomba ambapo wakulima hupeleka mazao yao.
Kilimo ambacho Ntabo anaendeleza ni cha ziada, na anasema asubuhi anapotoka kazini huenda shambani ‘kusalimu’ mimea na kila anapoitazama humfanya atabasamu.
Miaka miwili baadaye, Ntabo anakiri hajutii maamuzi yake kujitosa kwenye mtandao wa uzalishaji chakula.
Cha kutia moyo zaidi, mazao yake ambayo ndiyo chakula chake na familia yake, anasema yamemsaidia kupunguza uzani, sasa akichezea kati ya kilo 71 hadi 73.