• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Mkenya Cheruiyot Kirui alielewa kibarua cha kuukwea Mlima Everest

Mkenya Cheruiyot Kirui alielewa kibarua cha kuukwea Mlima Everest

NA BERNARD ROTICH

WAKATI mkweaji milima, Mkenya Cheruiyot Kirui, alipoanza kupanda Mlima Everest mnamo Aprili 2024 bila mitungi ya oksijeni, shabaha yake ilikuwa kufika hadi kilele cha juu cha mlima huo.

Alifahamu hatari iliyokuwa ikimkodolea macho, ikiwa ni pamoja na barafu kuharibu ngozi yake na tishu za mwili, pamoja na maradhi yanayoambatana na mtu kuwa katika nyanda za juu zaidi.

Akiwa ni mfanyakazi wa benki, Kirui alionyesha uchangamfu alipoanza safari yake ya kufikia kilele cha mlima mrefu zaidi duniani, kulingana na jinsi alivyokuwa akiweka machapisho katika kurasa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Alijiamini angefanikiwa, lakini hilo halikuwezekana.

Kirui alisomea katika Shule ya Upili ya Chebisaas.

Mkweaji huyo aliaga dunia alipokuwa katika hatua za mwisho mwisho kufika hadi kileleni. Mwili wake uligunduliwa mita chache tu chini ya eneo la kilele, siku moja tu baada ya taarifa kuibuka kwamba yeye pamoja na mwelekezi wake walikuwa wametoweka.

Katika safari yake ya ujasiri wa hali ya juu, Kirui alikuwa na mpango kabambe ambapo alikuwa akiwafahamisha mashabiki wake kila hatua, habari hizi akizichapisha katika majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Katika ukurasa wake wa Instagram, aliandika kwamba baada ya siku 10 kwenye safu ya chini ya kuanzia, mpango wake wa kufikia kilele cha mlima huo ulioko kwenye eneo la Mahalangur Himal katika kilele cha mita 8,848.86 ingekuwa jaribio la kukwea bila mitungi ya oksijeni.

Jaribio la aina hiyo bila mitungi ya oksijeni huhitaji maandalizi spesheli kwa sababu huwa na hatari zake. Hilo alikuwa amebaini alipoanza safari yake mnamo Aprili. Alihisi alikuwa sawa kiafya na kwamba mwili wake ulikuwa tayari.

Alijifahamisha na namna ya kukabiliana na changamoto katika safari hiyo ya zaidi ya mwezi mmoja, akijiua jinsi ya kukabiliana na baridi, dawa alizohitaji, pamoja na oksijeni ya dharura endapo ingehitajika.

Alifanya masasisho ya safari yake kwenye Instagram na Facebook.

Lakini kurasa zake za mitandao ya kijamii zimekuwa zimetulia kwa siku tano zilizopita.

Alijua kule kuna baridi kali na alikuwa akiwaambia mashabiki kuhusu hilo.

Aliwafahamisha mashabiki kwamba bila oksijeni, mkweaji alikuwa akijiweka kwa hatari ya kupata matatizo kutokana na baridi kali. Ili kukabiliana na hatari hiyo ya kiafya, alikuwa na glavu jozi za joto, na soksi za mkononi za kuupa mwili joto, zote zikitumia betri. Pia alibeba betri za ziada.

Alikuwa amebeba dawa ya Nifedipine, na alifichua katika mpango wake kwamba ni kwa sababu alikuwa katika hatari ya kupata maradhi ya mapafu kwa kuwa katika safu ya juu zaidi duniani, hali inayofahamika kama HAPE na inayofanya mapafu kujaa maji hali inayoweza kuhitaji tiba ya dharura.

HAPE ni rahisi kumwandama mtu aliyezoea nyanda za kawaida lakini akapanda upesi hadi mwinuko wa kati ya mita 2500-3000.

Hatari nyingine aliyokabiliwa nayo ni ubongo kuathirika (HACE) kwa kupata uvimbe. Akiwa amewahi kutatizwa na hali hii awali, alisema alikuwa amebeba dawa za deksamethasone na acetazolamide.

HACE ikizidi hufanya maungo kukosa uthabiti, mwili kunyong’onyea kwa uchovu na kumfanya mweaji kutojielewa akiwa katika nyanda za juu. (AMS).

Kwa oksijeni ya dharura, Nawang Sherpa, ambaye sasa naye haijulikani aliko, ndiye alikuwa akimpa Kirui chupa ya oksijeni ya dharura wakati alihitaji.

“Ninafahamu hata ninaweza kulemewa, nikawa ninasawijika au nikalemewa kukamilisha kwa wakati unaofaa, au hali ya hewa ikawa si shwari, na hata mwili kufika ukomo wake na hapo ndipo ninagundua mimi si Superman. Pia kunaweza kukawa na msongamano. Ndiposa niliamua kuanza kuukwea mlima kutoka upande wa Tibet/Kaskazini ili kuepuka msongamano, lakini sisi ndio hawa, natumai, tutaepuka msongamano huo, ” aliandika kwenye ukurasa wake.

Kuhusu hitaji la kifedha, alisema akitania “nikitoka huku na kurudi nchini Kenya nitakuwa nimesota sana kwa sababu hii ni safari ghali mno. Kama kawaida tunajumuika hapa kwa siku kadhaa kuona kutaendaje.”

Alikuwa amemuahidi mwandishi huyu kwamba angesimulia kila hatua aliyokuwa akiichukua wakati akijaribu kufika kileleni, ikiwa ni pamoja na kupiga picha.

“Ninafika kwenye kambi ya kuanzia leo hii tunapozungumza na hakika nitapiga picha ingawa sio za kitaalamu ili tukio hili tulinakili nitakapofika kileleni,” Kirui alikuwa amemuahidi huyu mwandishi.

Kirui na mwelekezi wake Nawang Sherpa waliripotiwa kutoweka baada ya kupoteza mawasiliano katika eneo la Bishop Rock.

Waokoaji kutoka Seven Summit Treks waligundua mwili wake mita chache chini ya eneo la kilele la Mlima Everest.

Kulingana na jarida la Himalayan, ni kwamba Nawang aliwasiliana mara ya mwisho na maafisa wa chini ya kambi hiyo kutoka eneo la Bishop Rock kwamba Kirui alikataa kurudi na hata kutumia oksijeni ya chupa, huku akionyesha tabia isiyo ya kawaida.

Kulingana na rafiki yake ambaye walisoma pamoja shuleni Chebisaas, Bw Shadrack Mwirotsi, kila mara Kirui alipendelea kufanya mazoezi ya kupitiliza ambayo kwa kawaida huwa zaidi ya kilomita 42 za kawaida.

Mwanafunzi huyo mwenzake wa zamani alifichua kwamba Kirui hakupenda marathon za kawaida au nusu marathon, akifichua kwamba alipenda msisimko wa matukio ya ujasiri zaidi.

“Nakumbuka tulikutana naye Kericho ultra-challenge ambapo alitaka tukimbie masafa ya kilomita 50. Nilikuwa mpya kwa hili kwa hivyo nilikimbia kilomita 30 na yeye alifanikiwa kukamilisha kilomita 50. Alipenda kuburudika na pombe aina ya whitecap akiwa anatulia baada ya shughuli zake. Alikuwa mtu mzuri. Ninaamini alikuwa na ujasiri wa kuukwea huo mlima na alifahamu changamoto zote,” akasema Bw Mwirotsi.

  • Tags

You can share this post!

Maangamizi ya halaiki yananukia Sudan, UN yaonya

Ugavi wa mapato hauwezi kutegemea idadi ya watu, CRA...

T L