Mkojo wa sungura wapanda bei na kufikia Sh1,000 kwa lita kichinjio kikilia upungufu wa wanyama hao
MAHITAJI ya mkojo wa Sungura yameongezeka lita moja ikiuzwa kwa Sh1,000 sungura pia yakiongezeka kwa kiwango kikubwa.
Wafanyabishara wanasema kando na kufuga na kuuza wanyama hao kupata nyama, wakulima pia wanapata pesa kutokana na mkojo wa sungura, ambao hutumiwa kama mbolea ya asili na dawa ya kuua wadudu wanaoshambulia mimea.
Nusu lita ya mkojo wa sungura huuzwa kwa zaidi ya Sh500, na kuifanya kuwa nambna ya kujipatia mapato kwa wafugaji wa sungura.
Nyama ya sungura huuzwa kwa kati ya Sh1,000 na Sh2,000 nchini.
Na licha ya ufugaji wa sungura kuwa na mapato mazuri, wajasiriamali wanaoendesha vichinjio vya sungura wameibua wasiwasi kuhusu uhaba mkubwa wa wanyama hao nchini na kuwafanya kushindwa kukidhi mahitaji ya nyama hiyo kwa wateja.
Chama cha Wafugaji wa Sungura nchini (RABAK), kinachomiliki kampuni inayochinja na kuuza nyama ya sungura, kinasema kinatatizika kutafuta sungura wa kuchinja.
Mwenyekiti wa RAABAK, Peter Waiganjo, alisema kichinjio chake hufanya kazi mara moja pekee kwa wiki kutokana na uhaba wa wanyama hao.
Alisema kutokana na uhaba huo, huwa wanachinja sungura 200 pekee kila Jumatano, ikiwa ni sehemu ya mahitaji ya nyama ambayo husambazwa kwa maduka makubwa na hoteli zilizochaguliwa pekee.
“Mahitaji ya nyama ya sungura yameongezeka kwa miaka mingi hadi kiwango ambacho wafanyabiashara hawawezi kukidhi,” alisema Waiganjo.
Wakulima wametakiwa kukumbatia ufugaji wa Sungura ili kunufaika na mapato kwa kuuza nyama na mkojo wake ambazo mahitaji yake yako juu nchini.
Wajasiriamali katika sekta hizo wamezitaka serikali za kaunti kusambaza sungura bila malipo kwa wakulima wanaovutiwa kama motisha ya kuimarisha uzalishaji.
Kulingana na RAABAK, nyama ya sungura imepata umaarufu na kuna faida kubwa katika ufugaji wa sungura, kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo kunaweza kuunda nafasi za kazi na kuimarisha uchumi wa kilimo – biashara nchini Kenya.