Mkulima wa avokado anavyokabili wadudu kupitia mtego wa sola
KINYUA Nkanata amekuwa kwenye uzalishaji wa avokado kwa zaidi ya miaka 16, akiwa aliingilia kilimo chake kama njia ya kujipa pato la ziada.
Hata ingawa tayari ameshastaafu, alikuwa akihudumu katika mashirika mbalimbali kitengo cha mauzo, ikiwemo shirika moja la habari nchini.
Avokado, pia maparachichi, anaendeleza kilimo chake eneo la Meru.
Matunda hayo yameanza kupata umaarufu mkubwa Meru, na yanaepelekana sako kwa bako na chai—zao linalokuzwa kwa wingi katika kaunti hiyo.

Nkanata hulima maparachichi kwa ajili ya soko la nje ya nchi.
Hata hivyo, kwa miaka mitatu hadi minne iliyopita, uzalishaji wake umekumbwa na changamoto si haba kutokana na mdudu anayefahamika kama False Codling Moth (FCM).
FCM ni mdudu hatari sana anayeshambulia matunda kama vile avokado, na hushinikiza wakulima kutumia dawa zenye kemikali kuua wadudu, ambazo pia huhatarisha afya ya binadamu.

Kenya ikiwa mzalishaji mkuu wa maparachichi Barani Afrika na kuorodheshwa sita bora duniani, uwepo wa FCM unatishia nafasi yake ya kipekee katika soko la kimataifa.
Soko la Ulaya, linaloongoza kwa uagizaji wa avokado kutoka Kenya, lina masharti makali kuhusu viwango vya mabaki ya dawa kwenye mazao. Nkanata anaeleza kuwa FCM ilianza kushambulia shamba lake 2022, na kusababisha hasara na upotevu mkubwa wa mazao.
Awali, mazao yaliyoishia kukataliwa sokoni yalikuwa yakichezea kilo 200 hadi 500 kwa msimu.
Lakini kuanzia 2022, kiwango hicho kiliongezeka hadi tani 2.2 (sawa na kilo 2,200).

“Maparachichi ya kuuza nje huuzwa kwa kati ya Sh100 hadi Sh140 kwa kilo, lakini yakishambuliwa, bei hushuka hadi Sh30 kwa kilo katika soko la ndani,” anasema mkulima huyo.
FCM ni mdudu ambaye ni karantini; akigunduliwa kwenye kontena, bidhaa hiyo hurudishwa nchi ilikotoka.
Katika harakati za kukabiliana na changamoto hiyo, barobaro mbunifu amebuni mtego unaotegemea nguvu za kawi, yaani miale ya jua unaosaidia kudhibiti FCM.
“Kutumia mitego ya wadudu ya sola ni njia ya kiasili kudhibiti wadudu,” anasema Nkanata, ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa wakulima wa maparachichi Abogeta West, Meru.

Mbunifu huyo ni Mutuma Muriuki, ambaye ni mwanzilishi wa Eco Bristo Ltd, kampuni inayounda na kusambaza mitego maalum hasa kukabiliana na mdudu hatari aina ya FCM. “Sikutaka tu kutengeneza teknolojia maarufu, nilitaka sana kuangazia mahangaiko ya wakulima kutokana na wadudu ili chakula kinachotufikia kiwe salama—ambacho hakijakuzwa kwa kutumia dawa zenye kemikali,” Mutuma akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.
Akiwa na taaluma ya kilimohai (Agroecology), Mutuma ametumia tajriba yake kutoa huduma za kilimo Bara Afrika, India, Colombia na Mexico kusaidia wakulima wa mashamba madogo. Mwaka 2021, kwa kutumia Sh150, 000, akiba, alianza kutengeneza mitego hiyo akiwa Meru.
Mtego wa sola unavyofanya kazi
Teknolojia hiyo hutumia mwanga wa buluu wa LED kuvutia wadudu. Baada ya kuvutiwa, wadudu huanguka kwenye chombo chenye maji na sabuni au huangamizwa kwa umeme—kulingana na aina ya mtego.

Miundo ya mitego hiyo ni Kifaru—ya mashamba madogo, Ndovu, mashamba makubwa, na Chui iliyotengenezwa kuhudumu kwenye ekari moja.
Bei, inalingana na saizi na muundo.
Eco Bristo pia hutengeneza bidhaa ya kuongeza rutuba kwenye udongo kwa kutumia biochar—makaa ya Kaboni.
Licha ya changamoto za kifedha kuboresha ubunifu wake, 2023 Mutuma alipata granti ya Sh1 milioni kutoka kwa Shirika lisilo la Kiserikali la Heifer International, ambalo lina mpango maalum kusaidia wakulima.

Aidha, granti hiyo ambayo pia ni tuzo hutolewa kupitia shindano la AYuTe linalolenga vijana wanaoshiriki mtandao wa kilimo na uzalishaji chakula, wenye bunifu kuangazia changamoto zinazozingira wakulima.
Lengo la Mutuma ni moja tu; kuhakikisha Kenya na Bara Afrika inazalisha chakula salama, bila dawa.