Makala

Mnajiharibia kwa kulega lega, upinzani waambiwa

Na PIUS MAUNDU,BENSON MATHEKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Viongozi wa upinzani wamesema kuwa wako katika hatua za mwisho za kumteua mgombea wao wa urais kwa uchaguzi mkuu wa 2027, huku wakikosolewa vikali kwa kuchelewa kuamua atakayepeperusha bendera dhidi ya Rais William Ruto.

Huku wakikosoa vikali utendakazi wa Rais William Ruto, hasa katika sekta ya elimu ya juu, uchumi na haki za binadamu, wahadhiri wa vyuo vikuu waliwalaumu kwa kujivuta kutangaza mgombea urais wa upinzani.

Katika mkutano uliofanyika nyumbani kwa kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka katika Kaunti ya Machakos, viongozi hao walivutia wasomi na viongozi wa wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, wakilenga kuwajumuisha katika kampeni dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Kalonzo Musyoka, Dkt Fred Matiang’i, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Dkt Mukhisa Kituyi, Omigo Magara, na Ben Momanyi walihutubia wahadhiri kutoka vyuo 23 pamoja na viongozi wa wanafunzi kutoka taasisi 30 za elimu ya juu.

Baadhi ya wahadhiri waliotoa maoni yao kwenye mkutano huo walikubaliana na msimamo wa upinzani kuwa nchi inazidi kupotea mwelekeo chini ya uongozi wa Rais Ruto. Waliahidi kuunga mkono kampeni ya kumng’oa mamlakani Rais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Profesa Nduku Mutuku, mtaalamu wa Hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, alijitolea kutumia ujuzi wake wa kitaaluma kusaidia upinzani kubuni mikakati ya kampeni zinazotegemea data.

Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media aliwahimiza wahadhiri kuhamasisha wanafunzi walioko chini yao kuwaunga mkono viongozi wa upinzani, pamoja na kuwahimiza vijana kujisajili kuwa wapiga kura.

“Tupo hapa kwa sababu viatu tunavyovaa kama taifa vinatuumiza. Kama mtaalamu wa Hisabati, najitolea kuongoza timu ya kubuni mkakati wa kampeni unaoongozwa na takwimu,” alisema Prof Mutuku.

Hata hivyo, baadhi ya wahadhiri waliotoa kauli zao walieleza wasiwasi wao.

David Osebe, mhadhiri wa jiografia ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, aliwahimiza viongozi wa upinzani kujifunza mbinu fulani za kampeni kutoka kwa Rais Ruto.

“Kati yenu yeyote anaweza kuwa rais wa sita wa Kenya. Lakini mnapaswa kujiboresha zaidi kwenye masuala ya kujitangaza. Rais wa sasa alikuwa akitembelea kijiji kimoja mara tano hadi sita. Katika uuzaji bidhaa, mtu anapaswa kurudia sehemu mara tano hadi nane kabla ya kukubalika. Bw Musyoka, umekuwa ukitumia muda mwingi Ukambani. Watu wa huko wanakujua na wamekukubali. Hali ni sawa kwa Dkt Matiang’i. Sasa mnapaswa kupanua wigo wenu. Nyumbani mnalindwa, lakini nje hamjulikani vya kutosha,” alisema.

John Esikumo Auna, mhadhiri wa fasihi katika vyuo vya GRETSA na Murang’a, alisema muungano wa upinzani unachelewesha ushindi dhidi ya Rais Ruto kwa kuchukua muda kumtangaza mgombea wao wa urais.

“Tunaweza kupiga kelele ‘wantam’ mara elfu moja, lakini kama hatutawasilisha mgombea mmoja wa urais, basi ni kazi bure,” alionya.

Dkt Matiang’i aliwataka wasomi kutumia maarifa yao kusaidia kubadilisha uongozi wa taifa.

“Kuna wazalendo waliopoteza maisha yao wakipigania taifa hili. Kazi tunayopaswa kufanya sasa ni ndogo sana. Serikali ya sasa imefeli waziwazi. Ni jukumu letu kuhakikisha wanaondoka mamlakani,” alisema.

Viongozi hao wa upinzani walidai kuwa serikali ya Rais Ruto imeporomoshwa na sakata ya Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA), ukandamizaji wa haki za binadamu, na kushindwa kusimamia uchumi ipasavyo.

Viongozi hao walisema kuwa harakati za kuunda muungano imara zinaendelea kwa kasi, na uteuzi wa mgombea urais wa upinzani upo karibu kukamilika.

“Tumeamua kuwa na kikosi cha pamoja. Hatugawanyiki. Wanaotarajia tutatengana watashangaa. Tutaendelea kushikamana licha ya porojo zinazoenezwa,” alisema Dkt Matiang’i.

“Bw Musyoka, kweli tunahitaji kufanya kampeni? Kuna jambo lolote ambalo tunapaswa kuwaambia wananchi?” Dkt Matiang’i aliuliza akimaanisha kuwa wananchi wako tayari kuondoa serikali ya Kenya Kwanza katika uchaguzi ujao kwa kuwafeli. Mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Kitui Central Makali Mulu na mwenzake wa Bomachoge Borabu Obadiah Barongo.

“Mkituona tukila pamoja, jua kwamba tunajenga timu imara. Tumekubaliana lazima tuwe na kikosi cha pamoja,” alisema Bw Musyoka alipowasilisha salamu kutoka kwa Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na kiongozi wa chama cha People Liberation Party Martha Karua

Haya yanajiri wakati ambapo kuna shinikizo kutoka kwa wadau mbalimbali wa kisiasa kutaka upinzani uweke wazi mpango wao wa kugawana mamlaka.