Mnogeshaji video za burudani ya muziki ambaye anafanya kazi na wasanii maarufu
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
NI kutokana na uamuzi wake wa kuhama alipokuwa akiishi hadi kwengine ndiko kulomfanikisha na kuwa na matumaini ya kuinua kipaji alichonacho.
Kwa Purity Minage almaarufu Kapoor Vixen kukumbwa na matatizo kumemwezesha achukue uamuzi wa kibafte yaani kutekeleza majaribio ya pata potea.
Kapoor Vixen alipoona hali ya maisha yake na wazazi wake yamekuwa magumu, aliondoka Mombasa na kwenda kuishi Nairobi kutafuta njia zitakazomfanya aweze kujikimu kimaisha na kuwasaidia wazazi wake.
Alipofikia umri wa miaka 17, Kapoor Vixen alianza kujiunga na wasanii kadhaa akiwa mnenguaji kwenye nyimbo za wasanii hao, wengine wakiwa maarufu na wenye majina makubwa nchini.
“Uamuzi wangu haukuwa mbaya na namshukuru Mungu kwani tangu niishi Nairobi, nimefanikiwa kwa lengo langu la kujikimu katika maisha yangu na pia nimeweza kuwasaidia wazazi wangu kwa uwezo nilonao,” amesema msanii huyo.
Kati ya mafanikio yake makubwa aliyopata akiwa mnenguaji ni kwa nyimbo zilizoimbwa na Winny na Masauti ya Umenishika, Bad gal ya Magix Enga na System ya Gin Idel na Dufla Dligon.
Pia amekuwa kwenye video za Mr Ohanga katika wimbo wake wa Owod baba na nyimbo ya Brax iliyoimbwa na Stay na Kenracy na nyenginezo kadhaa.
“Ninafurahikia ninapokuwa najihusisha kwenye nyimbo za wasanii mbalimbali na sichagui kwani natambua hata chipukizi wanahitaji nao wapate wanenguaji wenye kutamba,” akasema Kapoor Vixen.
Msaanii huyo alikumbana na changamoto kadhaa akiwa mnenguaji. Amekuwa mara nyingine akirudi nyumbani bila ya kulipwa na mavazi ni ghali na yanahitajika kila video na mavazi mengine.
“Mbali na gharama kubwa zinazokukabili, unahitajika uwe na vipodozi vyako mwenyewe ili ukijitayarisha kwa kucheza nyimbo yoyote, uweze kujipamba kwa njia ya kupendeza,” akasema.
Mbali na kuwa mnenguaji kwenye nyimbo za wasanii kadhaa, Kapoor Vixen pia ni mpambaji mashuhuri akiwa anapamba maharusi na wanawake wengine wanaokwenda kuhudhuria sherehe na tafrija mbalimbali.
“Nashukuru kuwa niko mpambaji ninayetajika kati ya wale walio bora na nimekuwa nawahudumia maharusi wa watu mashuhuri hapa jijini Nairobi na sehemu nyingine ninazoalikwa kwenda kuwapamba maharusi,” akasema.
Katika fani ya uigizaji, Kapoor Vixen ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 21 amewahi kuwa katika filamu mbalimbali zikiwemo zile za ‘Kina water’, ‘The cut’, ‘Ma-slayqueen’, ‘Stella’ kati ya nyingine kadhaa.
Msanii huyo anapanga kwenda safari hadi Tanzania ambako ana mipango ya kuonana na waigizaji ambao ana imani watamsaidia kuinua kipaji chake.
“Natambua na naendelea vizuri, lakini nataka kipaji changu kifikie kuwa cha kimataifa,” akasema.
Mbali na kwenda huko nchini Tanzania kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi wa fani ya uigizaji, anafikiria kuvuka milima, bahari, mabonde na anga afike huko ng’ambo kushuhudia wanamitindo na waimbaji wa huko barani Ulaya na Marekani.
“Nina hamu kubwa kuinua vipaji vyangu kuwa vya kimataifa kwani ninaamini ninaweza kuwa kama hao wanaotamba huko ng’ambo. Ninafanya bidii nifanikiwe hapa Afrika Mashariki halafu niweze kupigania kuwa msanii mtambulika kote barani Afrika,” akasema.
Anawaambia wanenguaji na wasanii chipukizi wasife moyo wakiona hawajafanikiwa bali wafanye bidii zaidi na watafanikiwa.
“Nilianza kupata shida hadi nikahama Mombasa kuelekea Nairobi na naanza kuona matunda.
“Kwa mtu yoyote kutaka afanikiwe kwa jambo lake, ni lazima afanye bidii na kama halitakuwa haraka, asubiri na kufanya bidii zaidi mwishowe atafanikiwa,” akasema Kapoor Vixen huku akiwashauri wasanii wasichana wapambane kwani anaamini wataweza kutambulika kote duniani.
Kwake mpambaji, mnenguaji, mwigizaji na mwana mitindo huyo anasema kuwa hakuna lisiloweza kufanyika, ni mtu na bidii yake na kutokata tama.