Makala

Moi alivyodumisha Uafrika

February 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

KATIKA utawala wake, Rais Mstaafu Daniel Moi alithamini sana kauli zilizomjenga Mtu Mweusi na utamaduni wa Mwafrika.

Hivyo, alikabili vikali jambo lolote lililoonekana kukinzana na maadili ya Kiafrika, huku akitilia maanani masuala yaliyokuza tamaduni hizo.

Alifikia hayo kupitia nyimbo, vyombo vya habari, vipindi, mavazi, lugha, densi kati ya masuala mengine.

Vile vile, alitoa kauli mbalimbali kila wakati akihimiza umuhimu wa umoja miongoni mwa Wakenya.

Ni katika enzi ya utawala wake ambapo nyimbo kama ‘Fimbo ya Nyayo’, ‘Tawala Kenya Tawala’, ‘Tushangilie Kenya’, ‘Fuata Nyayo’, ‘Maziwa ya Nyayo’, ‘Enzi Zao’ kati ya zingine ambapo zilipata umaarufu mkubwa kwa kuhimiza uzalendo miongoni mwa Wakenya.

Mzee Moi angetumbuizwa na kwaya mbalimbali katika hafla muhimu kama sikukuu za kitaifa, ambapo baadaye angetumia nafasi hiyo kusisitiza jumbe zilizotolewa kwenye nyimbo hizo.

“Mimi mara kwa mara huwa nahimiza umuhimu wa umoja wa Waafrika. Na niliwaambia wananchi tusimame kwa kupendana, tusimame kwa kukaa na amani,” angesema Moi.

Mwalimu Thomas Wesonga, ambaye ameshiriki kwenye utunzi wa baadhi ya nyimbo alizopenda Mzee Moi, anasema kuwa kando na kumwongoa, nyimbo hizo zilikuwa nguzo kuu ya kuhimiza utamaduni wa Mkenya.

Mzee Moi pia hakusita kuwachukulia hatua wanamuziki ambao walitunga nyimbo zilizoukosoa utawala wake, kwani aliziona kama kikwazo cha kusambaratishwa mwito wa Uafrika.

Baadhi ya nyimbo zilizopigwa marufuku ni ‘Nchi ya Kitu Kidogo’ uliotungwa na mwanamuziki Eric Wainaina kwa kukashifu ufisadi katika serikali ya Mzee Moi.

Wimbo huo ulipigwa marufuku mnamo 1998, huku Bw Wainaina akitolewa jukwaani alipokuwa akiwatumbuiza wageni katika hafla moja.

Baada ya jaribio la mapinduzi ya 1982, serikali ya Mzee Moi ilipiga marufuku kwa muda muziki aina ya ‘Reggae’ kuchezwa vilabuni, kwa hofu kwamba “ulikuwa ukiwachochea wananchi.”

Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wamebobea na kupata umaarufu nchini wakati huo ni Bob Marley kutoka Jamaica, Peter Tosh kati ya wengine.

Serikali ya Mzee Moi pia ilitumia vyombo vya habari kushinikiza umoja na thamani kuu ya Uafrika.

Ilifikia hilo kwa kutumia Shirika la Habari la Kenya (VOK) kupitia nyimbo na vipindi vilivyohimiza maadili hayo.

Baadhi ya nyimbo ambazo zilichezwa sana, hasa katika miaka ya themanini ni ‘Amka Kumekucha’ wa Maroon Comandos, ambao uliwahimiza Wakenya kuhusu umuhimu wa kutia bidii kazini ili kuijenga nchi.

Inaelezwa ni kutokana na hilo ambapo Moi aliwakabili vikali wale walioanzisha majarida yenye misimamo huru kama ‘Beyond’, ‘Weekly Review’ kati ya mengine ambayo yaliikosoa serikali yake.

Ingawa Kenya iliegemea mfumo wa chama kimoja katika enzi ya Mzee Moi, wanachama wa Kanu walikuwa na mavazi maalum.

Mavazi hayo yalikuwa yenye rangi nyekundu, kijani kibichi na nyeusi, ambazo ndizo rangi za bendera ya taifa.

Wale waliohudumu wanasema kuwa lengo kuu la mavazi hayo lilikuwa kuonyesha moyo wa uzalendo miongoni mwa Wakenya.

“Mzee Moi alipenda umoja miongoni mwa Wakenya. Aliamini umoja kama nguzo kuu ya Uafrika, ndipo akakita hilo kwenye falsafa ya Kanu,” asema Dkt Amukoa Anangwe, aliyehudumu kama waziri katika serikali ya Mzee Moi.

Wadadisi wanasema kuwa imani hiyo ndiyo ilimweka wasiwasi kukubali Kenya kuanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Kwenye mojawapo ya hotuba yake, Moi alieleza kuwa mfumo huo ungesambaratisha umoja ambao alikuwa amejenga kupitia Falsafa ya Nyayo, iliyohimiza Amani, Upendo na Umoja.

Ni kutokana na wasiwasi huo ambapo kauli yake ya “Siasa mbaya, maisha mbaya” ilitoka.

Mzee Moi anadaiwa kuamini kwamba mfumo huo ulitokana Umagharibi, ambapo ungekuwa kikwazo kikubwa kuiunganisha nchi.

Kwenye hotuba zake nyingi, Mzee Moi alipendelea kutumia Kiswahili, wadadisi wakisema kuwa hilo liliwiana na lengo la kutilia maanani dhana ya uzalendo miongoni mwa Wakenya.

Mtindo huo ndio umeshinikiza baadhi ya wabunge katika Bunge la sasa kama Mohamed Ali (Nyali) kuwaomba wenzao kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi wanapowasilisha hoja zao bungeni.

“Ili kukuza uzalendo na Uafrika, lazima tuwaige viongozi kama Mzee Jomo Kenyatta na Mzee Moi, ambao walijivunia sana kutumia Kiswahili kila mara walipotoa hoja zao ama kuwahutubia Wakenya,” akasema mbunge huyo kwenye mojawapo ya michango yake.