MOKUA: Haja ya kuteua kozi kwa kuzingatia vigezo vinavyostahiki
NA HENRY MOKUA
AWAMU nyingine ya kuteua kozi za kusomea kwenye vyuo vikuu na vya kadri imewadia.
Kwa mujibu wa tangazo la Huduma ya Usajili kwenye Vyuo Vikuu na vya Kadri Nchini, watahiniwa wa KCSE wa mwaka jana wana takriban juma moja unusu tokea sasa kutamatisha kutuma maombi. Ilivyo ada, kuku mgeni hakosi kamba mguuni.
Watahiniwa hao wana ndoto zinazopaa licha ya kwamba hawajayatimiza baadhi ya matakwa ya huduma husika ya usajili. Nimewaona wengine wakishikilia watasomea udaktari, uuguzi, licha ya kwamba alama zao zi chini mno.
Mwaka jana walipoelekezwa na kunasihiwa wengi wao walionekana kuridhishwa na hali zao za wakati huo wakatumaini kwamba zamu yao ya kufanya mtihani wa kitaifa ikiwadia, nyota ya rehema ingewaangazia. Kweli iling’aa, lakini si kiasi cha matazamio yao.
Unayejiandaa kuufanya mtihani wako wa kitaifa mwaka huu kumbuka wahitaji kujinyima kiasi cha haja ili uyafikilie matazamio yako kikamilifu.
Kwa kawaida, wanafunzi wengi walio katika madarasa na vidato vya nyuma huwaona wenzio ambao ni watahiniwa kama waliokosa kumakinika, kujiandaa. Wao hudumu kukariri hali zao zitakavyokuwa nzuri hadi wanapotanabahi kwamba muda wao umekwisha nao wapaswa kuwa watahiniwa.
Ndoto zao huanza kufifia wakaanza kujiliwaza kwa: ‘Hata waliofeli huishi vyema…si lazima mtu afanikiwe masomoni’.
Wanapoifanya mtihani wenyewe, mambo huwa yale yale – matokeo yao hukosa kuwaridhisha wala kuwafaa kujiunga na kozi wanazozimezea mate. Ili hali yako iwe tofauti, tafuta mashauri mapema na uyatie maanani.
Leo tunawalenga zaidi wanaonuia kusajiliwa kusomea kozi mbalimbali. Wachache waliojitahidi kadri ya uwezo wao hawana lolote la kujutia kwani wapo radhi kuteua kozi walizofuzu kusomea.
Waliofanya mzaha wataka wasomee kozi zile zile walizoota kuzihusu licha ya alama zao kuwa chini kiasi cha haja.
Hebu sikiliza usije ukajikwaa: ukiyatuma maombi ya kusajiliwa visivyo, tarajia kujikuta kwenye kozi ambayo hujawahi kuiwazia… Kwani unanilaani nini! La, nakunasihi tu kwamba matukio ya kihalisia yahitaji maamuzi ya kihalisia. Kwa hivyo nichukue hatua gani?
Ikubali hali halisi kwa moyo mkunjufu. Wakati mwingine mambo hutukia kinyume na yalivyo matarajio yetu. Ikiwa imefanyika hivyo kwako, jiliwaze na kuikubali hali yako ya sasa.
Labda umekuwa ukiomba na kutarajia kusomea uhandisi lakini umegundua alama zako hazikuruhusu; kubali kwamba hiyo ndoto haitatimia kwa sasa.
Sema na nafsi yako na uishawishi kukubali kwamba itabidi uchukue mkondo tofauti sasa. Kwa mfano, waweza kusomea digrii ya ukufunzi katika vyuo vya uhandisi – yaani, Bachelor of Technology Education badala ya uhandisi moja kwa moja.
Ikiwa ulikuwa na nia ya kusomea udaktari, yaani Bachelor of Medicine & Surgery na huyafikilii matakwa ya kimsingi au ya jumla, wazia kusomea uuguzi, yaani, Bachelor of Science (Nursing).
Ikiwa hufuzu kujiunga na taaluma ya ualimu – Bachelor of Education Science/ Arts, wazia kutuma maombi ya kusajiliwa kwenye Bachelor of Science/Arts with Education.
Tafuta nasaha taaluma. Wazazi wengi wanababaishwa na wanao kwamba madhali waweza kubonyeza vitufe vya simu, tableti au kompyuta, basi wanao uwezo wa kujikamilishia zoezi lenyewe.
Huku ni kujidanganya na kudanganyana kwa wakati mmoja. Taaluma si tukio bali harakati na huenda ukasalia katika taaluma moja tu aushini mwako.
Koma kuchukulia suala hili kimzaha kwa msingi huu. Tafuta nasaha kwa mtaalamu wa masuala ya taaluma ili akufae.
Ikiwa atakutoza ada kwa huduma hiyo, itoe bila kulalamika. Endapo waweza kumshawishi akupunguzie ada yenyewe, sawa; muhimu, msikilize akufae pamoja na mwanao katika kuufikia uamuzi bora zaidi kuhusu taaluma ya kuiteua.