Makala

MOKUA: Mfumo wetu wa elimu wapaswa kusisitiza stadi za maisha

January 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA HENRY MOKUA

Gharama ya maisha inazidi kupanda kila uchao nazo changamoto kuongezeka kwa kiwango sawa. Licha ya kila mwalimu na mzazi kutamani wana walio chini ya uangalizi wake ajiunge na chuo kikuu au cha kadri, wakati mwingine haiwezekani.

Kwa sababu ya vikwazo mbalimbali, wengine wanakosa kufikilia ngazi hizi. Hata wanaozifikilia huegemeza matumaini yao yote kwenye ajira wanayoitarajia baada ya kufuzu kisomo cha juu; lakini ni kwa kiasi gani wazo hili litasibu?

Miongoni mwa mambo yanayowachochea vijana wa jumuiya ya Wahafidhina kuiporomosha nchi yao kwa mujibu wa riwaya ya Chozi la Heri inayotahiniwa katika shule sekondari kwa sasa, ni elimu duni.

Wanadai kwamba ingawa wamepata shahada mbili au hata tatu, hawajapata ajira walizoahidiwa. Aidha, hawana stadi za kuwawezesha kujikimu kwani elimu waliyoipata ni ya kinatharia tu.

Kwa kuwa kazi za fasihi huakisi jamii halisi, huenda tunapitia changamoto karibu sawa na zilizoangaziwa katika riwaya hiyo. Je, twapaswa kuchukua hatua gani kukabiliana na hali hii tusije tukajikuta pale pale inapojipata jamii ya Wahafidhina?

Kwanza, uduni wa elimu waweza kutazamwa kwa namna mbili au tatu. Ya kwanza, ni mfumo wenyewe kuwa na dosari katika uandaaji wao hivi kwamba unakosa vipengele vya kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na hali halisi ya maisha tokea mapema.

Pili, wanaoutekeleza waweza kulegea na kukosa kuwaelekeza wanafunzi wao vilivyo, kuwapa stadi zinazostahiki. Tatu, wanafunzi wenyewe wanaweza kupuuza stadi hizi wakajifanya wajuaji wakitaraji mambo yatakuwa nywee. Katika kutatua changamoto hizi, pana haja ya kuanza panapo nafuu.

Hivi ni kusema kwamba tunapotaraji serikali ibadilishe mfumo wa sasa wa elimu, walimu na wanafunzi waweza kufanya marekebisho wanayoweza kuyamudu.

Walimu twapaswa kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwajia kabla ya, na wakati wa ajira zao. Vema zaidi, wanafunzi wanapaswa kuelekezwa kukuza vipaji vyao kadri iwezekanavyo kwani hamna ajuaye kipi miongoni mwavyo kitaweza kuwazumbulia riziki mwanzo.

Kusisitiza shughuli za darasani zinazolenga mitihani daima bila kuwazia uwezekano wa mitihani hiyo kutokuwa suluhu ya pekee kwao ni upungufu unaofaa kushughulikiwa.

Kuwaelekeza wanafunzi au watoto chini ya uangalizi wetu kutilia mkazo kisomo ni muhimu, lakini ni muhimu zaidi kuhusisha kisomo hicho na stadi mahsusi za kupambana na hali ngumu za sasa na za baadaye.

Wazazi pia tuna jukumu la kuwasisitizia wana wetu suala hili. Ili kuwa na vijana waliofinyangwa vilivyo kiakili, kisaikolojia, kiroho, kimhemko na kimwili, yatupasa kutengee vipengele vyote hivi muda.

Baadhi ya masuala ya kuwaandaa kuukabili ulimwengu ni yale yale yaliyo uraibu wao. Kwa hivyo tukiwaangalia kwa makini wanapokuwa nyumbani na kuchunguza masuala wayapendayo na yenye uadilifu, huenda tukagundua vipaji vyao na kwa kushirikiana na walimu twaweza kuwafaa wana wenyewe pakubwa.

Aliye na kipaji cha kuimba ahimizwe kukitumia vilivyo bila kuvuruga shughuli yake ya masomo. Aliye na kipaji cha kuigiza, kucheza kandanda, kusoma taarifa wazisomazo warideni, kunasihi na kadhalika, wote waongozwe kuvichukulia vipaji hivi kwa uzito bila kutatiza shughuli zao za masomo.

Ijapo wengi tunavidhalilisha vipaji hivi, inashangaza kwamba hatimaye wengine hata huasi ajira zao za kimsingi na kujikita katika vipaji hivi vilivyochipuka kama uraibu tu.

Mwisho, yachukulie kwa uzito uambiwayo na wakubwa zako ewe mwanafunzi.

Nimewaona wengi wakizichukulia kama mzaha jitihada za walimu kuwaelekeza kujiimarisha kupitia kwa klabu mbalimbali zilizomo shuleni.

Hata somo lenyewe la Stadi za Maisha lililoingizwa katika silabasi maksudi kukuandaa kukabiliana na changamoto kadha za maisha walichukulia hivi hivi? Ukome kabisa mkondo huo wa maisha na utaona mambo yakianza kukutengenea.