Akili MaliMakala

Mpango kuinua jamii za wafugaji

Na SAMMY WAWERU March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ZAIDI ya asilimia 80 ya ardhi ya Kenya inaorodheshwa kama jangwa na nusu-jangwa (ASAL), maeneo mbayo kwa kiasi kikubwa yanamilikiwa na jamii za wafugaji wa kuhamahama.  

Licha ya wakazi kutegemea ufugaji kujiendeleza kimaisha, jamii hizo zinakodolewa macho na changamoto za soko.

Gapu hiyo hata hivyo, huenda ikawa historia kufuatia mpango mpya kuwaboreshea miundomsingi ya soko ya mifugo wao.

Hii, ni kufuatia kuzinduliwa kwa African Pastoral Markets Development (APMD) Platform, mpango unaoendeshwa na African Union Inter-African Bureau for Animal Resources (AU-IBAR).

Ukipaniwa kulenga wafugaji wa kuhamahama Barani Afrika, mpango huo unatazamiwa kuweka mikakati maalum kuwatafutia masoko yenye ushindani mkuu.

“Sekta ya ufugaji Kenya na Bara Afrika kwa jumla ina uwezo mkuu kupiga jeki uchumi. Hata hivyo, mazingira ya sasa yananyima wafugaji mianya kufanikiwa,” akasema Dkt Huyam Salih, Mkurugenzi Mkuu AU-IBAR wakati wa uzinduzi wa mradi huo Jijini Nairobi.

Dkt Huyam Salih, Mkurugenzi Mkuu AU-IBAR. PICHA|SAMMY WAWERU

Ufugaji, ukitiliwa mkazo na kuboreshwa, utaleta mchango mkubwa kwenye kapu la pato jumla (GDP).

Kulingana na Dkt Salih, APMD inalenga kuangazia changamoto zinazozingira wafugaji wa kuhamahama, hususan kuboresha miundomsingi ya soko.

Mpango huo unafanyiwa majaribio Kenya – kuwakilisha Upembe wa Afrika na mataifa jirani, na Nigeria kwa niaba ya nchi za Afrika Magharibi na eneo la Sahara.

Mpango wa APMD umeasisiwa kwa nguzo tatu; kufanya mabadiliko ya sheria, ukusanyaji data za mifugo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha sekta ya kibinafsi kujiunga na wadauhusika kuinua jamii za wafugaji wa kuhamahama.

“Kwanza, tunatathmini sheria zilizopo na kupendekeza mpya, zitakazohakikisha wafugaji wa ASAL wanatambuliwa,” Dkt Salih akaelezea.

Kuwepo kwa jukwaa la data za mifugo, ni hatua kubwa itakayosaidia kufungua mianya ya ufanisi, ili kuhakikisha mifugo na bidhaa zake zinaafiki sheria za taifa, kikanda na za kimataifa.

Dkt Salih alifafanua haja ya ushirikiano na sekta ya kibinafsi, akisema ni nguzo kuu kuleta mafanikio katika sekta ya mifugo – ambayo ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi.

Nchini Kenya kwa mfano, sekta ya ufugaji huchangia asilimia 12 kwa GDP moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwa mujibu wa data za 2024 za Idara ya Ufugaji inayohudumu chini ya Wizara ya Kilimo na Ustawishaji Mifugo.

Eneo la ASAL linachangia pakubwa katika uzalishaji wa nyama.

Mradi wa APMD utagharimu kima cha Dola za Amerika 5.3 milioni (Sawa na Sh686.35 milioni thamani ya Kenya), na utafadhiliwa na Wakfu wa Gates, ndio Gates Foundation.

Utaendelezwa kwa kipindi cha muda wa miaka mine.

Dkt Christopher Wanga, Mkurugenzi wa Utafiti wa Sheria za Mifugo na Udhibiti, alisema malengo ya APMD yanaenda sambamba na mikakati ya serikali kufufua sekta ya mifugo.

Dkt Christopher Wanga, Mkurugenzi wa Utafiti wa Sheria za Mifugo na Udhibiti, katika Wizara ya Kilimo na Ustawishaji Mifugo. PICHA|SAMMY WAWERU

Kwa sasa, serikali inashughulikia mpango unaopania kukusanya data za mifugo, wakiwemo kuku na ndege wa nyumbani, unaojulikana kama National Livestock Master Plan.

Isitoshe, mpango huo vilevile unajumuisha teknolojia ya kutambua iliko mifugo, Dkt Wanga akisifia hatua hiyo kuwa itasaidia kuboresha miundomsingi ya masoko katika ngazi za kimataifa.

Ukosefu wa data za mifugo ungali changmoto kuu Barani Afrika, ukizuia serikali kuwa na mikakati bora kuboresha sekta.

“Kujua idadi kamili ya mifugo – ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, na hata ngamia, kutasaidia kulainisha utoaji huduma na kuboresha soko,” akasema Dkt Wanga.

Kwa sasa, serikali inaendeleza zoezi la utoaji chanjo za maradhi ya FMD na Foot Peste des Petits Ruminants (PPR), hatua inayotajwa kwamba itasaidia nyama za mifugo wa Kenya kuwahi masoko ng’ambo.

“APMD imejiri wakati ufaao, na itawezesha bidhaa zetu zionekane ughaibuni. Miaka miwili ilyopita, tulianza kuandikisha wakulima kwa minajili ya usambazaji wa mbolea ya bei nafuu, ni muhimu wafugaji pia wasajiliwe,” akasisitiza Dkt Wanga.

Kulingana na takwimu kutoka Idara ya Mifugo, idadi ya ng’ombe wa maziwa nchini inakadiriwa kuwa milioni 5.1.

Waziri wa Mifugo Nigeria, Idi Mukhtar Maiha. Mpango wa APMD pia unatekelezwa nchini Nigeria. PICHA|SAMMY WAWERU

Mwaka 2023, uzalishaji wa maziwa ulikadiriwa kufikia lita bilioni 5.2, zenye thamani ya Sh312.7 bilioni.

Idadi ya ng’ombe wa nyama ni karibu milioni 16.3.

Mwaka wa 2023, Kenya ilizalisha tani 237,907 za nyama za ng’ombe zenye thamani ya Sh129.5 bilioni.

Kondoo na mbuzi ni sehemu muhimu ya usalama wa chakula na mapato kwa jamii za wafugaji kutokana na muda wao mfupi wa uzazi, uwezo wao mkubwa kuhimili mazingira tofauti, na hulka yao kula aina mbalimbali za malisho.

Kenya inakadiriwa kuwa na mbuzi milioni 34.9 na kondoo milioni 23.2, ambapo 2023 nchi ilizalisha tani 77,521 za nyama za mbuzi zenye thamani ya Sh53.9 bilioni na tani 51,691 za nyama za kondoo zenye thamani ya Sh34.2 bilioni.

Vilevile, nchi ilizalisha tani 93,622 za nyama za kuku kutoka kwa kuku milioni 68.9, uzalishaji wenye thamani ya Sh34.7 bilioni, tani 40,055 za nyama za nguruwe kutoka kwa nguruwe wapatao 840,160 zenye thamani ya Sh19.5 bilioni, na tani 55,204 za nyama za ngamia kutoka kwa ngamia milioni 4.3, uzalishaji wenye thamani ya Sh32.5 bilioni, pamoja na bidhaa nyinginezo za mifugo.