Mpasuaji wa maiti yuko wapi? Familia za waliouawa Saba Saba zalia
FAMILIA tatu kutoka Kaunti ya Kirinyaga zinapitia masaibu tele katika juhudi za kuwazika wapendwa wao waliopigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya Saba Saba.
Familia hizo zimeshindwa kuwapa wapendwa wao mazishi ya heshima kwa sababu serikali haijatoa wataalamu wa upasuaji wa maiti.
Mazishi hayo yamekuwa yakiahirishwa mara kwa mara, hali inayoongeza majonzi na uchungu kwa familia hizo.
Familia ya marehemu Ndambiri ni miongoni mwa zilizoathirika, ambapo mwili wake umehifadhiwa katika mochari ya Kibugi baada ya daktari wa serikali kukosa kufika kufanya uchunguzi wa maiti.
Mnamo Julai 7, 2025, Ndambiri, 25 alipatwa na risasi kichwani polisi walipokuwa wakikabiliana na waandamanaji, yeye akiwa amesimama eneo moja la wazi mjini Kutus, Kaunti ya Kirinyaga, akitazama kilichokuwa kikiendelea.
Alikuwa akifanya kazi za vibarua, na siku hiyo, alikuwa ametoka kazini baada ya duka lake kufungwa kufuatia maandamano hayo.
Mjombake Karimi pamoja na waendeshaji bodaboda walimkimbiza katika hospitali ya kibinafsi iliyo karibu, lakini alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Risasi ilimpiga paji la uso na kutokea nyuma ya kichwa, hakuwa na nafasi ya kupona. Alifariki siku hiyo hiyo jioni,” alisema Bw Karimi.
Mwili wa Ndambiri bado uko katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Kibugi huku familia ikijaribu kukubaliana na msiba huo mzito.
Katika eneo la Makutano, familia ya James Muriithi, 41, ambaye pia alipigwa risasi wakati wa maandamano, bado haijamzika kwa sababu hiyo hiyo ya kukosa daktari wa upasuaji wa wa serikali.
“Sababu kuu ya kutomzika Muriithi ni kukosekana kwa daktari wa serikali,” alisema Bw Benson Mwangi, nduguye marehemu. Familia hiyo ilisema Muriithi alikuwa akifanya shughuli zake mjini Makutano alipopigwa risasi.
“Polisi waliokuwa na mori walikuwa wakifyatua risasi kiholela na ndipo risasi ilimpata kijana wetu. Alikimbizwa katika hospitali ya White Rose na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Kenyatta ambako alifariki baada ya siku mbili,” alisema Bw Mwangi.
Mjini Kerugoya, mazishi ya Peter Macharia yalifutwa baada ya mpasuaji maiti wa serikali kukosa kufika katika mochari ya hospitali ya rufaa ya Kerugoya kufanya uchunguzi wa maiti.
“Macharia alitarajiwa kuzikwa Jumatano. Tulikuwa tumechimba kaburi lakini tukashangazwa daktari wa serikali alipokosa kufika,” alisema Bw Hezekiah Kang’e, mwakilishi wa familia.
Macharia alipigwa risasi na polisi wakati wa maandamano na kujeruhiwa vibaya. Alifariki siku hiyo hiyo alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kerugoya Level 5.
Mama yake, Bi Margaret Wainoi, alisema mwanawe alikuwa mjini aliponaswa na maandamano na kupigwa risasi na polisi waliokuwa wakikabiliana na waandamanaji.
“Nikiwa nyumbani nilipokea habari kuwa mwanangu amepigwa risasi na kupelekwa hospitalini. Nilipofika nikakuta amefariki,” alisema.