Akili MaliMakala

Mradi wa kustaafu wa ng’ombe wa maziwa unaniingizia Sh300, 000 kwa mwezi 

Na SAMMY WAWERU August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NEMUEL Mbicha, 75, kutoka Kaunti ya Kisii, pamoja na mkewe Nyaboke Mbicha, 71, walianza kupanga maisha yao ya baada ya kustaafu pindi tu walipopata ajira na kufunga ndoa.

Mbicha alioa akiwa bado kijana mdogo wa umri wa miaka 24, na anasema walifahamu umuhimu wa kuanza kujiandaa kwa maisha ya uzeeni mara tu walipopata ajira.

Wakati huo, Mbicha alikuwa afisa wa watoto katika Ofisi ya Makamu wa Rais, huku mkewe akifanya kazi kama karani katika idara mbalimbali za serikali.

Miaka kadhaa baadaye, mwaka wa 2000, baada ya kuweka akiba kwa muda mrefu, walifanya uamuzi wa kununua kipande cha shamba kama sehemu ya mpango wao wa kustaafu.

Nemuel Mbicha na mkewe wakifuatilia ng’ombe wao wa maziwa wanavyoendelea. Picha|Sammy Waweru

“Tulinunua ekari tano eneo la Joska kila moja tukiuziwa Sh80, 000,” anafichua Mzee Mbicha, ambaye pia ni kiongozi wa kanisa.

Shamba hilo lipo kilomita moja kutoka Kangundo Road, karibu na barabara inayounganisha Joska na Mombasa Road.

Wakati huo, eneo analoishi lilikuwa kame, lisilo na maendeleo, na lilijulikana kuwa hatari kutokana na wanyamapori kama nyoka, fisi na pundamilia.

Zaidi ya hayo, eneo hilo linaloorodheshwa kama jangwa na nusu-jangwa (ASAL), upatikanaji wa maji ulikuwa changamoto kubwa.

Mwaka wa 2006, walihamia kwenye ardhi waliyonunua baada ya kujenga nyumba, na hapo ndipo walianza kuiboresha.

Mwaka mmoja baadaye, Mbicha anadokeza kwamba walikopa Sh490, 000 kutoka kwa shirika la kifedha, mtaji waliotumia kujenga zizi la mifiugo na kununua ndama sita aina ya Friesian.

Mzee Nemuel Mbicha na ng’ombe wake aina ya Friesian. Picha|Sammy Waweru

Hata hivyo, baadaye walipoteza ng’ombe hao waliofariki kutokana na maradhi ya East Coast Fever.

Mbicha anasema changamoto hiyo haikuwavunja moyo, bali iliwapa motisha na kuendeleza safari kuafikia ndoto zao.

Mkewe anakumbuka jinsi alivyopanua mradi wao wa ng’ombe wa maziwa hadi Eldoret baada ya kuhamishiwa humo kikazi, ambako alikuwa akisambaza maziwa kwa idara mbalimbali za serikali na pia kwa wafanyakazi wenzake.

Kufuatia mafanikio waliyopata, Bi Mbicha aliamua kustaafu mapema ili kuboresha mradi wao.

“Nilistaafu nikiwa na umri wa miaka 46,” anafichua.

Hifadhi ya malisho ya Nemuel Mbicha. Picha|Sammy Waweru

Miaka 18 baadaye, mradi wao wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa umeimarika na kuwanufaisha kwa kiasi kikubwa.

Kwa sasa wana zaidi ya ng’ombe 40, mbuzi asilia kwa ajili ya nyama, pamoja na kuku wa kienyeji, bata na batamzinga wanaozunguka huru shambani mwao.

Ekari moja imetengwa kwa ajili ya kusitiri ng’ombe, huku sehemu nyingine ikiwa na bustani ya mseto wa matunda.

Zizi la ng’ombe, sakafuni limeundwa kwa saruji, na paa za mabati, ng’ombe wao wakijivunia huduma bora ikiwemo kuburudishwa kwa redio wanapokamuliwa na pia kulishwa.

Mbicha anadokeza kuwa kwa sasa, wanakama ng’ombe 20, ambao huzalisha wastani wa lita 250 hadi 300 za maziwa kwa siku, ingawa wakati wa kiangazi kiwango hicho hupungua hadi lita 200.

Maziwa ya Mzee Mbicha yakipimwa tayari kuchukuliwa na kampuni ya New KCC. Picha|Sammy Waweru

Huyauza kwa kampuni ya New Kenya Cooperative Creameries (New KCC), wakilipwa Sh50 kwa kila lita.

Wanandoa hao pia huuza ng’ombe wanapozaana kwa wingi.

Ndama mmoja huuza Sh70, 000, huku ng’ombe aliyekomaa akigharimu zaidi ya Sh200, 000.

Wanamiliki ekari nne karibu na mto wa Athi, ndio Athi River ambako hulima majani ya mifugo yanayohifadhiwa kama silage na hay.

Wana mashine kuunda malisho ya mifugo. Msimu wa kiangazi na ukame, hutegemea maji ya kisima walichochimba ambapo maji hupampiwa kwa kutumia nguvu za kawi – sola.

Mfanyakazi wa Mzee Mbicha akisaga malisho kwa mashine aina ya Chaff Cutter. Picha|Sammy Waweru

Tumekumbatia mifumo ya mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji, Mzee Mbicha akaambia Akilimali wakati wa mahojiano.

Kwa upande wake Bi Mbicha, anasema mifugo wao humtuliza moyo na kumpa furaha – akiwafananisha na daktari.

Aidha, wameajiri vijana kadhaa wanaowasaidia kazi za mradi huo, na huduma huanza saa kumi asubuhi kwa kusafisha makazi ya mifugo na vifaa vya malisho na maji.

Maziwa hukusanywa kuanzia saa nane mchana na New KCC, na wana majokofu kuyahifadhi.

Mbicha anashauri vijana kuanza kujipanga mapema kwa minajili ya maisha ya uzeeni.

Mzee Mbicha pia hufuga mbuzi na mafahali wa nyama. Picha|Sammy Waweru