Makala

Msamaha na kupuuza porojo ni msingi wa ndoa ya kudumu, mshauri wa ndoa asisitiza

Na BENSON MATHEKA September 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ULIMWENGU umejaa talaka  na hii imefanya watu kuchukia na kuogopa ndoa. Vijana wanataka mahusiano ya muda mfupi, bila kujifunga, wasitumbukie katika masononeko wanayoshuhudia watu walio katika ndoa wakipitia.

Lakini ndoa inaweza kukingwa dhidi ya talaka na hii inahitaji mchango wa wachumba wote wawili. Wawili tu, kwa kuwa mtu wa tatu anaweza kuwa sumu katika ndoa.

Anza na kutambua umuhimu na thamani ya mawasiliano katika ndoa. Bila mawasiliano ya dhati ndoa haiwezi kustawi na hii ndiyo sumu kali ambayo watu hualika kuua ndoa.

Usitarajie mke au mumeo kusoma yaliyo ndani ya moyo wako. Tenga muda wa kuketi na kuzungumza na mchumba wako. Mnapozungumza mara nyingi, ndivyo mnavyokaribiana. Mazungumzo haya yanafaa kuwa ya roho safi hata mkitofautiana.

 Kuna mada nyingi ambazo wanandoa wanaweza kuzungumzia. Mnaweza kuzungumzia kuhusu Mungu, mapato, miradi, matarajio, kazi, watoto, maisha ya ngono na burudani bora msigombane.

Kukosea na kukosewa ni kawaida katika ndoa lakini thibiti hasira zako. Kutokuwa mwepesi wa hasira ni kinga ya ndoa dhidi ya talaka. Kwa hakika,  chanzo cha talaka nyingi ni hasira.

Uwezo wa mtu wa kuthibiti hasira ni muhimu sana. Ukikosa kuthibiti hasira yako, usitarajie kudumisha uhusiano wowote wa kimapenzi. Ukikosewa na mtu wako, msamehe na uepuke kulipiza kisasi. Watu wengi wamesambaratisha ndoa zao kwa kulipiza kisasi makosa wanayotendewa na wachumba wao. Mojawapo ya kinga thabiti ya ndoa ni kusamehe na kuepuka kisasi.

 “Iwapo unataka ndoa idumu hadi kifo kiwatenganishe, iliyokolea raha na  amani, kusameheana ni lazima kwa kuwa ni lazima mchumba wako atakukosea mara nyingi tu. Bila msamaha,  ndoa haiwezi kudumu,” asema mshauri wa wanandoa Samuel Femi.

Kukosa kusamehe kunazaa machungu, hasira na hujuma katika ndoa. Kunaharibu amani nyumbani na kuvua familia furaha. Kunabomoa upendo na kuzua vurugu. Unaweza kukinga ndoa yako kwa kusamehe mchumba wako mradi tu vitendo vyake haviweki maisha yako katika hatari. “ Hii ni sawa na bima ya ndoa,” asema Femi.

Tambua kuwa ndoa ni baina ya watu wawili; wewe na mtu wako. Usiruhusu mtu wa tatu aitawale. Ukitaka ndoa yako inawiri, ikinge isivamiwe na watu kutoka nje ambao wanaweza kuwa hata wale wa karibu nawe.

Watu kutoka nje huwa wanasababisha migogoro katika ndoa. Jitenge na mtu au watu wanaoonyesha dalili za kukufanya utofautiane na mtu wako. Mpende mchumba wako zaidi ya mtu mwingine yeyote yule.  Ni ubavu wako, usikubali mtu akutenganishe nao. Ataua ndoa yako.