Makala

Msanii azidisha mjadala kuhusu ufaafu wa minisketi

June 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MSANII Ng’ang’a wa Kabari akitumia lugha ya Gikuyu ana ujumbe kwa akina dada walio na mazoea ya kuvalia nusu uchi.

Anasema kuwa isipokuwa ni vile sheria hapa nchini zimeundwa za kuwalinda kina dada wanaovalia sawa na karibu na uchi, angewajibikia suala la kuwa askari wa kuwarejesha hadi kwa mavazi nadhifu.

Ukatili wa hizo sheria ni kwamba, katika harakati za kujigeuza kuwa nyapara wa mavazi ya wanawake mitaani na uingiwe na pepo wa kumtoa hilo vazi unalofikiria linakera, ukinaswa na upatikane kwa hatia utafungwa kifungo cha miaka 20 gerezani.

Katika kuandikisha taarifa yake ya kulalamika, akisema kuwa ulimwibia hata shilingi moja tu katika hizo harakati za kumvua nguo, basi kosa linageuka kuwa wizi wa kimabavu ambapo hukumu ni kifo au maisha gerezani.

“Kwa kuwa sheria ziko, za kutuhukumu miaka 20 ndani tukijaribu kuwashinikiza mvae nadhifu, hata mna kaulimbiu ya ‘vazi langu chaguo langu’, basi sina lingine la kufanya bali kuwarushia tu ushauri wangu kupitia wimbo,” anasema msanii huyu.

Ng’ang’a wa Kabari.

Katika kanda yake ya video ya wimbo huo ukifahamika kama Ukari Muhithe (Uchoyo uliofichwa) anaagiza wanawake wawe wa kuficha sehemu zao za siri ili kuwaweka wanaume tamaa ya uhakika ya kutaka kujua ni nini hasa wameficha.

Katika kanda hiyo, anatumia picha za kusisimua bongo na hisia za wanawake wakiigiza mateso kwa wanaume ambapo mada inaonyesha jinsi ambavyo wanaume wanachachawika mitaani wakila kwa macho.

“Ukianika, basi umegeuka kuwa nyama ya umma ambapo hata mwewe akitaka kipande cha nyama hiyo, atatua tu na kunyakua,” anasema.

Anawaomba kina dada: “Hata ikiwa ni kuvaa ndio mtusukume sisi wanaume kwa maamuzi ya kuangamia; tuangamizeni polepole kwa kuwa hata ninyi hamutaishi milele.”

Anasema kuwa wahudumu wa bodaboda ndio wako kwa moto mkuu wa maangamizi kutoka kwa mitindo ya mavazi ya hawa wanadada ambapo “ukiwa mteja wa huyo mwanadada na ukiwa na minisketi ambayo urefu wake ni sawa na ule wa koti, kisha ukishakalia kiti cha pikipiki yake unamkumbatia na mapaja…

“Joto mbovu la mapaja linamkaba kisawasawa na kwa wakati wote wa safari mawazo yake hayako kwa barabara bali yako kwa yanayomfanyikia mwilini….ajali ndiyo hiyo na mnaaga dunia nyote wawili…au akishafanikiwa kimiujiza kukufikisha salama, kiungo chake kiko sawa na kutingisha kidole juu ishara ya ufuasi wa chama cha kanu, wima wa mlingoti,” anasema.

Anasema kuwa mavazi hayo ndiyo yamewafanya vijana wengi wasifanye maamuzi ya kuoa “kwa kuwa kile mtu hutamani akisaka mchumba wa kuoa, kilianikiwa wote nje kila siku kitazamwe na kinyonyezwe kiasi kwamba tamaa ya hicho kitu imewatoka wengi kwa kuwa wamezoea kukiona…”

Anakuuliza ewe mwanadada wakati umevalia za ufupi kila mahali ya kuanika kote uko nako, na unahitajika ghafla kuinama labda ukiwa umeangusha kitu ambacho huwezi ukakiacha nyuma, utajihisi namna gani?

“Umeinama na nyuma unaonyesha dunia nzima kusikofaa kuonwa… Urembo uliodhania unasambaza kwa umma unageuka kuwa aibu, laana na hata kwa watoro wa ustaarabu, kichapo,” anasema.

Anakuonya kuwa urejelee Biblia na upatane na kisa cha mwanamke Jezebeli ambaye alikuwa mtundu wa kimaadili kiasi kwamba alipoaga dunia, Mungu aliwapa ushawishi wa kutupa mwili wake kwa majibwa.

Anaambia hawa kina dada kuwa wanaume wengi wamepevuka kiasi cha kuelewa kuwa chochote kizuri huwa kimefichwa na hakianikwi ovyoovyo.

Anasema: “Ushawahi kumbana na dhahabu ikiwa imewekwa kandokando mwa barabara? Ikiwa hata ng’ombe hujua kuficha na mkia usiri wake nyuma!”