MSHAIRI WETU: Joel Odhiambo almaarufu Mwana Wa Nyoka
Na CHRIS ADUNGO
NYOTE ambao hamjapiga mbizi katika bahari ya ushairi na fasihi kwa jumla, na mnajivunia kipaji cha utunzi, basi mnakosa mengi matamu.
Maisha si maisha bila Jalali kuwa mwamuzi mkuu wa mkondo wa maisha ya binadamu. Yeye ndiye mwamuzi mkuu. Ukiwa naye, chombo kitaelea salama hata kukiwa na dhoruba kali.
Tueleze kwa ufupi kukuhusu
Jina langu ni Joel Odhiambo. Wanaonijua kwa kipaji changu cha utunzi na kukariri mashairi huniita Mwana wa Nyoka. Nilizaliwa katika gatuzi la Nyandarua mnamo Juni 15, 1994. Kwa kudura za Mwenyezi Mungu, nililelewa na wazazi wangu na nikasomea huko hadi kitumbua kilipoingia mchanga mnamo 2007.
Kwa kuwa wino wa Mungu haufutiki na kalamu yake haikosei, nilipiga hatua zilizonisogeza mbele licha ya kuonja asali na shubiri katika maisha. Panda-shuka za kila sampuli ni kati ya mambo yaliyonikomaza.
Ulisomea wapi?
Nilianza masomo ya chekechea katika Shule ya St Mary’s Nyahururu. Mnamo 2000, nilijiunga na Shule ya Msingi ya Ninty One Mnicipality Nyahururu. Kati ya mwaka wa 2008–2011, nilisomea katika Shule ya Wavulana ya Tenges, Baringo na hatimaye nikajiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea ualimu (Kiswahili na Dini).
Nani na nini kilikuchochea kuupenda ushairi?
Nina uraibu wa kusoma mashairi na kusoma mashairi katika gazeti hili la Taifa Leo, diwani za waandishi mbalimbali kama vile Said. A. Mohamed, kuwasikiliza magwiji wa ushairi kama vile Victor Mulama wakighani redioni na waandishi wenzangu wanaoibuka kumenipa hamasa ya kuyapenda mashairi.
Ulitunga lini shairi lako la kwanza?
Mnamo 2013 na nikalipa mada ‘Nchi ya Ruwaza’.
Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?
Hugusia masuala kama vile ufisadi, siasa, mapenzi, elimu na jambo lolote muhimu ambalo linawamhusu binadamu wa kawaida katika jamii.
Nini hukuongoza kuteua mada hizo?
Matukio mbalimbali katikia jamii na mambo ambayo huteka hisia zangu kimakusudi au ghafla tu.
Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?
Muda wa dakika 50 hivi hunitosha kutiririsha shairi la tarbia lenye beti saba au nane hivi.
Mbona mashairi yako ni ya arudhi?
Mashairi ya arudhi huwa na mahadhi ambayo huvutia na kumpa mtunzi, msomaji na msikilizaji mshawasha na hamu ya kutaka kujihusisha na mashairi ya sampuli hii ambayo yana uwezo wa kuimbwa kirahisi kwa mahadhi mbalimbali.
Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?
Ingawa hutekeleza majukumu mbalimbali katika jamii, mashairi haya hayana mnato unaopatikana katika tungo za kiarudhi. Hata hivyo, cha msingi mno ni ujumbe kufikia wapenzi wa sanaa.
Ushairi umekuvunia tija ipi?
Lakabu ‘Mwana wa Nyoka’ imenipa umaarufu miongoni mwa wenzangu katika ulingo wa ushairi. Katika chuo kikuu, nyumbani na shuleni ninakotagusana na wanafunzi wengi, huwa navuliwa kofia kutokana na umahiri wangu katika ushairi.
Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na ushairi wako?
Ndio. Nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi na upili, nilituzwa kwa kuibuka bora zaidi katika vitengo mbalimbali vya kughani mashairi. Katika chuo kikuu, nilituzwa mara si moja kwa utunzi na uimbaji wa mashairi.
Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi na makuzi yake?
Hiki ni kipaji kutoka kwa Maulana. Wito wa Mungu haukatiliwi. Kila niamkapo naona mwangaza, najua ipo siku nitakapoandika diwani pamoja na marafiki wanaokichapukia Kiswahili. Sina shaka kwamba itakuwa diwani ambayo itamulika jamii na kuendeleza makuzi ya fani hii.
Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?
Mimi ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Wavulana ya Litein, Kericho.
Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako katika taaluma ya ushairi?
Chipukizi wasije wakabeza hatua ndogo wanazozipiga kitaaluma kwa kuwa safari huanza kwa hatua.
Pia wawe tayari kuwasikiliza waliowatangulia ulingoni. Nawahimiza washairi wa zamani wasichoke kutushika mkono na kutufunza kusimama.