MSHAIRI WETU: Nashon Kibet Domongole almaarufu Malenga Mbarikiwa
Na CHRIS ADUNGO
KUPATA si kwa werevu na kukosa si kwa ujinga.
Kila jambo hutokea katika maisha ya binadamu kwa sababu. Kujituma katika chochote unachokishughulikia ndio msingi wa maendeleo. Hatua ndogo mwishowe huwa kubwa! Huu ndio ushauri wa mshairi Nashon Kibet Domongole almaarufu Malenga Mbarikiwa.
Tueleze kwa ufupi kukuhusu
Nilizaliwa mnamo Februari 13, 2000, katika kijiji cha Chepinat, kata ya Lelan, eneo la Pokot Kusini nikiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw Paul Domongole na Bi Josephine Domongole.
Mimi ni Mkristo anayependa kukuza vipaji vya chipukizi wenzangu kisanaa na kujishughulisha na mambo yanayochangia maendeleo ya jamii.
Ulisomea wapi?
Safari yangu ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Goodwill Academy katika eneo la Lubao, Kaunti ya Kakamega. Nilisomea huko kati ya 2004 na 2012 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili Chewoyet Boys, Pokot Magharibi mnamo 2013. Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST), Kakamega mnamo 2017 kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Historia). Mimi kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu.
Nani na nini kilikuchochea kuupenda ushairi?
Penye nia pana njia. Ari ya kukichangamkia Kiswahili ni zao la kusoma kazi nyingi za fasihi. Mbali na mazingira nilimolelewa kunipa msukumo wa kutaka sana kujihusisha na Kiswahili, wazazi wangu walichangia pakubwa katika kunihimiza baada ya kutambua mapema sanaa ya utunzi iliyoanza kujikuza ndani yangu tangu utotoni.
Ulitunga lini shairi lako la kwanza?
Mnamo Septemna 2017.
Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?
Hujadili matatizo ya mara kwa mara ambayo huwakabili wanajamii, masuala ya uchumi, jinsi ya kuimarisha kilimo, uhifadhi wa mazingira na ujenzi wa jamii mpya katika taifa lenye nguvu-kazi kubwa kutoka kwa vijana.
Nini hukuongoza kuteua mada hizo?
Mitazamo binafsi, hisia za watu mbalimbali kuhusiana na masuala ibuka katika jamii na utafiti wangu kuhusu matukio ya mara kwa mara ninayoyashuhudia.
Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?
Kati ya dakika 10 na saa moja kutegemea uzito wa mada husika na aina ya shairi. Ufupi au urefu wa muda ninaohitaji pia hutegemea utulivu wa mawazo.
Mbona mashairi ya arudhi?
Mashairi ya arudhi huvutia nadhari ya watu hasa kutokana na mapigo ya sauti za kimuziki, urari wa vina na mizani. Isitoshe, uwezo wa kutunga mashairi ya sampuli hii huwa kipimo halisi cha ukomavu wa mtunzi.
Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?
Mchele mmoja mapishi mbalimbali! Mashairi haya pia yana nafasi kubwa katika makuzi na maendeleo ya Fasihi ya Kiswahili.
Ushairi umekuvunia tija ipi?
Umenifanya maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wenzangu. Hakuna tuzo kubwa zaidi kuliko jumbe za pongezi na za kumotisha ambazo mimi hupokea kila mara mashairi yangu yanapochapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo. Gavana wa Pokot Magharibi, Profesa John Lonyangapuo aliwahi kunihongera si haba baada ya kumkariria shairi katika mojawapo sherehe alizohudhuria.
Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?
Napania kuwakuza washairi wanaoinukia katika fani hii na pia kuchapisha diwani itakayobadilisha sura ya kusomwa na kufundishwa kwa ushairi wa Kiswahili katika shule za upili za humu nchini.
Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?
Nipo katika kundi moja la waigizaji na pia hutoa ushairi nasaha kwa vijana wenzangu.
Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?
Nawasihi chipukizi kujituma zaidi na wasome kazi nyingi za fasihi ndipo wakomae kisanaa. Nawahimiza washairi wa zamani wazidi kutushika mikono na kutuelekeza ipasavyo.